Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2003-12-15 15:37:39    
Makala ya nne ya chemsha bongo kuhusu vivutio vya
utamaduni na utalii wa eneo la magharibi ya China

cri
    Wasikilizaji wapendwa, leo tunawaletea makala ya 4 inayowafahamisha sehemu kadhaa zenye vivutio vya utalii zilizoorodheshwa na UNESCO kwenye kumbukumbu za urithi wa mali duniani.

    Kwenye mkutano wa 15 kuhusu urithi wa mali duniani ulioitishwa na Shirika la UNESCO mwezi Julai, mwaka huu, sehemu yenye kivutio cha ?Mito mitatu iendayo sambamba? ilikubaliwa kuorodheshwa kwenye kumbukumbu za urithi wa maumbile duniani. Sehemu hiyo iko katika eneo la kusini magharibi ya China. Hivyo, katika eneo la magharibi ya China, kuna sehemu 10 zenye vivutio vya mandhari nzuri ambazo zimeorodheshwa kwenye kumbukumbu za urithi wa duniani. Aidha, katika eneo la magharibi ya China, zipo sehemu nyingine nyingi zenye vivutio vya maumbile ya kiasili na utamaduni.

    Bwana Xie Ningao ni mtaalamu maarufu wa China anayeshughulikia utafiti wa urithi wa duniani, ambaye pia ni profesa wa Chuo kikuu cha Beijing, aliwahi kuzunguka mara 4 nchini kote China. Anatuelezea:

    China ni nchi yenye hali inayotatanisha kijioglafia, hasa toka Bonde la Turufan lililoko mita 154 chini ya usawa wa bahari hadi Uwanda wa juu wa Qinhai-Tibet ulio kama paa la dunia, hali ya kijioglafia ni yenye matata mengi sana, hivyo ziko sehemu nyingi zenye maumbile ya kiasili. Katika eneo hilo, hali ya hewa pia ni ya aina mbalimbali ya ukanda wa tropiki na wa vuguvugu.

    Matata ya hali ya hewa na hali ya kijiografia yakikutana yanaleta viumbe vya aina nyingi tofauti na maumbile maalum ya kiasili.

    China ni nchi yenye historia ya miaka 5000, hivyo mabaki ya urithi wa utamaduni ni mengi sana. China ina makabila 56, kila kabila lina umaalum wake wa utamaduni.

    Profesa Xie alisema, eneo la magharibi ya China ni kubwa na watu wake ni wachache, hivyo athari mbaya na uharibifu kutokana na shughuli za binadamu kwa sehemu zenye maumbile ya kiasili za huko ni chache. Hivyo katika eneo la magharibi ya China, sehemu zilizoorodheshwa kwenye kumbukumbu za urithi duniani zinaonekana kuwa na vivutio zaidi vya maumbile ya kiasili.

    Ndugu wasikilizaji, sasa tunawafahamisha sehemu mbili za urithi wa dunia katika eneo la magharibi ya China. Moja ni Mapango ya Mogao yenye vivutio vya utamaduni, nyingine ni Bonde la Jiuzhaigou yaani Bonde la vijiji 9 vya kitibet lenye vivutio vya maumbile ya kiasili.

    Mapango ya Mogao yalichongwa kwenye mlima ulioko nje ya mji wa Dunhuang, mkoani Gansu, kaskazini magharibi ya China, ambapo yako mapango zaidi ya 700, miongoni mwake, mapango 500 ni yenye vinyago vya rangi na michoro ya kutani. Mapango hayo yalichongwa kwa miaka 1000 kuanzia karne ya 4 hadi karne ya 14. Mwaka 1987, Mapango ya Mogao yaliorodheshwa na UNESCO kwenye kumbukumbu za urithi wa utamaduni duniani.

    Ndani ya Mapango ya Mogao vipo vinyago zaidi ya 2000, michoro ya kutani zaidi ya mita elfu 40 za mraba, vinyago hivyo na michoro ya kutani ni vya mitindo tofauti na kiwango cha juu cha usanii ambavyo vimeonesha vilivyo usanii wa vinyago na michoro ya kutani ya China katika kipindi hicho cha historia.

    Aidha, katika mwaka wa 1900, watu waligundua pango lililojificha ndani ya pango moja huko, ndani ya pango hilo zimehifadhiwa data nyingi zenye thamani zinazohusu utamaduni wa kidini, utamaduni wa raia na maingiliano ya utamaduni kati ya China na nchi za magharibi. Data hizo zimewawezesha watu kuongeza ujuzi kuhusu jamii ya zama za kale ya China.

    Miaka zaidi ya 1600 imepita kuanzia karne ya 4 hadi sasa, lakini michoro mingi ya kutani ndani ya Mapango ya Mogao bado inang?ara kwa rangi zake na uchoraji wake; hata vinyago vya rangi pia vimehifadhiwa vizuri ndani ya mapango. Mtaalamu wa utafiti wa mambo ya kale wa Taasisi ya sayansi ya jamii ya China Bwana Wu Xinhua alifahamisha akisema:

    Sehemu ya Dunhuang iko katika eneo la jangwa, kuna uhaba mkubwa wa mvua. Hali hiyo ya ukame inasaidia hifadhi ya vinyago vya rangi na michoro kutani. Aidha, sehemu ya Dunhuang ilikuwa sehemu yenye waumini wengi sana wa dini ya Budha katika zama za kale, ambapo watu wa zama hizo walihifadhi kwa makini vinyago na michoro hiyo.

    Ndugu wasikilizaji, Bonde la Jiuzhaigou yaani Bonde la vijiji 9 vya kitibet ni bonde moja la miujiza lililoko kwenye wilaya ijiendeshayo ya kabila la wachiang na watibet la Aba mkoani Sichuan, jina lake linatokana na kuwepo kwa vijiji 9 bondeni. Kwenye bonde hilo, yapo maziwa makubwa na madogo zaidi ya 100, na maziwa hayo mengi yanaungana na maporomoko. Maji ya maziwa hayo ni safi sana ambayo yanaonekana kuwa na rangi mbalimbali na hali ya kupendeza kutokana na mionzi ya jua kutoka pande tofauti au kutokana na mabadiliko ya majira tofauti na mabadiliko ya mazingira.

    Ziwa la maua matano lenye rangi tofauti liko katikati ya Bonde la Jiuzhaigou, kama jina lake lilivyo, ziwa hilo huonekana rangi mbalimbali, ambapo rangi nyepesi ya manjano, kijani nzito, na rangi ya buluu huonekana kwa mara nyingi zaidi. Profesa Fan Xiao wa kikosi cha utafiti wa jiolojia cha mkoa wa Sichuan anatuelezea: Maji yenyewe hayana rangi, lakini wakati wa anga buluu, maji huonekana rangi nzuri ya kibuluu na kijani inayopendeza sana.

    Ziwa la maua matano ni ziwa lenye miujiza, mbali ya mabadiliko ya rangi ya maji, kila ifikapo majira ya baridi, maji ya maziwa mengine ya Bonde la Jiuzhaigou huganda, lakini maji ya ziwa la maua matano kamwe hayagandi.

    Aidha, misitu na maua pori huongezea vivutio kwa Bonde la Jiuzhaigou. Katika majira ya mpukutiko, bonde hilo linawapendeza watu zaidi, rangi mbalimbali zinaonekana popote pale, watu wakitembelea huko hujisikia kama wako katika dunia yenye miujiza.

    Mwaka 1992, Bonde la Jiuzhaigou yaani Bonde la vijiji 9 vya kitibet liliorodheshwa kwenye kumbukumbu za urithi wa maumbile ya kiasili duniani.

    Ndugu wasikilizaji, sasa tunatoa maswali mawili ya leo: Mapango ya Mogao ambayo ni kumbukumbu za urithi wa maumbile ya kiasili duniani yako katika mkoa gani nchini China? Swali la pili: Bonde la Jiuzhaigou yaani Bonde la vijiji 9 vya kitibet ambalo ni moja ya urithi wa maumbile ya kiasili duniani linajulikana kutokana na miujiza gani?