Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2004-03-02 11:01:21    
Mwandishi wa Vitabu Pan Jun

cri

Bwana Pan Jun   

    Mwandishi wa vitabu Pan Jun mwaka huu ana umri wa miaka 47. Kabla ya kuwa na umri wa miaka 30 alikuwa ni mfanyabiashara. Mwaka 1987 alichapisha kitabu chake cha kwanza "Duara ya Mwangaza wa Jua", na tokea hapo aliacha shughuli ya biashara na kujizamisha katika uandishi. Katika muda wa miaka zaidi ya kumi alichapisha riwaya zaidi ya 30, na kuwa mmoja kati ya waandishi walioandika vitabu vingi nchini China.

    Riwaya yake ya "Kujisemea Mwenyewe" yenye sehemu tatu yaani "Nyeupe", "Buluu" na "Nyekundu" imempatia nafasi kubwa miongoni mwa waandishi wa vitabu. Baadhi ya wahakiki wanaona kuwa hiyo ni riwaya nzuri kabisa katika karne ya 20 nchini China. Riwaya yenyewe iliandikwa kutokana na maisha yake halisi kwa kiasi fulani, hata hivyo yeye anaona kuwa kwa mwandishi wa vitabu si lazima awe na maisha halisi aliyoandika katika riwaya yake. Alisema, "Sioni kuwa ni lazima mwandishi wa vitabu awe na maisha halisi aliyoandika katika riwaya yake, bali mwandishi lazima awe na uwezo wa ubunifu. Kwa mfano, mwandishi wa riwaya ya 'Kuuza Damu', Yu Hua, hakuwahi kuwa mkulima lakini alieleza vizuri mkulima aliyeuza damu yake katika riwaya hiyo kuliko waandishi waliowahi kuwa wakulima."

    Dhamira katika riwaya za Pan Jun zinawahusu watu wa kawaida, na zinajaa huruma na utunzaji kwa watu hao. Katika riwaya yake ya "Ndoa ya Mkataba" alieleza mtazamo wake mpya kuhusu utaratibu wa ndoa unaofuatwa hivi sasa. Kadhalika, katika riwaya zake nyingine nyingi ametoa fikra zake zisizo za kawaida kuhusu matatizo yaliyopo katika jamii ya sasa.

    Kuhusu riwaya yake ya "Ripoti kuhusu Hukumu ya Kifo", Pan Jun alisema, aliwahi kuzingatia muda mrefu hukumu ya kifo nchini China, kwa maana nyingine yeye ni mtetezi wa kuondoa hukumu ya aina hiyo ingawa China bado iko mbali na kuibatilisha hukumu ya kifo kutokana na mazingira yalivyo sasa. Lakini anaamini kuwa hukumu ya kifo itabatilishwa tu nchini China kutokana na maendeleo ya binadamu. Alisema, "Thamani ya wasomi ni kuwa na mitazamo yao wakiwa wamesimama kileleni na kuangalia jamii, hii haimaanishi wanaipinga jamii yenyewe, lakini wanapaswa kuikosoa, la sivyo jamii haitaendelea. Wajibu wa waandishi wa vitabu sio kutoa dawa ya kutibu ugonjwa ulioshamiri katika jamii bali ni kuonesha hadharani ugonjwa wenyewe."

    Pan Jun aliongeza kusema kuwa uandishi wake umemhusisha na dunia nzima. Kwa macho ya mwanafasihi anaangalia uwanja wa dunia na kuueleza kwa maandishi yake. Anavutiwa sana mwandishi mashuhuri wa vitabu, Lu Xun. Alisema, "Juzuu Kamili za Lu Xun" kwa uchache alisoma mara nne. Anapenda lugha aliyotumia Lu Xun kutokana na matumizi makini ya lugha ya Kichina. Anaona kuwa mpaka sasa hajaandika maandishi aliyoridhika nayo. Alisema, "Sina lengo la mwisho, maana nikiwa na uwezo nitaendelea kuandika hata baada ya kupata tuzo ya Nobel. Ingawa sasa nimechapisha vitabu vingi na nimejipatia pesa na umaarufu kiasi fulani, lakini nitaendelea. Kwa nini? Jibu ni kuridhisha hamu yangu, kwa kuwa ninao uwezo basi naendelea."

    Pan Jun alieleza, waandishi wa vitabu huwa na shauku za aina mbili: moja ni jukumu la maisha yote, wanaweza kujitolea maisha yao mpaka wanapokufa; shauku nyingine ni kwa ajili ya kujipatia riziki ya kuendesha maisha. Ni wazi kuwa Pan Jun amechagua aina ya kwanza.

Idhaa ya Kiswahili 2004-03-02