EAC yapoteza dola zaidi ya bilioni 37 katika sekta ya biashara kutokana na janga la COVID-19
Ofisa Mkuu wa Baraza la Biashara la Jumuiya ya Afrika Mashariki Bwana Peter Mathuki amesema, tangu janga la virusi vya Corona lilipotokea, nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki zimepoteza zaidi ya dola bilioni 37, kutokana na kukwama kwa shughuli nyingi za kibiashara .
Akizungumza na Idhaa ya Kiswahili ya Radio China Kimataifa jijini Nairobi, Bw. Mathuki amezitaka nchi sita zinazounda Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), kushirikiana ili kutatua mizozo ya mipakani inayoathiri biashara katika ukanda huo. Katika siku za hivi karibuni, madereva wa malori ya mizigo wanaotoka Kenya kwenda Uganda, wamekuwa wakilalamika vikali kuhusiana na masharti makali yaliyopo mipakani, yanayowalazimisha kukaa mpakani kwa zaidi ya wiki moja, hali inayoathiri bidhaa nyingi haswa vyakula, kando na kulemaza shughuli za kibiashara katika mataifa husika.
Bwana Peter Mathuki amesema, tayari Baraza hilo limewaarifu mawaziri husika kutoka nchi sita wanachama wa Jumuiya hiyo, ili kutafuta suluhisho la tatizo hilo. Aidha, Bw. Mathuki amesema, sekta ya utalii katika kanda ya Afrika Mashariki imeathirika zaidi na kuchangia asilimia 92 ya hasara ya kibiashara katika kandahiyo.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |