Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2004-03-03 21:48:21    
Bibi Wang Xiaoying na miti yake.

cri
    Bibi Wang Xiaoying ni mkazi wa kawaida katika mji wa Shihezi, mkoani Xinjiang, kaskazini magharibi mwa China. Hata hivyo, mwanamke huyo ni maarufu sana mjini humo. Tukiongea na wakazi wa mji wa Shihezi kuhusu Bibi Wang Xiaoying, watu wengi wanamfahamu kuwa, alikuwa amepanda miti katika miaka ya makumi kadhaa iliyopita.

    Mwandishi wetu wa habari alipomkuta Bibi Wang Xiaoying, ilikuwa vigumu kwake kuamini kuwa, mzee huyo mwenye umri wa miaka 70 na urefu wa mita 1.5 tu ndiye aliyepewa sifa ya shujaa wa kupanda miti. Na ni vigumu zaidi kuamini kuwa, mzee huyo mwenye uzito usiozidi kilo 50 aliwahi kuchukua treni na magari akibeba miche ya miti yenye uzito wa mara mbili za uzito wake. Lakini baada ya kuongea sana na Bibi Wang, mwandishi wetu wa habari aliona kuwa, mzee huyo ni mchangamfu, uvumilivu na anayewajibika kupita kiasi.

    Katika miaka ya 50 ya karne iliyopita, Bibi Wang Xiaoying alipokuwa kijana, aliondoka maskani yake mkoani Sichuan, kusini magharibi mwa China, akienda kusoma katika chuo kikuu mjini Wulumuqi, mji mkuu wa mkoa wa Xinjiang. Kwa nini alichagua taaluma ya misitu katika chuo kikuu, Bibi Wang Xiaoying alieleza kuwa, "Mwaka 1952, niliposafiri kutoka Kashi, mji wa kusini mwa mkoa wa Xinjiang hadi Wulumuqi, mji mkuu wa mkoa huo, ilikuwa ni kati ya majira ya Spring na siku za joto, ambapo upepo ulikuwa mkali sana ukiwa na michanga. Nilikuwa nashuhudia jangwa na michanga popote pale. Ilikuwa ni nadhra kuona mti mmoja, lakini tulifurahi sana tukipumzika katika kivuli cha mti. Kwa hiyo, nilikuwa nikakata nia ya kujifunza namna ya kupanda miti, kwa vile mkoa huo wa Xinjinga unahitaji sana miti."

    Muda si mrefu baada ya kuanza masomo katika chuo kikuu, Bibi Wang Xiaoying na wenzake walifanya mazoezi katika mji wa Shihezi, uliopo magharibi mwa mji wa Wulumuqi, ambapo waliweza kupata ufahamu zaidi kuhusu mazingira ya kijiografia ya jangwa. Kuhusu maoni yake ya mwanzo kuhusu mji wa Shihezi, Bibi Wang alisema, "Nilifika nikaona kuwa, kweli lilikuwa ni eneo kubwa sana. Wakati huo, ilikuwa hakuna barabara katika Shihezi, ila tu jangwa na majani yaliyojiotea yenyewe. Na katika kando za mifereji, miti kadhaa mikongwe ilikuwa inaonekana, lakini ilikuwa chache sana kiasi ambacho iliweza kuhesabika."

    Miaka kadhaa baada ya hapo, Bibi Wang alikuwa hakukwenda tena mji wa Shihezi, naye alikuwa amesahau mahala hapa penye umaskini. Lakini kitu asichotarajia ni kwamba, miaka ninne baadaye alipohitimu kutoka kwenye chuo kikuu, alipewa kazi katika mji huo wa Shihezi.

    Bibi Wang alikumbusha kuwa, kwa mara ya pili alifika mji huo, ingawa hali ilikuwa imeboreshwa kwa kiasi ikilinganishwa na ile ya miaka minne iliyopita, lakini mazingira yalikuwa bado ni mabaya, ambapo mjini humo, kulikuwepo jengo moja tu lenye orofa mbili na makazi kadhaa yenye orofa moja ambayo yanazingirwa na eneo pana la jangwa.

    Bibi Wang alipewa kazi katika idara ya kupanda miti na kutunza barabara. Mwanzoni mji wa Shihezi ulipojengwa, upandaji miti na ujenzi wa barabara zilikuwa kazi muhimu sana. Kwa vile, bila ya kinga za misitu, binadamu hawawezi kuishi katika sehemu ya jangwa. Na ujenzi wa barabara ni msingi wa ujenzi wa miji.

    Bibi Wang alisema, wakati huo ilikuwa kawaida kwake kutembelea jangwani, akiwa peke yake pamoja na farasi mmoja, panga moja na mfuko mmoja wa chakula, akifanya uchunguzi na kutafuta aina ya miti inayozoea mazingira ya jangwa. Alisema, akichoka, alikula chakula na kupata usingizi papo hapo jangwani, na zilikuwa mara kadhaa mikate yake aliyochukua mfukoni ilikuwa ikaganda kutokana na hali baridi.

    Kwa vile aina za miti inayokua jangwani ni chache, ilimbidi Bibi Wang kununua aina nyingine za miti kutoka sehemu nyingine, hata alikwenda sehemu iliyopo kilomita kadhaa mbali na mji huo, na halafu alisafirisha miche ya miti hiyo kwa treni au magari. Akikumbusha ugumu wa siku zile, Bibi Wang alisema, "Ili kuchukua miche mingi ya miti, nilipeleka vitu vyangu binafsi vikiwemo dawa ya kusafisha meno na mswaki kusafirishwa kama mizigo, lakini mwenyewe nilichukua mbegu. Unaona urefu wangu ni mdogo, wakati huo nilibeba mbegu wenye uzito wa kilo mia moja hadi mbili. Pamoja na kubeba mabegani, niliweka mfuko mmoja mbele yangu na kuchukua miwili mikononi. Ilikuwa nzito sana, na nilikuwa natembea na kupumzika ili kuwahi treni."

    Bibi Wang alieleza kuwa, safari moja alipoenda sehemu nyingine kununua miche ya miti, aliumwa vibaya takriban kupoteza maisha.

    Kutokana na jitihada za pamoja za Bibi Wang na wenzake, miti mingi zaidi na zaidi ilipandwa mjini Shihezi. Mpaka mwishoni mwa miaka ya 50 ya karne iliyopita, kutokana na upanuzi wa eneo la misitu, idara ya kupanda miti na kutunza barabara pia ilipanuka kutoka watu 100 hadi 300, na Bibi Wang akawa mkuu wa idara hiyo. Wakati huo, misitu ya kukinga upepo tayari imejengwa kuzingira mji huo, na kando za barabara kuu, pia imepandwa miti.

    Hivi sasa, miaka 50 imepita, mazingira ya mji wa Shihezi yameboreshwa sana, ambapo katika mji huo wenye eneo la mita kilomita 400 za mraba, eneo la asilimia 40 limefunikwa na miti au majani, hali ambayo ni nadra kuonekana katika miji iliyopo kaskazini magharibi ya China. Idadi kubwa ya miti pia imeboresha mazingira ya kuishi kwa mji huo. Mwaka 2000, mji huo ulipewa tuzo ya mfano mzuri ya kuboresha mazingira ya kukaa iliyotolewa na Umoja wa mataifa, na mwaka 2002, ulisifiwa kuwa mji wa bustani nchini China.

    Hivi sasa, Bibi Wang Xiaoying amestaafu. Anawasaidia mtoto wake ambaye anaendesha kampuni moja ya bustani, pia anaendelea na utafiti kuhusu mazingira ya kiasili na bustani. Mzee huyo alisema, ingawa hana nguvu ya kupanda miti kwa hivi sasa, lakini angependa kuendelea kutoa mchango kwa kuboresha mazingira ya mji wa Shihezi.

Idhaa ya Kiswahili 2004-03-04