Felix Tshisekedi ameshinda uchaguzi wa urais nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Tume ya uchaguzi imesema Matokeo ya awali yanaonyesha mgombea huyo wa upinzani amemshinda mgombea mwingine wa upinzani Martin Fayulu, pamoja na mgombea aliyekuwa anaungwa mkono na serikali Emmanuel Shadary.
Mkuu wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Ceni) Corneille Nangaa, alisema mapema Alhamisi kwamba Bw Tshisekedi alipata asilimia 38.57 ya kura zilizopigwa na anatangazwa mshindi wa urais mteule.
Saa chache baada ya Tume ya Uchaguzi kumtangaza Tshisekedi mshindi, baadhi ya maeneo yalikumbwa na machafuko, ambayo yamesababisha watu 11 kupoteza maisha na wengine kadhaa kujeruhiwa.
Polisi wanasema,watu sita wamepoteza maisha katika mji wa Kikwit, katika mkoa wa Kwilu, mashariki mwa mji wa Kinshasa, na wengine wengi kujeruhiwa .
Tshisekedi alipata zaidi ya kura 7 milioni naye Bw Fayulu akapata kura takriban 6.4 milioni, huku mgombea wa serikali Emmanuel Ramazani Shadary akipata takriban kura 4.4 milioni.
Bw Fayulu ameyapinga matokeo hayo yaliyotangazwa na tume ya taifa ya uchaguzi.
Bw Tshisekedi, kwa upande wake ameyafurahia matokeo hayo na kumsifu pia rais anayeondoka Joseph Kabila.
Akiwahutubia maelfu ya wafuasi wake waliokusanyika mji mkuu Kinshasa, Tshisekedi amesema atakuwa rais wa raia wote wa Congo.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |