3: Uchumi wa China

Hali ya Jumla ya Miundo ya Uzalishaji

Miundo ya uzalishaji ni uhusiano wa moja kwa moja wa uwiano na muundo wa vitu muhimu vya uzalishaji mali kati ya sekta mbalimbali za uzalishaji mali. Uhusiano huo hasa upo katika sekta tatu za uzalishaji mali za kilimo, viwanda na utoaji huduma pamoja na uhusiano wa uwiano ndani ya sekta hizo.

Tangu China mpya iasisiwe mwaka 1949, muundo wa sekta za uzalishaji mali ulipita katika vipindi vitatu vya maendeleo: Kipindi cha kwanza ni kati ya mwanzoni mwa miaka ya 50 ya karne iliyopita na mwishoni mwa miaka ya 70, ambapo China ilibadilisha hali ya uchumi wa nusu koloni na kuweka msingi wa viwanda. Kipindi cha pili ni kutoka mwaka 1979 hadi mwanzoni mwa miaka ya 90 ya karne iliyopita, China ilitekeleza sera za mageuzi na kufungua mlango kwa nje na kurekebisha miundo ya sekta za uzalishaji mali, ili kuiwezesha China kuingia kipindi cha kati cha maendeleo ya viwanda. Kipindi cha tatu ni kuanzia mwanzoni mwa miaka ya 90 ya karne iliyopita, China ilipoweka lengo la kujenga utaratibu wa uchumi wa kimasoko wa kiujamaa, hadi mwaka 2020, ambapo China licha ya kukamilisha ujenzi wa mambo ya viwanda, itafikia kwa hatua ya mwanzo mafanikio ya upashanaji habari.

Katika miaka zaidi ya 50 iliyopita, mabadiliko makubwa yametokea katika uhusiano wa uwiano kati ya sekta tatu za uzalishaji mali. Toka mwanzoni mwa miaka ya 50 ya karne iliyopita hadi mwaka 2002, shughuli za kilimo nchini China zilipungua kutoka 45.4% hadi 14.5%, shughuli za viwanda ziliongezeka kutoka 34.4% hadi 51.8%, na sekta ya utoaji huduma ilikuwa na ongezeko la 33.7% kutoka 20.2%.

Kilimo

China ni nchi yenye idadi kubwa kabisa ya wakulima, na kilimo kinachukua nafasi muhimu sana katika uchumi wa China.

Ingawa eneo la ardhi ya China ni kilomita za mraba milioni 9 na laki 6, lakini ardhi ya mashamba ni kiasi cha kilomita za mraba milioni 1.27, ikiwa ni 7% ya ardhi ya mashamba duniani, ambayo hasa iko katika sehemu ya tambarare ya mashariki na mabonde. Ukulima ni sehemu muhimu sana katika sekta ya kilimo nchini, mazao muhimu ya nafaka ni pamoja na mpunga, ngano, mahindi na maharage, pamoja na mazao ya biashara kama pamba, karanga, mbegu za chakula cha mifugo, miwaa na viazi vitamu.

Maendeleo ya kasi ya kilimo ya China yalianza kutokea baada ya mageuzi ya vijijini mwaka 1978. Katika muda wa zaidi ya miaka 20 iliyopita, mageuzi ya vijijini yakiwa chini ya utaratibu wa umilikaji wa ushirika, yaliondolea mbali vikwazo vya umilikaji wa kijadi na kubuni mikakati mipya ya uchumi wa kimasoko. Mageuzi yalileta manufaa kwa wakulima, na kukuza ufanisi wa nguvu-kazi ya vijijini. Mikakati hiyo ilichangia ongezeko kubwa la kilimo, hususan la uzalishaji wa nafaka, kuboresha hatua kwa hatua muundo wa kilimo na kuleta maendeleo makubwa ya kilimo. Hivi sasa, uzalishaji wa nafaka, pamba, mbegu za chakula cha mifugo, tumbaku, mifugo, mayai, mazao ya baharini na mboga, umechukua nafasi ya kwanza duniani.

Katika miaka ya karibuni, serikali ya China imekuwa ikitoa kipaumbele kwa maendeleo ya kilimo, kuongeza uwekezaji kwa kilimo, kuongeza pato la wakulima na kuleta maendeleo ya uwiano ya miji na vijiji hatua kwa hatua.

Viwanda

Maendeleo ya kasi ya viwanda vya China yalianza kutokea mwanzoni mwa miaka ya 50 ya karne iliyopita. Baada ya China mpya kuasisiwa mwaka 1949, viwanda vya China viliingia kipindi cha kufufuka na maendeleo. Hadi kabla ya kufanyika mageuzi mwaka 1978, China ilikuwa imejenga mfumo wa uchumi wa viwanda. Sekta ya kijadi ya uzalishaji wa mafuta ya asili ya petroli na viwanda vipya vya kemikali na elektroniki vilikuwa na maendeleo ya haraka, wakati viwanda vya nyuklia na usafiri kwenye anga ya juu ambavyo ni sekta ya uzalishaji mali ya sayansi na teknolojia ya kiwango cha juu, vilipata mafanikio makubwa. Tokea mwishoni mwa miaka ya 70 ya karne iliyopita, maendeleo ya viwanda vya China yaliimarishwa kwa hatua kubwa zaidi. Kati ya mwaka 1979 na mwaka 2003, wastani wa ongezeko la nyongeza ya thamani ya uzalishaji wa viwanda ulikuwa zaidi ya 10% kwa mwaka.

Kutokana na kuendelezwa kwa miaka zaidi 50 iliyopita, bidhaa muhimu za viwanda vya China ziliongezeka zaidi ya mara mamia kadhaa ambazo baadhi yake zinasafirishwa katika sehemu mbalimbali duniani. Toka mwaka 1996, uzalishaji wa chuma cha pua, makaa ya mawe, saruji, mbolea za chumvichumvi na televisheni umekuwa ukichukua nafasi ya kwanza duniani.

Mwaka 2003, nyongeza ya thamani ya uzalishaji wa viwanda ilikuwa Yuan za Renminbi trilioni 5 bilioni 361 na milioni 200, ikiwa ni ongezeko la 12.6% ikilinganishwa na ile ya mwaka uliotangulia. Hivi sasa, si kama tu kwamba China inaweza kuzalisha ndege, meli na magari, bali pia inaweza kuunda satellite ya dunia pamoja na zana za kisasa za viwanda. Hivi sasa China imekuwa na mfumo kamili wa viwanda. Katika siku za baadaye, China itatekeleza mkakati mpya wa kuleta maendeleo ya viwanda kwa teknolojia ya upashanaji wa habari na kuimarisha kuboresha viwanda kwa maenedeleo ya uchumi wa China.

Sekta ya Huduma

Maendeleo ya haraka yalianza kutokea katika sekta ya huduma nchini China mwishoni mwa miaka ya 70 ya karne iliyopita.

Maendeleo hayo yalionekana hasa katika pande mbili: kwanza ni kupanuka kwa mfululizo kwa sekta ya huduma. Kutokana na takwimu, thamani ya ongezeko la sekta ya huduma nchini China kwa mwaka 2002 lilifikia Yuan za Renminbi trilioni 3 na bilioni 453.3 kutoka Yuan bilioni 86.05 mwaka 1978, ikiwa ni ongezeko la mara 39. Wastani wa ongezeko kwa mwaka ulikuwa zaidi ya 10%, kiasi hiki kilikuwa ni kikubwa zaidi kuliko jumla ya uzalishaji mali wa taifa nchini. Thamani ya ongezeko la sekta ya huduma katika jumla ya thamani ya uzalishaji mali kwa mwaka 2002 ilifikia 33.7%, kutoka 21.4% mwaka 1979. Mwaka 2003, japokuwa sekta ya huduma iliathiriwa vibaya na ugonjwa wa SARS na maafa ya kimaumbile ya ukosefu wa mvua na mafuriko, lakini bado kulikuwa na maendeleo ya kasi.

Kwa upande mwingine, sekta ya huduma nchini China ilikuwa njia muhimu ya kuongeza nafasi za ajira. Idadi ya watu wanaofanya kazi katika sekta ya huduma iliongezeka na kufikia zaidi ya milioni 210, ikiwa ni mara mbili kuliko ongezeko la wafanyakazi wapya katika sekta ya viwanda.

Hivi sasa, sekta ya huduma inahusiana na mambo ya migahawa, utalii, biashara rejareja ya bidhaa, sarafu, bima, upashaji wa habari, uchukuzi, matangazo ya biashara, sheria, uhasibu na utunzaji wa majengo ya wakazi. Kwa mujibu wa mpango wa maendeleo ya China, itakapofika mwaka 2020, ukubwa wa sekta ya huduma katika jumla ya uzalishaji mali wa nchini, utaongezeka kwa zaidi ya 50% kutoka kiasi cha theluthi moja ya hivi sasa.


1 2 3 4 5 6 7 8 9 10 11 12