Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2004-01-11 16:16:05    
Suzhou yakuwa sehemu ya wanafunzi wanayopenda kuanzisha makampuni

cri

Mji wa Suzhou ambao ni maarufu kwa mandhari nzuri pia ni mji wenye historia ndefu na msingi imara wa kiutamaduni. 

  Katika miaka zaidi 20 iliyopita China ilikuwa na wanafunzi karibu laki 6 ambao waliokwenda kusoma katika nchi zilizoendelea. Katika miaka ya hivi karibuni kadiri uchumi wa China unavyopata ongezeko la kasi, ndivyo wanafunzi wengi zaidi waliosoma katika nchi za nje, wamekuwa wakirudi kuanzisha makampuni yao hapa nchini. Katika mkondo huo, Suzhou ambao ni mji maarufu katika historia na utamaduni ulioko sehemu ya mashariki ya China, umekuwa ni sehemu mojawapo ambayo wanafunzi wanaorudi nchini wanapenda kwenda kuanzisha makampuni kutokana na huduma nzuri zinazotolewa huko.

  "Hapa panafanana kidogo na Silicon Valley." Mkurugenzi mkuu wa kampuni ya Anboxin Bi. Wu Hong aliusifu mji wa Suzhou. Bi. Wu Hong alikwenda kusoma Marekani mwaka 1980 ambapo alipata shahada ya udaktari katika mambo ya "software" katika chuo kikuu cha Berkeley cha jimbo la Carifonia na kufanya kazi huko kwa zaidi ya miaka 10. Miaka minne iliyopita alifika mjini Suzhou na kuanzisha kampuni ya "software" kutokana na kuvutiwa na mazingira bora ya kuanzisha makampuni yaliyoko katika mji huo. Alisema, "Wakati ule nilivutiwa sana na mazingira pamoja na uungaji wa mkono wa serikali ya Suzhou, hivyo nilichagua sehemu hiyo. Licha ya hayo, mji wa Suzhou uko karibu na mji wa Shanghai, lakini gharama za nguvukazi ni ndogo ikilinganishwa na Shanghai. Pia kwa sisi tunaofanya kazi katika sekta ya "software", tunahitaji sehemu ambayo gharama za uzalishaji ni ndogo na ambayo imetulia. Mazingira ya eneo la ustawishaji la hapa ni yenye kivutia sana."

  Katika kipindi cha mwanzoni, kampuni ya Anboxin ni moja kati ya makampuni machache yaliyoanzishwa na wanafunzi waliosoma nchi za nje. Hivi sasa, Bi. Wu Hong hajisikii mpweke tena, kwani katika eneo hilo la ustawishaji kumekuwa na makampuni zaidi ya 260 yaliyoanzishwa na wanafunzi zaidi ya 400 waliosoma nchi za nje na kurejea nchini, wote wakijitahidi kutimiza azma zao. Habari zinasema kuwa makampuni yanayoanzishwa mjini Suzhou na wanafunzi waliosoma nchi za nje, yanaongezeka kwa karibu 20% kila mwaka, ambayo yote yanahusika na sekta za teknolojia za kiwango cha juu zikiwa ni pamoja na upashanaji habari, teknolojia ya uhifadhi mazingira ya asili na utengenezaji wa dawa.

  Eneo la mji wa Suzhou ni kiasi cha kilomita za mraba 8,500. Mji huo hauna majengo mengi makubwa isipokuwa una bustani nyingi nzuri. Mjini Suzhou hakuna sauti ya makelele kama ya miji mingine mikubwa. Machoni mwa wachina, Suzhou ni mji wenye utamaduni mkubwa ambao ulikuwa na wanafasihi, wasomi na wanasayansi wengi mashuhuri katika historia ya China. Mbali na hayo, mji huo upo katika sehemu ya delta ya mto Changjiang ambayo ni sehemu iliyoendelea sana kiuchumi nchini China, kutokana na kuwa karibu sana na mji wa Shanghai, ambao ni mji wa kwanza kwa ukubwa kwa mambo ya viwanda na biashara nchini China. Mji huo ambao uko umbali wa kilomita 90 tu kutoka Shanghai, umekuwa na mazingira bora zaidi ya kuvutia wanafunzi waliosoma nchi za nje kwenda huko kuwekeza na kufanya kazi.

  Aidha, uungaji mkono wa serikali ya huko ni moja kati ya sababu muhimu zinazowavutia wanafunzi hao kwenda kuwekeza huko. Kabla ya miaka michache iliyopita, mji wa Suzhou ulianzisha eneo maalumu la kuanzisha makampuni kwa wanafunzi waliosoma nchi za nje linajulikana duniani kama chombo cha uzalishaji wa makampuni "Incubator" na kuwasaidia kisera. Ofisa wa mji wa Suzhou Bi. Cui Ping alipohojiwa na mwandishi wa habari alisema kuwa uungaji mkono wa serikali ulianzisha mazingira bora. Alisema, "Tumeanzisha kituo cha kuhamasisha uanzishaji wa makampuni ambacho ni kama chombo cha uzalishaji wa makampuni ya kimataifa na pia ni eneo la kuanzisha makampuni kwa wanafunzi wanaorejea nchini baada ya kumaliza masomo yao nchi za nje. Kituo hicho kilizinduliwa mwaka 1994, serikali ilitenga Yuan milioni 400, sawa na dola za kimarekani milioni 48.8 kusaidia ujenzi wa kituo hicho, na makampuni yaliyoanzishwa kwa msaada wa kituo chetu ni zaidi ya 400 na mengi kati ya hayo yamefanikiwa."

  Ofisa huyo alisema kuwa mwanzoni baada ya kujengwa kituo hicho cha kuhamasisha uanzishaji wa makampuni, kamati ya usimamizi ya kituo ilibuni sera kadhaa mwafaka za kuweka mazingira bora ya kuwavutia wanafunzi waliosoma nchi za nje, kutokana na kufahamu kuwa wanafunzi hao watakabiliwa na matatizo kadhaa katika shughuli za uanzishaji wa makampuni. Kwa mfano kamati ya kituo inasaidia wanafunzi kuomba leseni na kujiandikisha katika idara ya ushuru bila malipo. Mbali na hayo, kinawaruhusu wanafunzi hao kutumia bure majengo yao na kuwatoza ushuru kidogo kwa miaka mitatu baada ya kuanzisha makampuni yao.

  Aidha, kituo hicho kinawasaidia wanafunzi hao kupata msaada wa fedha kutoka serikalini na kuanzisha mazungumzo kati ya wanafunzi na mabenki ili kujenga uhusiano kati yao kwa haraka.

  Hivi sasa, nchini China kuna vituo zaidi ya 400 vinavyowasaidia wanafunzi wanaorejea nchini kutoka nchi za nje. Kuhusu mafanikio makubwa yaliyopatikana katika kituo cha Suzhou, ofisa wa serikali ya mji wa Suzhou anayeshughulikia kituo hicho Bw. Wu Tian-cheng alisema kuwa sababu kubwa ya mafanikio ni msimamo wa kuwahudumia wanafunzi wanaoanzisha makampuni pamoja na kuwa na sera za kutoa kipaumbele kwa mambo ya biashara.

  Hivi sasa, makampuni yaliyoanzishwa mjini Suzhou na wanafunzi waliorejea nchini yamedumisha maendeleo ya kasi. Hivi sasa kuna kampuni makumi kadhaa yanayosubiri kibali cha kuingia Suzhou. Kwa wanafunzi wanaorejea nchini, Suzhou ingali bado ni sehemu iliyo nzuri kabisa ya kuanzisha makampuni.

Idhaa ya Kiswahili 2004-01-06