3: Uchumi wa China

Mazingira ya uwekezaji

Ujenzi wa Miundo Mbinu   

China ni nchi kubwa, barabara za China zinafika kila mahali nchini, zikiwemo barabara kuu 12 za ngazi ya taifa zenye umbali wa kilomita elfu 35 ambazo ni barabara 5 kutoka sehemu za kusini hadi sehemu za kaskazini na barabara 7 muhimu za kati ya sehemu za mashariki na magharibi, ambazo karibu zote ujenzi wake umekamilika.

Siku zote China inauchukulia ujenzi wa barabara kuwa ni jambo moja muhimu katika ujenzi wa miundo mbinu. Uwekazaji katika ujenzi wa barabara kati ya mwaka 1998 na mwaka 2001 ulikuwa Yuan bilioni 300 kwa mwaka. Barabara mpya zilifikia urefu wa kilomita elfu 67 zikiwa ni pamoja na kilomita 5,700 za barabara za kasi. Mwaka 2003, ujenzi wa barabara mpya zenye urefu wa kilomita elfu 36 ulikamilika. Hadi kufikia mwishoni mwa mwaka jana, barabara za China zilifikia kilomita milioni 1 na laki 8, ikiwa ni pamoja na kilomita elfu 40 za barabara za kasi za kisasa. Aidha, serikali iliharakisha ujenzi wa barabara katika sehemu za kati na magharibi, ambazo zimeboresha mawasiliano ya sehemu hizo.

Ujenzi wa barabara kuu zote za China utakamilika mwaka 2008, ambapo miji ya Beijing, Shanghai, miji mikuu ya mikoa na miji mingine mikubwa zaidi ya 200 kwa jumla, itaunganishwa na barabara za kasi au barabara za ngazi ya juu.

RELI

Hadi kufikia mwishoni mwa mwaka 2003, urefu wa reli za China ulifikia kilomita elfu 73. Kati ya hizo zaidi ya kilomita elfu 20 ni zenye njia mbili pamoja na kilomita elfu 18 za treni ya umeme. Reli ya kwanza ya China inayovuka bahari kati ya mkoa wa Guangdong na mji wa Haikou ilianza kutumika tarehe 7 mwezi Januari mwaka 2003. Reli kati ya mikoa ya Qinghai na Tibet yenye umbali wa kilomita 1,142 ambayo inayojengwa kwenye uwanda wa juu kabisa duniani, ujenzi wake unatazamiwa kukamilika mwaka 2006. Hivi sasa China imekuwa moja ya nchi zenye shughuli nyingi za usafirishaji wa reli duniani, na pia ni nchi yenye ongezeko la kasi la usafirishaji wa reli na ufanisi mkubwa katika matumizi ya reli.

Tokea mwaka 1998, China iliinua kiwango cha reli ili kuongeza kasi za treni, hivi sasa treni nyingi za abiria zinasafiri wakati wa jioni na kufika stesheni ya mwisho wakati wa asubuhi ili kuwarahisishia abiria kufanya shughuli zao wakati wa mchana.

BANDARI

Ujenzi wa bandari za pwani ya China unafuata zilipo rasilimali za makaa ya mawe, makontena, na mawe ya madini ya chuma yanayoagizwa kutoka nchi za nje, njia za usafiri wa meli zenye kina kirefu za kuingia baharini, hususan kutilia mkazo ujenzi wa mfumo wa usafirishaji wa makontena. Serikali imejenga magati yenye kina kirefu kwa ajiri ya usafirishaji wa makontena katika miji ya Dalian, Tianjin, Qingdao, Shanghai, Ningbo, Xiamen na Xhenzhen, ambayo yameweka msingi kwa uundaji wa mfumo muhimu wa uchukuzi wa makontena, wakati baadhi ya magati ya kupakulia mafuta asili ya petroli na mawe ya madini ya chuma yaliyoagizwa kutoka nchi za nje, yalirekebishwa na kupanuliwa.

Hadi kufikia mwishoni mwa mwaka 2003, bandari muhimu zilizoko kwenye pwani ya China, zimekuwa na mahali pa meli 1800, zikiwemo meli zaidi ya 530 zenye uwezo wa kubeba mizigo zaidi ya elfu 10. Bandari hizo zina uwezo wa kushughulikia tani bilioni 1.7 za mizigo kwa mwaka. Baadhi ya bandari kubwa zimekuwa na uwezo wa kushughulikia mizigo zaidi ya tani milioni, wakati bandari nane kubwa za Shanghai, Shenzhen, Qingdao, Tianjin, Guangzhou, Xiamen, Ningbo na Dalian ni miongoni mwa bandari 50 zinazoongoza kwa upakiaji na upakuaji wa makontena duniani.

USAFIRI WA NDEGE

Safari za ndege za China zinafika mabara yote ya dunia. Hadi kufikia mwishoni mwa mwaka 2003, kulikuwa na viwanja vya ndege za abiria zaidi ya 140 vikiwa na safari zaidi ya 1000, ambazo ni pamoja na safari zaidi ya 160 zinazofika miji zaidi ya 60 ya nchi zaidi ya 30.

SIMU

Mwaka 2003, ongezeko la idadi ya simu mpya za nyumbani lilifikia milioni 49.08, na idadi ya jumla ya simu za nyumbani mwishoni mwa mwaka huo ilikuwa ni zaidi ya milioni 260. Kati ya hizo za mijini zilikuwa ni zaidi ya milioni 170 na za vijijini zilikuwa milioni 92.13. China ilianzisha utoaji wa huduma za simu za mikononi mwaka 1987, ambao ulikuwa na maendeleo ya kasi baada ya mwaka 1990, na ongezeko la wateja wapya lilikuwa ni zaidi 100%. Mwaka 2003, mtandao wa simu za mikononi ulifika katika miji yote mikubwa na wastani pamoja na miji midogo na ya wilaya zaidi ya 2,000. Ongezeko la wateja wapya lilifikia milioni 270, na jumla ya idadi ya wateja wa simu za mikononi ilikuwa ni zaidi milioni 530, ikiwa ni ongezeko la watu milioni 110 kuliko mwaka 2002, ambapo watu 42 kati ya watu 100 walikuwa na simu za mikononi. ?

Sera za Uwekezaji Vitega Uchumi

China ni moja kati ya nchi zinazovutia vitega uchumi vingi duniani. Katika hali ambayo uchumi wa dunia umezorota na uwekezaji wa kimataifa unapungua kwa kiwango kikubwa, China imeweza kupata mafanikio makubwa katika kuvutia mitaji ya nchi za nje. Sababu kubwa ya mafanikio hayo inatokana na kuwekwa sera nyingi mwafaka za uwekezaji.

Tangu mwanzoni mwa miaka ya 80 ya karne iliyopita, China imetenga nguvukazi, vifaa na fedha nyingi katika ujenzi wa miradi mingi ya miundo-mbinu ili kuanzisha mazingira bora ya uwekezaji na kujenga viwanda kwa wafanyabiashara wa nchi za nje. Katika muda huo, China ilitoa sheria na kanuni zaidi ya 500 za kiuchumi zinazowahusu wafanyabiashara wa nchi za nje ambazo zimeweka wajibu na dhamana ya sheria kwa uwekezaji wa wafanyabiashara wa kigeni hapa nchini. Mwishoni mwa mwaka 1997, China ilirekebisha "Orodha ya maelekezo ya uwekezaji kwa wafanyabiashara wa kigeni" ili kuwapa motisha na kuwaunga mkono wawekeze katika maeneo ya ustawishaji wa mambo ya kilimo, nishati, mawasiliano, vifaa na malighafi muhimu, teknolojia mpya za kiwango cha juu, matumizi ya rasilimali na hifadhi ya mazingira. Kutokana na kanuni za Shirika la Biashara Duniani WTO na ahadi ilizotoa China kwa nchi za nje, nyaraka za kisheria kiasi cha 2,300 zilichambuliwa na kurekebishwa, ambazo 830 kati yake zilitenguliwa, 325 zilirekebishwa, ambapo kwa hatua ya mwanzo, kazi za kuchambua na kurekebisha sheria na kanuni za kiuchumi zinazowahusu wafanyabiashara wa kigeni zilikamilika, na utaratibu wa sheria kuhusu uwekezaji wa wafanyabiashara wa kigeni, ambazo sheria tatu muhimu kuhusu viwanda vya ubia na vya ushirikiano kati ya China na wafanyabiashara wa kigeni pamoja na vya mitaji ya wafanyabiashara wa kigeni kuwa ni uti wa mgongo, umejengwa kwa ujumla. Hadi mwishoni mwa mwaka 2003, wafanyabiashara wa kigeni kutoka nchi na sehemu zaidi ya 170 duniani wamewekeza hapa nchini, hivi sasa idadi ya viwanda vilivyowekezwa na wafanyabiashara wa kigeni ni zaidi ya laki 4; makampuni na mashirika makubwa ya kimataifa yanavutiwa na soko la China, mashirika makubwa ya kimataifa yanayochukua nafasi 500 za juu duniani, karibu yote yamewekeza nchini China. China imechukuliwa na wawekezaji na sekta za mambo ya fedha kuwa moja ya nchi yenye mazingira bora sana ya uwekezaji. ?

Maeneo Maalumu ya Kiuchumi na Miji ya Kufungua Mlango

Serikali ya China wakati ilipoamua kufanya mageuzi mwaka 1978 dhidi ya utaratibu wa uchumi, ilianza kutekeleza hatua kwa hatua sera za kufungua mlango. Tokea mwaka 1980, China ilianzisha maeneo matano ya ustawishaji wa uchumi katika miji ya Shenzhen, Zhuhai na Shantou ya mkoa wa Guangdong pamoja na mkoa wa Hainan; Mwaka 1984, ilifungua milango ya miji 14 ya sehemu ya pwani ikiwa ni pamoja na Dalian, Qianhuangdao, Tianjin, Yantai, Qingdao, Lianyungang, Nantong, Shanghai, Ningbo, Wenzhou, Fuzhou, Guangzhou, Zhanjiang, na Beihai; Mwaka 1985 iliidhinisha delta za mito Changjiang, Zhujiang na Minnan, peninsula za Shandong na Liaodong, pamoja na mikoa ya Hebei na Guangxi kuwa ya kufungua mlango kwa nje, ambayo imeunda kanda ya kufungua mlango kwenye sehemu ya pwani. Mwaka 1990, serikali ya China iliamua kustawisha na kufungua mlango wa sehemu mpya ya Pudong ya Shanghai na baadhi ya miji iliyoko kando za mto Changjiang. Baada ya mwaka 1992, serikali iliamua kufungua milango ya baadhi ya miji iliyoko sehemu ya mpakani na kufungua milango ya miji mikuu ya mikoa yote; Kuanzisha maeneo 15 ya kuwekea bidhaa zinazosafirishwa nchi za nje, maeneo 49 ya ustawishaji wa uchumi wa ngazi ya taifa na maeneo 53 ya ustawishaji wa teknolojia mpya na ya kiwango cha juu. Baada ya hapo, China ilikamilisha hali ya kufungua mlango katika sehemu za pwani, kando za mito, mipakani na za bara kwa ngazi tofauti.

Kutokana utekelezaji wa sera nafuu za aina mbalimbali katika sehemu zilizofungua mlango, kulileta athari nzuri kwa sehemu za bara katika kukuza uchumi unaosafirisha bidhaa nje, kuongeza fedha za kigeni na kuingiza teknolojia ya kisasa kutoka nchi za nje.

Maeneo ya Ustawishaji wa Uchumi Na Teknolojia

Maeneo ya ustawishaji wa uchumi na teknolojia ni moja ya sehemu ya China inayofungua mlango kwa nchi za nje. Kutenga eneo dogo katika mji unaofungua mlango kwa nje, kukamilisha ujenzi wa miundo mbinu na mazingira ya uwekezaji wa kiwango cha kisasa duniani, ili kufanya sehemu hiyo kuwa sehemu muhimu katika uendelezaji wa uchumi na biashara ya nje kwa mji huo na kwa sehemu nyingine za karibu.

Mwaka 1988, baraza la serikali liliidhinisha kuanzisha maeneo ya ustawishaji wa uchumi na teknolojia katika miji 14 ya sehemu ya pwani ikiwa ni pamoja na Dalian, Qinhuangdao, Tianjin, Yantai, Qingdao, Lianyungang, Nantong, Minhang, Hongqiao, Chaohejing, Ningbo, Fuzhou, Guangzhou na Zhanjiang. Hadi sasa nchini China kuna maeneo 49 ya ustawishaji wa uchumi na teknolojia ya ngazi ya taifa, ambayo 27 yako katika sehemu ya pwani ya mashariki na 22 yako katika sehemu ya magharibi ya China. Aidha, baraza la serikali liliidhinisha kutekelezwa sera zinazotekelezwa katika maeneo ya ustawishaji wa uchumi na teknolojia ya ngazi ya taifa katika maeneo mengine ya viwanda na ustawishaji wa uchumi ya Suzhou, Jinqiao, Ningbo, Xiamen, Hainan na Yangpu.

Maeneo ya Teknolojia Mpya Na Kiwango cha Juu ya Ngazi ya Taifa

Hivi sasa, China imeanzisha maeneo zaidi ya 50 ya ngazi ya taifa ya ustawishaji wa teknolojia mpya na ya kiwango cha juu, ambapo mafanikio zaidi ya 600 ya utafiti wa sayansi ya ngazi ya mikoa na wizara, yanatumika katika uzalishaji mali. Wastani wa ongezeko la malengo muhimu ya kiuchumi katika maeneo hayo kwa mwaka, lilikuwa kiasi cha 60% katika miaka 10 iliyopita, na kuwa nguvu muhimu inayochangia ongezeko la uchumi wa taifa.

Eneo la sayansi na teknolojia la Zhongguancun la Beijing pamoja na baadhi ya maeneo ya ustawishaji wa teknolojia mpya na ya kiwango cha juu ya ngazi ya taifa yaliyoko katika miji ya Tianjin, Shanghai, Helongjiang, Jiangsu, Anhui, Shandong, Hubei, Guangdong, Shanxi, Dalian, Xiamen, Qingdao na Shenzhen yamethibitishwa na serikali kuwa vituo vya kwanza vya usafirishaji wa bidhaa kwa nchi za nje kutokana na maendeleo yake makubwa, mazingira bora na ongezeko la kasi la usafirishaji wa bidhaa za teknolojia mpya na ya kiwango cha juu. Kati ya maeneo hayo, maeneo ya delta za mto Lulu na Changjiang pamoja na sehemu ya Beijing na Tianjin ambayo kuna viwanda vingi vinavyozalisha bidhaa za kusafirishwa nje, thamani ya bidhaa zake zinazosafirishwa nchi za nje imechukua zaidi ya 80% ya thamani ya bidhaa za teknolojia mpya na ya kiwango cha juu za nchi nzima. Mwaka 2002, jumla ya thamani ya usafirishaji bidhaa za teknolojia mpya na ya kiwango cha juu kwa nchi za nje imechukua zaidi ya 20% ya jumla ya thamani ya bidhaa za China zilizosafirishwa nje, na kufanya bidhaa za China zinazosafirishwa nje kuwa bora zaidi.

Maeneo ya Bidhaa za Kusafirishwa Nje

Maeneo ya kuweka bidhaa zinazosafirishwa nchi za nje, yaliidhinishwa na baraza la serikali la kuendeleza biashara ya kimatafa na shughuli kuhusu bidhaa zinazosafirishwa nchi za nje, ambayo yanafanana na maeneo ya biashara huria duniani, katika maeneo hayo, wafanya biashara wa kigeni wanaruhusiwa kuendesha biashara za kimataifa, kujenga mabohari ya kuwekea bidhaa zinazosafirishwa nje, na shughuli za ushindikaji na usafirishaji. Hivi sasa nchini China kuna maeneo 15 ya bidhaa za kusafirishwa nje, likiwemo lile la Waigaoqiao la Shanghai. Maeneo hayo yamekuwa kama kiunganishi kipya kati ya uchumi wa China na dunia.

Hali ya Uagizaji wa Bidhaa

Wakati uchumi wa China unapokuwa na ongezeko mfululizo, biashara ya nje pia inapata maendeleo makubwa. Hivi sasa China imefikia nafasi ya 6 mwaka 2001 katika biashara ya duniani kutoka nafasi ya 32 mwaka 1978, nafasi ya 15 mwaka 1989, na nafasi ya 10 mwaka 1997. Mwaka 2001, jumla ya thamani ya usafirishaji bidhaa nje na uagizaji bidhaa ilifikia dola za kimarekani bilioni 509.5, ambayo ni mara ya kwanza kuzidi dola za kimarekani bilioni 500 kwa biashara ya China na nchi za nje. Kiasi hiki ni ongezeko la 24.7, 4.6 na 1.57 kuliko mwaka 1978, 1989 na 1997. Katika mwaka 2002, biashara nje ya China ilipanda kwa kiwango kingine na kufikia dola za kimarekani bilioni 602.77. Mwaka 2003, thamani ya biashara ya nje ya China ilifikia dola za kimarekani bilioni 851.2, ikiwa ni ongezeko la 37.1% kuliko mwaka uliopita. Kati hilo, thamani ya bidhaa zilizosafirishwa nje ilikuwa dola za kimarekani bilioni 438.4, ambazo ni ongezeko la 34.6%, na thamani ya bidhaa zilizoagizwa kutoka nje ilikuwa dola za kimarekani bilioni 412.8, kiasi hicho ni ongezeko la 39.9 kuliko mwaka uliopita. Nafasi ya China katika biashara ya duniani ilipanda hadi ya 4.

Hivi sasa, China imekuwa na uhusiano wa kibiashara na nchi au sehemu zaidi ya 220, Aidha nchi au sehemu kumi zinazochukua nafasi za mbele katika uhusiano wa kibiashara na China ni Japan, Marekani, Umoja wa Ulaya, mkoa wa utawala maalumu wa Hongkong, Umoja wa nchi za Asia ya kusini mashariki, Korea ya kusini, Taiwan, Australia, Russia, na Canada.


1 2 3 4 5 6 7 8 9 10 11 12