Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2003-12-16 15:15:08    
Kaburi la mfalme wa kwanza Qinshihuang

cri

Qinshihuang 

    Kaburi la mfalme wa kwanza Qinshihuang wa enzi ya Qin. Kaburi hili liko katika sehemu ya magharibi ya China. Sanamu za askari na farasi zilizozikwa ndani zinajulikana kama piramidi ya Misri ya kale, ni miujiza ya nane duniani.

    Mfalme Qinshihuang aliyezaliwa mwaka 259 na kufariki dunia mwaka 210 kabla ya kuzaliwa Kristo, alikuwa mfalme wa kwanza wa jamii ya kimwinyi ya China. Mfalme huyo anatajwa sana katika historia, lakini hadi sasa watu bado hawajapata kauli moja kuhusu hadhi yake kwenye historia. Alikuwa mfalme wa kwanza aliyeunganisha China nzima; alitumia hatua mbalimbali za kustawisha uchumi na utamaduni kama vile hatua za kusawazisha sarafu, maandishi, upimaji wa uzito na urefu; na mfalme huyo alijenga ukuta mkuu wa kukinga maadui. Hatua hizo zilimpatia sifa za kuwa mwanasiasa mashuhuri katika historia ya China. Lakini kwa upande mwingine alikuwa mfalme mkatili na mbadhirifu kupita kiasi. Ili kuwapumbaza kimawazo wananchi, hata mfalme huyo alitumia sera ya kuchoma moto vitabu ambavyo havikulingana na mawazo yake ya utawala, na aliwatesa wasomi wa Confucius; pia watu ambao walitofautiana naye kimawazo aliwazika wakiwa hai ili kudumisha utawala wake. Aidha, katika kipindi chake cha utawala alitumia fedha nyingi na watu wengi kujijengea kaburi na kasri ya anasa ili awe na maisha ya furaha.

    Mfalme Qinshihuang alianza kujenga kaburi lake si muda mrefu baada ya kuunganisha China nzima. Watu laki 7 walilazimishwa kujenga kaburi hilo, na mfalme huyo alipofariki dunia miaka 40 baadaye walikuwa hawajakamilisha ujenzi wa kaburi hilo. Kaburi la mfalme huyo lenye eneo la kilomita za mraba 56.25 liko kwenye mlima Lishan katika kitongoji cha Mji wa Shian mkoani Shanshi. Msingi wa kaburi ni wa mraba ambao una urefu wa mita 350 kutoka kusini hadi kaskazini, na mita 345 kutoka mashariki hadi magharibi, na kimo cha mita 76. Kutoka juu, kaburi hilo lina umbo la piramidi. Kutokana na utafiti, wataalamu wa elimukale wamegundua kwamba pembeni mwa kaburi hilo kuna mashimo na makaburi zaidi ya mia 5 ya vitu na makaburi ya wajenzi wa kaburi waliotumiwa kama kafara. Kwenye mashimo kulifukiwa sanamu za farasi na mikokoteni ya shaba nyeusi ambayo yameonesha jinsi mfalme Qinshihuang alivyokuwa kwenye gari la farasi, pia zipo sanamu za vibanda vya farasi ndani ya kasri, kwenye shimo kubwa sanamu za askari na farasi ambazo zinaashiria jeshi shupavu katika enzi yake ya Qin zimefukiwa.

    Sanamu za askari na farasi zinajulikana kama miujiza ya nane duniani na ugunduzi wake ni wa bahati tu. Mwaka 1974 wakulima wa sehemu hiyo walipochimba kisima walipata vigae vingi vya vyombo vya udongo, lakini hawakutilia maanani na walitaka kuvitupa. Kwa bahati nzuri wakati huo mtaalamu mmoja aliyekuwa huko, alivitazama na kuona kuwa pengine ni ugunduzi mkubwa. Alitoa taarifa kwenye idara ya mambo ya kale wilayani, hivyo sanamu za askari na farasi zikafukuliwa. Hadi leo sanamu 500 za askari, mikokoteni 18 ya vita ya mbao, na sanamu zaidi ya 100 za farasi zimegunduliwa. Sanamu za askari zina maumbile makubwa ambapo urefu ni wastani wa mita moja na sentimita 80, sura zao zilichongwa kama za halisi, na hisia kwenye nyuso zao ni tofauti, ambapo zimeonesha ustadi mkubwa wa uchongaji katika enzi ya Qin.

    Sanamu za askari na farasi zinawavutia sana wageni kutoka nchi mbalimbali, wageni wengi huja kuziangalia bila kujali umbali. Baadhi ya viongozi wakubwa wa serikali za nchi mbalimbali walipotembelea China pia waliomba kwenda huko kushuhudia wenyewe. Rais mstaafu wa Marekani Ronald Reagan alieleza kuwa sanamu hizo ni miujiza ya ajabu ya binadamu.

    Ili kuhifadhi kaburi hilo lisiharibike hivi sasa, serikali ya China haina mpango wa kuchimbua kaburi halisi la mfalme Qinshihuang. Katika miaka ya karibuni, vitu zaidi ya elfu 50 ambavyo ni kama johari adimu duniani viligunduliwa kutoka kwenye mashimo pembeni mwa kaburi la Qinshihuang. Mojawapo ni mkokoteni wa kuvutwa na farasi uliotengenezwa kwa shaba nyeusi na kupambwa kwa dhahabu na fedha. Mkokoteni huo uliotengenezwa kwa makini uligunduliwa mwaka 1980, ambapo ukubwa wake ni nusu ya mkokoteni halisi, ukionesha jinsi mfalme Qinshihuang alivyoendesha gari lake.

    Kutokana na hali halisi kwenye mashimo na kutokana na vitabu vya historia vilivyoelezea kasri ya mfalme Qinshihuang, kaburi la Qinshihuang inaonesha jinsi dola yake ilivyokuwa, mfalme akitamani kwamba baada ya kufa kwake angeendelea na utawala wake. Lakini hakutarajia kwamba miaka mitatu tu baada ya kifo chake, Enzi ya Qin ilipinduliwa katika mapinduzi ya wakulima. Kaburi hilo ambalo ni kubwa kabisa nchini China kuliko makaburi yote ya wafalme na lenye vitu vingi vilivyofukiwa, na lina miaka zaidi ya elfu 2 chini ya ardhi, limekuwa "ushahidi" wa mabadiliko ya historia ya China. Kutokana na thamani kubwa ya kihistoria, mwaka 1987, kaburi na sanamu za askari na farasi ziliorodheshwa na Unesco kwenye kumbukumbu ya urithi wa utamaduni wa dunia.

Idhaa Ya Kiswahili 2003-12-25