Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2004-01-22 21:09:22    
Mwaka wa Kima wa kichina

cri
    Tarehe 22 mwezi Januari ni sikukuu ya mwaka mpya wa Kichina. Katika kalenda ya Kichina kila mwaka unawakilishwa na mnyama wa aina moja, kwa hiyo kuna jumla ya wanyama kumi na wawili wanaowakilisha miaka 12. Kuanzia tarehe 22 mwezi huu watu wa China wameuaga mwaka wa mbuzi na kuingia katika mwaka mpya wa kima.

    Katika kalenda ya Kichina kila miaka 12 ni duru moja, na kila mwaka unawakilishwa na mnyama mmoja, jumla kuna wanyama wa aina 12, ambao ni panya, ng'ombe, chui, sungura, dragoni, farasi, mbuzi, kima, kuku, mbwa na nguruwe. Matumizi ya majina ya wanyama hao kuwakilisha miaka yalianza katika karne ya 6 K.K. nchini China. Lakini kuna imani tofauti ya matumizi ya majina ya wanyama kuwakilisha miaka yalivyotokea. Baadhi wanasema yalitokana na muungano wa namna ya kuhesabu miaka ya kabila la Han na ya makabila madogo madogo. Baadhi wanasema kuwa matumizi hayo yalikuja kutoka India. Kuhusu mfululizo wa wanyama 12 pia kuna misemo tofauti. Msemo unaowavutia watu zaidi unasemwa kuwa mfululizo huo unatokana na muda wakati mnyama fulani anashughulika zaidi katika siku. Kuanzia Enzi ya Han, karne ya 3 kabla ya kuzaliwa Kristo, China ilianza kuhesabu majira ya siku kwa vipindi 12. Usiku wa manane ulianzia saa 5 mpaka saa saba alfajiri, katika muda huo panya huwa na shughuli nyingi, kwa hiyo amepangwa kuwa wa kwanza. Kuanzia saa tisa mpaka saa 11 jioni ni kipindi cha kima kuwa na shughuli nyingi zaidi, na wakati huo kima huwa mchangamfu zaidi na mlio wake ni mzuri, kwa hiyo amepangwa kuwa wa tisa. Wakati mwaka wa kima unapokaribia, tunawaletea maelezo ya mnyama kima katika utamaduni wa China.

    Miongoni mwa wanyama kumi na wawili, kima anakaribia zaidi na binadamu. Na kwa jinsi anavyokuwa mwepesi katika kupanda miti na kuruka ruka bila kutaka kutulia anaonekana ni mnyama mwenye akili. Kuna masimulizi mengi kuhusu kima miongoni mwa Wachina. Kima anayejulikana kwa watu wote wa China ni Kima Mfalme Sun Wukong, mhusika mkuu katika riwaya ya "Safari ya Kwenda Magharibi", ambayo ni moja katika riwaya nne maarufu za China. Mfalme huyo alizaliwa chini ya jabali kubwa, alikuwa ni mtukutu na mwenye nguvu, aliweza hata kuruka kwa umbali kilomita laki moja akipigisha miguu chini, ana macho makali ambayo yanaweza kutambua mashetani waliogeuka kwa sura za binadamu na mnyama yeyote. Isitoshe alikuwa na uwezo wa kujigeuza mara 72. Mfalme Kima alikuwa na furaha kila wakati na hakuogopa kitu chochote. Kwa ujasiri alithubutu kupingana na mungu na kujinadi kuwa ni "Mtukufu Sawa na Mungu". Mfalme Kima alikuwa na utiifu mkubwa akimlinda sufii Tangzeng alipokwenda magharibi kupata msahafu halisi wa Dini ya Buddha. Akiwa safarini alipambana na mashetani wa aina mbalimbali ingawa aliwahi kuonewa bila haki na bwana wake sufii, lakini hakugeuza nia yake ya kumtii bwana wake. Mfalme Kima anawakilisha watu wenye tabia ya kutojali mambo madogo madogo na kuwa na unyoofu na mwenye nia thabiti ya kutimiza malengo yake makubwa ambayo ni vigumu kwa binadamu kuyatimiza. Katika miaka mia kadhaa iliyopita mfalme huyo amekuwa ni mfano wa shujaa mkubwa anayewapendeza watu wa China.

    Wachina wanaona kima ni nyota ya heshima. Katika michoro ya kale wahenga hutia michoro ya kima katika picha zao. "Kima wa Dhahabu" ni aina ya kima anayepatikana nchini China tu, ambaye manyoya yake ni marefu na yenye rangi ya dhahabu. Mwaka 1977 kima wa aina hiyo aliwekwa katika orodha ya wanyama wanaohifadhiwa wa daraja la kwanza, ni kama "johari ya taifa la China akimfuata panda".

    Pia kwenye stempu inaoneshwa jinsi kima wanavyopendwa na Wachina. Mwaka 1980 kwa mara ya kwanza, China ilitoa stempu ya kima, stempu hiyo ilikuwa na senti 8 kila moja, lakini sasa thamani yake ni yuan elfu 4 na mia tano.

    Sura ya kima imechaguliwa kuwa ni "nembo ya jaha" ya mashindano ya soka ya Asia.

    Wakati mwaka wa kima ulipokaribia, bidhaa zenye sura za kima zilimiminika madukani, na sanamu za dhahabu za kima kupongeza mwaka mpya tayari zimeuzwa zote.

    Wanaompenda kima sio Wachina peke yao bali pia hata watu wa nchi nyingine. Siku za karibuni Australia ilisambaza kote duniani sarafu za dhahabu na za fedha zenye sura za kima kwa mwaka 2004, na sarafu hizo zinauzwa nchini China. Kati ya sarafu hizo moja ya dhahabu ina uzito wa kilo moja, na inasemekana kuwa sarafu hiyo ya kumbukumbu ni nzito kabisa duniani. Pamoja na hayo Marekani pia imetoa spempu za kumbukumbu za mwaka wa kima na kila stempu imechapwa maneno ya Kichina "Mwaka wa Kima" na kwa Kiingereza "Happy New Year".

Idhaa ya Kiswahili 2004-01-22.