Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2003-12-15 15:40:17    
Makala ya tano ya chemsha bongo kuhusu vivutio vya utamaduni na utalii wa eneo la magharibi ya China

cri
    Makala hii ni ya mwisho ya chemsha bongo, ambayo itawaelezea mila na desturi tofauti za watu wa makabila madogomadogo wanaoishi katika eneo la magharibi ya China.

    Ndugu wasikillizaji, China ina makabila 56, kabila la wahan ni kabila kubwa zaidi, watu wake wanachukua asilimia 93 ya idadi ya jumla ya watu wa nchi nzima, na watu wa makabila mengine 55 ni wachache, hivyo makabila hayo yanaitwa kuwa ni makabila madogomadogo. Watu wa makabila mengi madogomadogo wanaishi katika eneo la magharibi ya China, katika makala ya 2 na ya 3 tuliwafahamisha kuhusu watu wa makabila ya watibet, wahui na wawiur wanaoishi katika eneo la kusini magharibi na kaskazini magharibi mwa China, leo tunawafahamisha hali kuhusu kabila la wamongolia wa kaskazini ya China na watu wa makabila mengine madogomadogo wanaoishi katika eneo la kusini magharibi ya China.

    Nchini China watu wengi wakisikia nyimbo zenye sauti nene na ndefu na kuimba kwa hisia nyingi watatambua mara moja nyimbo kama hizo ni za kabila la wamongolia. Watu wa kabila la wamongolia wa China wanaishi katika mkoa ujiendeshao wa Mongolia ya ndani wa kaskazini ya China.

    Kabila la wamongolia ni kabila moja kati ya makabila madogomadogo yenye watu wengi zaidi. Idadi ya watu wa kabila la wamongolia ni zaidi ya milioni 4. Watu wa kabila hilo wanaishi katika mbuga kubwa na kufanya kazi ya ufungaji, hivyo watu hao huwa ni watu jasiri na wachangamfu zaidi. Kila ifikapo majira ya joto, majani yanapositawi kwenye mbuga, tamasha kubwa la kijadi la Nadamu hufanyika kwenye mbuga. Tamasha kubwa la Nadamu ni sikukuu muhimu zaidi ya mwaka kwa watu wa kabila la wamongolia, tamasha hilo huendelea kwa siku 3. Maana ya Nadamu ni burudani na michezo kwa lugha ya kimongolia.

    Katika sikukuu hiyo, wamongolia hufanya kwanza sherehe ya kutambika kwa mungu ili kuombea hali nzuri ya hewa na mavuno mazuri, halafu wanafanya mashindano ya kupiga mieleka, kukimbia kwa farasi na ulengaji wa mishale. Jioni watu wanapiga vinanda vya kienyeji kwa kujiburudisha, ambapo wanaume wanakula nyama na kunywa pombe, wasichana wanaimba nyimbo na kucheza ngoma kwa furaha kubwa. Kama ukiwa mmoja miongoni mwao, utafurahia sana shamrashamra zilizofanyika kwenye mbuga kubwa ya Mongolia ya ndani.

    Katika eneo la kusini magharibi ya China, watu wa makabila madogomadogo zaidi ya 30 wanaishi huko, miongoni mwao idadi ya watu wa kila kabila la wazhuan, wayi, wamiao, watong, wayao, wabai na watai ni zaidi ya milioni moja. Wimbo mliosikia sasa hivi umeimbwa na wasichana wa kabila la watong. Watong ni watu wanaoishi mkoani Guizhou, watu wa kabila la watong ni wenye hulka ya muziki, tangu zamani watong wanajua sana kuimba nyimbo kwa sauti za ngazi tofauti bila kufuata upigaji wa muziki.

    Katika eneo la kusini magharibi ya China kuna milima mingi midogo midogo, hali ya hewa ya huko ni ya joto na unyevunyevu, na watu wa huko wengi wanakaa kwenye nyumba za miti na mianzi, na wanapenda kuvaa nguo walizozifuma wenyewe, na kuvaa mapambo ya madini ya fedha kichwani.

    Mkoa wa Yunnan ni mkoa wanakoishi watu wa makabila madogomadogo mengi zaidi nchini China, makabila hayo yamefikia 25, na kabila la wabai wanaishi katika wilaya ijiendeshayo ya kabila la wabai ya Dali. Wabai wanapendelea rangi nyeupe, hivyo mavazi yao hata majengo yao huwa ni ya rangi nyeupe. Katika wilaya ya Dali, lipo ziwa Erhai lililoko kwenye uwanda wa juu, na karibu na ziwa hilo, upo mlima Chang, watalii wakitembelea ziwa hilo wanaweza kukaa kwenye boti huku wakinywa chai maarufu ya kabila la wabai.

    Kabila la wazhuan lina watu wengi zaidi kuliko makabila mengine madogomadogo nchini China, idadi ya watu wake imefikia zaidi ya milioni 15, na wengi wao wanaishi katika mkoa ujiendeshao wa kabila la wazhuan wa Guangxi. Watu wa kabila la wazhuan wanapenda zaidi kuimba nyimbo nchini China. Katika vijiji au sehemu za milimani wanakoishi watu wa kabila la wazhuan, kuimba nyimbo ni kitu kisichokosekana katika maisha ya watu wa huko, na watu wa kabila hilo wanaweza kuelezea kila kitu kwa uimbaji wa nyimbo.

    Na kila ifikapo tarehe 3 ya mwezi wa tatu kwa kalenda ya kilimo ya China, wazhuan hufanya tamasha la nyimbo, siku hiyo ni siku yenye furaha kubwa kwa wazhuan. Katika sikukuu hiyo, wazhuan huvaa nguo maridadi wakati wa kushiriki tamasha la nyimbo, na wanajenga vibanda mbalimbali vya rangi kwa kuimba nyimbo, kuchagua wachumba, na kucheza ngoma ya dragon. Na shughuli kuu ya siku hiyo ni kuimba nyimbo, watu huimba vilivyo kwa kuelezea maisha, mapenzi, urafiki na dunia ya maumbile, ama kushiriki mashindano ya kuimba nyimbo.

    Mwimbaji mmoja wa kabila la wazhuan aitwaye Huang Chunyan alituelezea:

    Watu wa maskani yangu wanaweza kuimba nyimbo nyingi mbalimbali kuhusu milima, mapezi, maisha ya utotoni na vinywaji. Mababu zangu na wazazi wangu wote wanajua kuimba nyimbo za kienyeji, mimi nimekulia katika uimbaji wa nyimbo.

    Sasa tunatoa maswali mawili ya makala ya 5 ya chemsha bongo kuhusu vivutio vya utalii na utamadumni wa eneo la magharibi ya China. Swali la kwanza: Ni tamasha gani ambalo ni kubwa zaidi kwa watu wa kabila la wamongolia wa China. Swali la pili: Miongoni mwa makabila madogomadogo ya China, ni kabila gani ambalo lina watu wengi zaidi kuliko makabila mengine?

    Na kufikia hapa kwa leo tumekamilisha matangazo ya makala 5 za chemsha bongo kuhusu vivutio vya utamaduni na utalii kwenye eneo la magharibi ya China.