Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2004-01-20 20:40:26    
Mradi wa magenge matatu waleta nafasi mpya kwa maendeleo ya Chongqing

cri

  Mji wa Chongqing ulioko katika sehemu ya kuisni magharibi ya China, ni mji wa kale na wenye shughuli nyingi za viwanda. Mji huo ulioko kwenye sehemu ya juu ya mtiririko wa mto Changjiang, baada ya kuthibitishwa kuwa mji unaosimamiwa moja kwa moja na serikali kuu mwaka 1997, ulikuwa na mpango wa kuujenga mji huo uwe na ustawi kama Hongkong. Mji wa Chongqing uko katika sehemu ya Bwawa la Magenge Matatu, maofisa na wakazi wa huko wote wana matumaini makubwa kutokana na ujenzi wa mradi wa uzalishaji umeme wa Magenge Matatu.

  Mwandishi wa habari alipofika mjini Chongqing vitu alivyoona ni magari mengi yaliyoko kwenye barabara ya kasi, meli nyingi zilizoko kwenye magati ya mto Changjiang, majengo marefu yaliyojengwa karibu na milima iliyo kwenye kando za mto changjiang, taa za rangirangi na mabango ya matangazo pamoja na watu wanaopita haraka haraka barabarani. Mji wa Chongqing ukiwa na wakazi zaidi ya milioni 30 ni mji wa kwanza kwa wingi wa idadi ya wakazi nchini China. Wakati giza linapoingia , watu wakitazama mwangaza wa taa za mji wa Chongqing kutoka kando nyingine ya mto, wanahisi kwamba mji huo unafanana na Hongkong.

  Mwaka 2003, ni mwaka usio wa kawaida kwa wakazi wa Chongqing. Mradi wa uzaliishaji wa umeme kwa nguvu za maji ulioanza kujengwa miaka 10 iliyopita, ulianza kulimbikiza maji mwaka jana, kuzalisha umeme na kutumika kwa uchukuzi majini. Wakazi wa Chongqing wameanza kuona mabadiliko yanayoletwa na mradi wa magenge matatu. Mkazi wa Chongqing bibi Zhang Zong mwenye umri wa miaka 50, alisema, "Kwa kuwa maji ya mto Changjing yamekuwa mengi, hivyo meli zilizosafiri kwenye mto zimekuwa nyingi. Wavuvi badala ya kutumia mashua zao kuvua samaki, sasa wanazitumia mashua zao kupeleka watalii kutembelea sehemu ya magenge matatu madogo na mto Wu. Hivi sasa pato lao limeongezeka na maisha yao yameboreshwa. Mabadiliko makubwa yametokea katika matumizi yao ya umeme, hapo zamani baadhi ya sehemu za Chongqing zilikuwa na upungufu wa umeme na katika baadhi ya nyakati umeme ulikatika, sasa tatizo hilo limetatuliwa kabisa."

  Kutokana na hali bora uchukuzi kwenye mto Changjiang, Kampuni ya Minsheng ya Chongqing iliyoanzishwa mwaka 1984, imekuwa ni kampuni binafsi ya katika uchukuzi majini. Mwaka uliopita, baada ya maji ya bwawa kufikia kina cha mita 135, mazingira ya usafirishaji yaliboreshwa hususan katika sehemu ya Chongqing.

  Mkurugenzi mkuu wa kampuni ya Minsheng Bw. Lu guo-ji alisema, "Kabla ya kujengwa kwa bwawa, sehemu zote za juu za mtiririko wa mto zilikuwa hatari kwa usafirishaji. Baada ya kujengwa kwa bwawa la Magenge Matatu, sehemu hizo hazina hatari tena kwa usafirishaji. kulimbikiza maji katima eneo la Magenge Matatu ni muhimu sana kwa shughuli za usafirishaji wa sehemu zote za mto Changjiang. Hivi sasa kiasi cha bidhaa zinazosafirishwa kwenye mto Changjiang kimeongezeka, na muda unaotumika katika usafirishaji ni mfupi kuliko zamani."

  Bw. Lu Guo-ji alisema kuwa hali bora ya usafirishaji kwenye mto Changjiang ni kwamba uwezo wa usafirishaji ni mkubwa na gharama zake ni ndogo. Hivi sasa kampuni yao inatumia nafasi nzuri ya kukamilika kwa ujenzi wa bwawa, kuongeza meli zao na kujitahidi kusafirisha mizigo mingi zaidi.

  Kuhusu maendeleo yaliyopatikana katika shughuli za usafirishaji kwenye mto Changjiang baada ya kukamilika kwa ujenzi wa bwawa, naibu mkurugenzi wa shirika la uchukuzi la mji wa Chongqing Bw. Dou Yun-sheng alisema, "Katika usafirishaji wa mizigo, Chongqing imepata maendeleo makubwa katika ukusanyaji na usafirishaji wa mizigo. Hivi sasa, tunatumia njia mpya katika shughuli zetu za usafirishaji wa mizigo, ambayo mara kwa mara tunapeleka magari ya mizigo kwenye meli na kuyasafirisha hadi sehemu iliyo chini ya mji wa Yichang. Kufanya hivi si kama tu ni salama bali pia gharama ya usafirishaji inapungua. Katika usafirishaji wa abiria, Mji wa Chongqing unanuia kukuza shughuli za usafirishaji wa watalii, sasa inafikiria kuongeza meli za kifahari za abiria."

  Mkurugenzi Dou alisema kuwa hadi kufikia mwaka 2009, ujenzi wa mradi wa Magenge Matatu utakapokamilishwa kabisa, maji ya bwawa yatafikia mita 175, shughuli za usafirishaji wa abiria zitakuwa nyingi zaidi.

  Chongqing ukiwa ni mji wa viwanda katika sehemu ya magharibi ya China, unatumia umeme mwingi sana. Pamoja na maendeleo ya haraka ya uchumi wa Chongqing na kuinuka kwa kiwango cha maisha ya wakazi wake, umeme wa Chongqing umekuwa shida kukidhi mahitaji ya huko. Mwaka 2003, mradi wa Magenge Matatu ulianza kupeleka umeme kwenye mji wa Chongqing. Mkurugenzi wa idara ya mpango ya kampuni ya umeme ya mji wa Chongqing Bw. Wan Zai-yang alisema kuwa mwaka 2003, vituo vya umeme vya Magenge Matatu vilipeleka Kilowati/saa milioni 770 za umeme kwenye mji wa Chongqing, ambao ulichagia sana maendeleo ya uchumi wa Chongqing. Hivi sasa pato la mji wa Chongqing limeongezeka kwa 170% kuliko wakati kabla mji huo kuthibitishwa kuwa mji unaosimamiwa moja kwa moja na serikali kuu.

  Mkurugenzi Wan alisema kuwa hivi sasa 80% ya umeme unaotumika mjini Chongqing unazalishwa kwa makaa ya mawe au mafuta ya dizeli.Lakini hata hivyo, Chongqing imeanza kutumia umeme wa Magenge Matatu ambao utaboresha hali ya utoshelezaji wa umeme katika mji huo mzima.

  Mradi wa magenge Matatu umekuza uwezo wa Chongqing kuendeleza uchumi wake. Katika miaka ya karibuni, wafanya biashara wengi wa nchi za nje walikwenda kuwekeza mjini Chongqing kutokana na kupendezwa na mradi wa Magenge Matatu ambao utakuwa nguvu ya ustawishaji wa uchumi wa Chongqing.

Idhaa ya Kiswahili 2004-05-15