Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2004-02-16 15:55:59    
Confucius na Nadharia Yake

cri

   Confucius

     Mtu yeyote anapozungumzia utamaduni wa China hawezi kuacha kumtaja Confucius. Kwenye miaka ya 70 ya karne iliyopita, msomi mmoja wa Marekani alipoorodhesha watu 100 wenye taathira kubwa kabisa katika historia ya dunia, Confucius alipangwa wa tano, nyuma tu ya Yesu, Sakyamuni ambaye ni mwanzilishi wa dini ya Buddha, na wengine wawili. Lakini miongoni mwa watu wa China, Confucius ni wa kwanza kabisa, kwani kila mmoja hakika ameathiriwa na fikra zake kwa kiasi fulani.

    Katika miaka zaidi ya 2000 iliyopita nchini China, fikra za Confucius sio tu zilikuwa zikiathiri sana siasa na utamaduni, bali pia ziliathiri fikra za kila Mchina, kiasi kwamba hata baadhi ya wasomi wa nchi nyingine walidhani kuwa fikra za Confucius ni imani ya dini fulani nchini China. Lakini kwa kweli fikra za Confucius zilikuwa ni moja tu ya falsafa kadhaa zilizokuwepo katika China ya kale, ni aina ya falsafa, na wala haikuwa imani ya dini. Hata hivyo katika jamii ya kimwinyi ya miaka zaidi ya 2000 nchini China fikra zake zilikuwa zimetukuzwa kama ni fikra sahihi kabisa na zilikuwa na heshima ya kipekee. Fikra za Confucius sio tu zimeathiri kwa kina utamaduni wa China bali pia nchi nyingi za Asia. Hadi leo, kwa sababu Wachina wametapakaa kila pembe ya dunia, fikra za Confucius pia zimevuka China na Asia, na kuenea duniani kote.

    Confucius alizaliwa mwaka 551 K.K. na kufariki mwaka 479 K.K., aliishi kabla ya msomi maarufu wa Ugiriki ya kale, Aristotle, kwa zaidi ya miaka 100. Alipokuwa na umri wa miaka mitatu Conficius alifiwa na baba yake, kisha yeye pamoja na mama yake wakaweka makazi yao katika mkoa wa sasa Shandong uliopo mashariki mwa China. Jina lake la ukoo kwa Kichina ni Kong na jina lake ni Qiu, Wachina humwita "Kong Zi" kwa heshima. Katika jamii ya China ya kale mbele ya jina la ukoo likiongezewa neno "Zi" ina maana ya heshima kwa mtu huyo.

    Zama alizoishi Confucius zilikuwa ni kipindi cha "Spring na Autumn" katika historia ya China. Katika kipindi hicho China iliyoungana ilisambaratika na kuwa madola mengi madogo madogo, na dola alilokuwa akiishi liliitwa Dola la Lu, dola ambalo lilistawi zaidi kiutamaduni kuliko madola mengine.

    Maishani mwake, Confucius hakuwahi kuwa afisa mkubwa, lakini alikuwa na elimu kubwa. Katika China ya kale waliokuwa na fursa maalumu ya kupata elimu walikuwa ni watu kutoka familia za kitajiri tu. Lakini Confucius alivunja utaratibu huo, na alipokea wanafunzi bila kujali wanatoka katika familia gani ikiwa tu watalipa vitu, ikiwa kama ni karo. Confucius aliwaelimisha wanafunzi msimamo wake wa kisiasa na nadharia yake. Inasemekana kuwa jumla walikuwepo wanafunzi elfu 3, na kati ya hao waliibuka wanafikra kadhaa wakubwa kama Confucius, ambao walirithi na kuendeleza fikra zake na kuzieneza sana.

    Lakini je, ni kwa nini fikra za Confucius zilienziwa mpaka zikashika nafasi ya utawala katika zama za kimwinyi nchini China? Hili ni suala ambalo haliwezi kuelezwa kwa maneno machache. Lakini kwa kifupi, fikra zake zilizowagawa watu katika matabaka tofauti na mageuzi yake ya kisiasa yalilingana na manufaa ya tabaka la utawala, na katika zama hizo fikra hizo zilileta matokeo ya kutuliza na kuiendeleza jamii. Confucius alitilia sana mkazo katika utaratibu wa maadili, akiona kwamba ni kosa kubwa kwa watu wa chini kutowaheshimu wakubwa, au watoto kutowaheshimu baba zao. Kutokana na nadharia yake, jukumu la wafalme ni kutawala vyema taifa na jukumu la raia ni kutii wafalme. Pengine mmoja anaweza kuwa na nafasi kadhaa kwa pamoja, maana pengine yeye ni mwana na huku ni baba wa mtu, na labda pia ni afisa, lakini kutokana na mazingira tofauti anapaswa ajiweke katika nafasi yake. Hivyo taifa litakuwa shwari, maisha ya raia yatakuwa ya utulivu.

    Nadharia ya Confucius ilipoibuka haikuwa wazo tawala mara moja hadi kabla ya karne ya pili, China ilipokuwa nchi ya muungano yenye kiini kimoja cha madaraka na ilistawi kwa nguvu. Wakati huo watawala waliona kuwa nadharia ya Confucius inasaidia sana kuleta utulivu wa jamii, ndipo nadharia yake ikatukuzwa na kuwa nadharia ya kutawala taifa.

    Fikra za Confucius zimekusanywa katika kitabu kimoja, nacho ni "Maneneo Yaliyoteuliwa ya Confucius". Katika China ya kale kitabu hicho kilikuwa kama msahafu sawa na biblia ilivyokuwa katika nchi za Magharibi. Raia wa kawaida walikuwa wanajichunga kwa mawazo ya kitabu kicho; Endapo watu walitaka kupata nyadhifa iliwabidi kusoma kitabu hicho kwa undani. Katika historia ya China kuna usemi unaojulikana sana, nao ni "Nusu kitabu cha 'Maneno Yaliyoteuliwa ya Confucius' yanaweza kutawala dunia nzima" maana yake ni kuwa mradi tu ukifuata nusu ya nadharia ya Confucius utaweza kabisa kutawala taifa.

    Kwa kweli Maneno Yaliyoteuliwa ya Confucius sio kitabu cha mahubiri ya maadili tu bali vile vile ni kitabu chenye mambo mengi ikiwa ni pamoja na kusoma vitabu, kuhusu muziki, utalii na kujenga urafiki n.k. Katika kitabu hicho, imeandikwa kuwa mwanafunzi wake mmoja aliyeitwa Zi Gong alimwuliza Confucius kwamba, ikiwa lazima afute moja kati ya jeshi, chakula na raia katika utawala wake, basi ni bora afute lipi? Bila wasiwasi, Confucius akamjibu: jeshi.

    Nadharia ya Confucius inagusia mambo mengi, na baadhi ya mambo hayo yanafuatwa hata katika zama zetu, na maneno aliyosema yalikuwa mengi katika kitabu hicho, hadi sasa baadhi yamekuwa usemi unaojulikana kwa wote, mathalan, "Kati ya watu watatu, hakika mmoja anafaa kuwa mwalimu wangu", maana yake ni kuwa kila mmoja huwa na sifa zake, wanadamu wanapaswa kujifunza kutoka kwa wengine.

Idhaa Ya Kiswahili 2004-02-16