Kamisheni ya Umoja wa Afrika (AU) imetoa wito kwa kukabilaina na vizuizi visivyo vya ushuru ili kutimza malengo makuu ya Makubaliano ya Biashara Huria ya Afrika.
Katika taarifa yake iliyotolewa jana jumapili, Umoja wa Afrika umesisitiza kuwa bara hilo linakaribia kuwa eneo kubwa la biashara huria duniani, na kama suala hilo halitashughulikiwa, linaweza kupunguza kasi ya juhudi hizo.
Kwa mujibu wa Umoja huo, ingawa athari mbaya za vizuizi visivyo vya ushuru katika maingiliano ya kibiashara inatambulika, lakini kumekuwa na juhudi hafifu za kukabiliana nazo hadi sasa.
Kamishna wa Biashara na Viwanda wa Umoja huo Bw. Albert Muchanga amesema, mafanikio ya Eneo la Biashara Huria barani Afrika (AfCFTA) yanategemea kwa sehemu kubwa jinsi serikali za nchi za bara hilo zinavyoweza kufuatilia na kuondoa vizuizi vyote visivyo vya ushuru.
Kutokana na Shirika la Biashara na Maendeleo ya Umoja wa Mataifa (UNCTAD), kama vizuizi hivyo vitaondolewa, uchumi wa Afrika unaweza kuongezeka kwa dola za kimarekani bilioni 20, ikiwa ni zaidi ya dola za kimarekani bilioni 3.6 zinazoweza kupatikana kama ushuru ukifutwa.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |