Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2004-02-05 17:46:29    
Uhifadhi wa Mabaki ya Kale katika Eneo la Magenge Matatu.

cri

Watu wanavutiwa na vitu vya kale vilivyogunduliwa katika eneo la magenge matutu.

  Mradi wa maji wa magenge matatu unaojengwa hivi sasa katika mto Changjiang, China ni mradi mkubwa kabisa kuliko mingine duniani kwa hivi sasa, bwawa lake limemaliza kulimbikizwa maji kwa hatua ya mwanzo na limeanza kuzalisha umeme. Ujenzi wa mradi huo mkubwa unatarajiwa kukamilika ifikapo mwaka 2009. Kwa hiyo, kazi za kuhifadhi mabaki ya kale katika eneo zima la bwawa zinabidi kukamilika kabla ya mwaka huo. Mwandishi wetu wa habari alipotembelea sehemu ya magenge matatu hivi karibuni, aliona kuwa, mbali na shughuli za ujenzi, bwawa hilo pia limebadilika kuwa eneo kubwa la utafiti wa mambo ya lake, ambapo vikundi mbalimbali vya wataalamu wa mambo ya kale vinafanya kazi kutwa kucha, vikilenga kuhifadhi urithi wa kiutamaduni wa binaadamu.

  Wafanyakazi wa kikundi cha taasisi ya mambo ya kale ya mji wa Chongqing hupanda kivuko na kuvuka mto Changjiang kila siku, wakielekea sehemu iitwayo Yuxiping ambayo ina vitu vya kale ardhini, na wamefanya kazi katika eneo la bwawa la mradi wa magenge matatu kwa miaka 6. Katika sehemu ya Yuxiping, mwandishi wetu wa habari aliona mashimo manane yaliyochimbwa na wafanyakazi hao pamoja na kauri za kale. Wafanyakazi hao walikuwa wanaendelea na kazi zao.

  Sehemu hiyo ya Yuxiping ipo eneo la mtiririko wa juu wa bwawa la magenge matatu. Mkuu wa kikundi hicho cha wataalamu wa mambo ya kale Bw. Bai Jiujiang alifafanua kuwa, sehemu hiyo ina mabaki mengi ya kale. "Tuligundua mabaki ambayo mpaka hivi sasa yamekuwepo katika sehemu ya Yuxiping kwa miaka elfu 7, ambayo ni mabaki mengi ya kale kutoka miaka elfu 7 iliyopita mpaka mwaka 1911. Tumeyapa mabaki hayo jina la utamaduni wa Yuxi."

  Changjiang ni mto wa kwanza kwa ukubwa nchini China, ambao pia ni miongoni mwa vyanzo vya utamaduni wa Kichina. Mwanzoni mwa miaka 90 ya karne iliyopita, serikali ya China iliamua kujenga mradi wa maji wa magenge matatu katika mto Changjiang, na uhifadhi wa mabaki ya kale katika magenge matatu ikawa sehemu muhimu ya kazi za mradi huo. Kazi hiyo ina sehemu mbili za juu ya ardhi na chini ya ardhi, ambapo sehemu zipatazo 1,074 ziliwekwa kwenye orodha ya majina ya sehemu zinazopewa uhifadhi, na eneo la sehemu hizo linachukua asilimia 70 ya bwawa la magenge matatu. Kwa upande wa uhifadhi wa mabaki ya kale yaliyopo juu ya ardhi, majengo maarufu kama vile mahekalu yamepewa uhifadhi mzuri kwa hivi sasa. Kazi ngumu zaidi ni kulinda mabaki ya kale yaliyopo chini ya ardhi. Naibu mkuu wa taasisi ya mambo ya kale ya mji wa Chongqing, Bw. Zou houxi alieleza kuwa, "Katika sehemu za bwawa la magenge matatu zilizopo mjini Chongqing, kuna sehemu 506 zenye mita milioni 1.3 za mraba ambazo zinahitaji kuchimbwa ili kutafuta mabaki ya kale. Serikali imetenga Yuan za Renminbi milioni 270 kwa kazi hiyo. Kiasi hicho cha Pesa ni cha ajabu kweli kwa shughuli za utafiti wa mambo ya kale. Ili kukamilisha kazi hiyo, inabidi kutegemea nguvu za nchi nzima. Chini ya msaada wa idara ya mabaki ya kale ya taifa, idara ya utamaduni ya mji wa Chongqing imealika vikundi 68 vya wataalamu wa mambo ya kale kutoka sehemu mbalimbali nchini. Na kazi zao zimepata mafanikio."

Wataalamu wa vitu vya kale wanafanya kazi katika eneo la magenge matatu.

  Katika miaka zaidi ya 10 iliyopita, wataalamu hao walikuwa wanafanya kazi na kuishi katika eneo la bwawa la mradi wa magenge matatu. Katika hali ngumu, walikuwa wamekamilisha mujukumu mbalimbali muhimu. Na wanafurahia kazi ya kufichua ustaarabu uliotengenezwa na watu wa kale.

  Kikundi kimoja cha wataalam wa mambo ya kale cha mji wa Chongqing kinaundwa na watu 14. Watu hao Wanakaa nyumbani kwa wanavijiji, kila asubuhi wanaondoka nyumbani saa 1 na nusu, wakitembea kwa miguu kwa dakika 25, halafu wanatumia kivuko kuvuka mto Changjiang, na kufika katika sehemu ya uchimbaji ambako wanafanya kazi kwa siku nzima. Kazi zao ni kukusanya mabaki ya kale yaliyopatikana, kuyahesabu, kuchora picha, kutengeneza kadi za vitu hivyo na kuandaa ripoti za utafiti wao. Katika miaka 6 iliyopita, eneo la sehemu walizochimba linachukua asilimia 10 ya maeneo yote yanayosubiri kuchimbwa katika sehemu ya magenge matatu. Kiongozi wa kikundi hicho Bw. Bai Jiujiang alieleza kuwa, kazi hiyo si rahisi.

  "Kwetu hakuna siku za Jumamosi na Jumapili, kwa hiyo hatuna siku za mapumziko. Safari hii, inakadiriwa kuwa, tutakaa hapa kwa miezi mitatu. Sisi tunawakumbuka sana jamaa zetu, lakini tunaweza tu kuwapigia simu na kuwaandikia barua. Kila sikukuu zinapowadia, tunasherehekea na kupumzika kwa siku moja, ambapo sisi tunaimba na kucheza karata kwa pamoja, tunakula chakula na kunywa pombe kwa pamoja."

  Kwa maoni ya wataalam hao, kugundua sehemu yenye mabaki mazuri ya kale ni ndoto katika maisha yao. Bw. Huang Wei mwenye umri wa miaka 40 mwaka huu ni profesa mshiriki wa taasisi ya mambo ya kale ya chuo kikuu cha Sichuan. Mwaka 1993, alipewa kazi ya kuhifadhi mabaki ya kale yaliyopo chini ya ardhi katika wilaya ya Yunyang, mjini Chongqing, ambapo aligundua sehemu kadhaa zenye mabaki muhimu ya kale. Na sehemu mojawapo iitwayo Lijiaba iliorodheshwa kama moja ya mafanikio kumi makubwa ya utafiti wa kale katika mwaka 1998 nchini China. Alipogusia jinsi alivyoigundua sehemu hiyo ya Lijiaba, Bw. Huang Wei alisisimka sana. Alisema, "Tulichunguza sura ya sehemu hiyo kufuatia tawi moja la mto Changjiang, na kuwauliza wenyeji wa huko. Walituambia kuwa, kila mwaka kimo cha maji ya mto kilipoongezeka, maji yalileta mapanga mengi. Wenyeji wakasema, mapanga hayo ni ya watu waliokufa. Tulifanya uchunguzi kwa mara kadhaa, tukaona kuwa, sehemu hiyo ina mabaki muhimu ya kale. Mwanzoni tulipoanza kuchimba, tulikuwa na wasiwasi kuwa labda hatutapata kitu, lakini tukagundua baadaye kuwa, sehemu hiyo ni hazina. Kulikuwa kuna makaburi mengi. Tuliendelea na kazi za uchimbaji kwa miezi mitatu mpaka tukachoka kabisa."

  Katika sehemu hiyo ya Lijiaba, Bw. Huang Wei na wenzake waligundua mabaki ya nyumba 55 za miaka 3000 hadi miaka 1500 iliyopita, makaburi zaidi ya 380, majiko manane ya kutengeneza kauri pamoja na vitu vingi vilivyotengenezwa na kauri, mawe ya thamani, mawe ya kawaida na mifupa.

  Hivi sasa, tunauelekea taratibu mwaka 2009 wakati ambapo ujenzi wa mradi wa maji wa magenge matatu utakamilika, na inabidi kukamilisha pia kazi za uchimbaji wa mabaki ya kale katika eneo la bwawa la mradi huo. Naibu mkuu wa taasisi ya mambo ya kale ya mji wa Chongqing, Bw. Zou Houxi alisema kuwa, ingawa kazi yao ni ngumu, lakini wataalam hao watakamilisha kazi yao kabla ya wakati uliopangwa, na kuwaonesha watu duniani ustaarabu wa miaka mingi wa eneo la magenge matatu.

  "Tatizo kubwa tunalokabiliana nalo ni muda mfupi na kazi nyingi. Hata hivyo, mpaka hivi sasa, tumepata ushindi katika vita vigumu kabisa. Mwaka 2003, bwawa la magenge matatu lilikimbikizwa maji hadi kufikia kiwango cha mita 139, na tulikuwa tumemaliza kazi za uchimbaji katika sehemu zilizomezwa na maji, na kazi hizo zinachukua asilimia 60 ya kazi zote. Kutokana na mwendo wa kazi wa hivi sasa, tutaweza kutimiza lengo letu la kumaliza kazi zote kwa muda uliopangwa. Vyombo vingi vya habari vya kigeni vimekuja kutembelea kazi zetu ambavyo vinazifuatilia sana, na kazi zetu zinasifikiwa na wataalamu wenzetu wa mambo ya kale wa nje ya China."

Idhaa ya Kiswahili 2004-02-05