Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini ametangaza kuwa, kutokana na mwelekeo mzuri wa udhibiti wa maambukizi ya virusi vya Corona, nchi hiyo itazidi kupunguza hatua za vizuizi kuanzia tarehe 20 mwezi huu, na kurejesha safari za ndege za kimataifa kutoka na kwenda nchi zenye hatari ya chini ya maambukizi kuanzia tarehe Mosi Oktoba.
Akihutubia taifa kwa njia ya televisheni, Rais Ramaphosa amesema, tangu mlipuko wa maambukizi ya virusi vya Corona ulipotokea mwezi Machi mwaka huu, Afrika Kusini imepambana na janga hilo kwa ushirikiano, na hali ya maambukizi nchini humo kwa ujumla imeonesha mwelekeo wa kupungua.
"Katika miezi sita ya mwanzo ya mwaka huu tangu janga hili kuripotiwa nchini Afrika Kusini, wananchi zaidi ya laki 6.5 wamethibitishwa kuambukizwa virusi vya Corona, na zaidi ya watu elfu 15 wamefariki kutokana na janga hilo. Miezi miwili iliyopita, wastani wa idadi ya maambukizi ulikuwa elfu 12 kwa siku, na sasa idadi hiyo imepungua na kufikia chini ya elfu 2, na kiwango cha uponaji kimeinuka na kufikia asilimia 89. "
Kutokana na mwelekeko huo mzuri, rais Ramaphosa ametangaza kuwa, kuanzia tarehe 20 mwezi huu nchi hiyo itazidi kupunguza hatua za vizuizi na kupunguza kiwango cha karantini hadi kuwa cha chini zaidi. Pia kuanzia siku hiyo, muda wa kupiga marufuku kutembea usiku utazidi kupungua, na mawasiliano, mikusanyiko ya mambo ya kidini na kisiasa vitarejeshwa kwa kiasi. Mbali na hayo Afrika Kusini itafungua tena sehemu za mpaka hatua kwa hatua kuanzia Oktoba Mosi, na kurejesha utalii wa kimataifa.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |