Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2003-12-12 11:11:58    
Maisha Ya Watu Wa Kawaida Wa Nan Chizi Mjini Beijing

cri

  Nan Chizi

    Siku moja katika mwezi uliopita, Mzee Qin Zhen mwenye umri wa miaka 74, akiambatana na watoto na wajukuu wake, alirudi kwenye makazi yake yaliyopo Nan Chizi, katikati ya mji wa Beijing, ambapo tayari nyumba zimefanyiwa ukarabati. Mzee Qin ana familia yenye vizazi vinne, na ameishi katika eneo hilo la Nan Chizi kwa miongoni kadhaa. Mwaka jana mradi wa ukarabati wa eneo hilo ulipoanza, familia hiyo ilihama kutoka kwenye makazi ya zamani. Hivi sasa, mwaka mmoja umepita, pamoja na familia nyingine 300, Mzee Qin na familia yake wamerudi kwenye makazi mapya.
Eneo hilo la Nan Chizi lipo kando ya kusini ya Kasri la wafalme ambalo hujulikana kama Forbidden City. Katka kipindi cha miaka zaidi ya 500, eneo la Nan Chizi lilikuwa mahali pa maghala ya kifalme, ambapo raia walikuwa hawaruhusiwi kuingia. Kufuatia kupinduliwa utawala wa kifalme nchini China mwaka 1911, Nan Chizi ikabadilika kuwa eneo la makazi ya watu wa kawaida.
    Siku nenda siku rudi, idadi ya wakazi ilikuwa ikiongezeka katika eneo hilo, ambapo hivi sasa miundo mbinu imechakaa na huwa ni kawaida kwa watu wa familia tofauti kuishi katika nyumba moja ya ua. Na nyumba za nyua hakukuwa na misala,na iliwabidi wakazi kwenda hata umbali wa mita 100. Mbali na hayo, katika eneo hilo, pia kuna majengo kadhaa ambayo ni mabaki ya majengo ya kale yanayopewa uhifadhi na serikali ya Beijing, kwa mfano hekalu la Pudu. Majengo hayo vile vile yameharibika sana.
    Mwishoni mwa mwaka 2002, serikali ya mji wa Beijing iliamua kufanya ukarabati au kujenga upya nyumba zenye nyua zipatazo 192 katika eneo la Nan Chizi, ikilenga kuhifadhi sura yake maalumu ya kijadi. Kiongozi wa mtaa wa Dongcheng mjini Beijing Bw. Wang Peili alitufahamisha, akisema, "Katika eneo la Nan Chizi, mabaki ya kale na nyumba zenye nyua yenye thamani, yote yamehifadhiwa, kwa jumla, ni nyumba za nyua zipatazo 31. Aidha, tumebakiza miti mikubwa mikongwe ipatayo 64 kwenye eneo hilo na miti yote iliyo kando ya njia za miguu. Na majengo haramu yenye mita za mraba karibu elfu 10 yamebomolewa."
    Mtoto mkubwa wa Mzee Qin, Bw. Qin Yuanzhang ameishi katika eneo hilo kwa miaka zaidi ya 40. Hivi sasa, amerudi katika nyumba mpya yenye ua yenye mtindo wa kijadi. Katika nyumba hiyo, alionekana mwenye furaha sana, alieleza kuwa,    

    "Leo nimefurahi sana, kwani majirani wote wamerudi. Nilikua katika eneo hilo, nalipenda sana. Nyumba tayari zimekarabatiwa, zina sura nzuri kweli, hivyo nimefurahishwa nazo."
    Sasa hebu tutembelee kidogo nyumba mpya ya Bw. Qin, yenye orofa mbili. Katika orofa ya kwanza, kuna sebule, msala na jiko. Tukipanda juu hadi orofa ya pili, tunakuta chumba kikubwa cha kulala ambacho ukuta mzima wa upande unaoelekea jua ni dirisha. Tukitembea uani, imewekwa framu kwa mzabibu na  imepandwa miti. Pia kuna meza na viti, vyote vimetengenezwa kwa mawe. Jengo hilo lina rangi ya kijivu, ukuta wa ua ni mweupe, na milango na framu za madirisha ni za rangi nyekundu na rangi ya kijani. Kwa hiyo, ua hilo kutoka mtindo wa jengo mpaka rangi zake, umejengwa kwa kufuata mtindo wa kijadi wa makazi ya watu mjini Beijing. Lakini tofauti ni kwamba,sasa hivi zimewekwa zana mbalimbali za kisasa, kama vile maji, umeme, gesi n.k..
    Bw. Wang Peili alieleza kuwa, eneo la mauazi ya Nan Chizi ni la kwanza kufanyiwa ukarabati miongoni mwa maeneo yenye mabaki mengi ya kale mjini Beijing, mradi huo umetekelezwa kama majaribio. Katika ukarabati wa eneo hilo ,nyumba zenye nyua zimejengwa upya kwa mtindo wa kijadi, imepandwa miti na nyasi mbele ya majengo,kwenye njia za waenda kwa miguu yametandazwa na matofali yanayofanana na yale yakijadi. Katika ujenzi wa baadhi ya nyumba zenye nyua, wajenzi walitumia ufundi wa kijadi, na kudumisha kabisa sura ya kijadi ya makazi ya watu wa Beijing. Kwa mfano, baadhi ya nyumba zenye nyua  kwenye makazi zimejengwa kwa mbao bila kutumia msumari.
    Naibu mkuu wa idara ya hifadhi ya mabaki ya kale ya Beijing Bw. Kong Fansi alipohojiwa na mwandishi wetu wa habari, alisema, "Mradi huo wa ukarabati wa eneola mauazi ya Nan Chizi una maana kubwa kwa uhifadhi wa kasri la wafalme lijulikanalo kama Forbidden City, ambapo umeboresha mazingira na kuhifadhi vitu vya kale. Tukiangalia kwa upeo wa mbali, mradi huo unasaidia kulegeza shinikizo la idadi kubwa ya wakazi mjini, na kuboresha makazi makongwe yenye hatari. Siku za baadaye, serikali ya Beijing itaendelea na kazi ya kuboresha mazingira na kuhifadhi maeneo yenye thamani ya kiutamaduni na kihistoria."
    Wasikilizaji wapendwa, eneo la makazi ya Nan Chizi ni miongoni mwa maeneo 25 yaliyopewa uhifadhi na serikali ya Beijing kama maeneo yenye mabaki ya kale. Beijing ni mji mkongwe wenye historia ya miaka 850, ambao pia ni mji mkuu wa China kuanzia enzi za kifalme, kwa hiyo, mji huu una mabaki mengi ya kale. Ukiwa unaelekea kuwa  mji wa kisasa na wa kimataifa, watu wa Beijing pia wanajitahidi kuhifadhi sura ya kijadi ya mji huo na utamduni wake