Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2004-03-15 15:21:34    
Maonesho ya Kumbukumbu za Utamaduni wa Dola la Kifalme la Dian

 


cri

   

    Maonesho ya Kumbukumbu za Utamaduni wa Dola la Kifalme la Dian

    Kama mjuavyo, China ni nchi yenye eneo kubwa na makabila mengi, kutokana na hali hiyo utamaduni wake katika sehemu tofauti pia ni wa aina nyingi. Utamaduni uliokuwepo miaka 2,000 iliyopita mkoani Yunnan, kusini-magharibi mwa China ni moja ya aina za tamaduni hizo. Siku hizi "Maonesho ya Kumbukumbu za Utamaduni wa Dola la Kifalme la Dian" yanafanyika mjini Beijing.

    Maonesho hayo ni ya mwisho baada ya kufanyika kwa maonesho mfululizo ya Mkoa wa Gansu uliopo kaskazini magharibi mwa China, Mkoa wa Tibet uliopo kusini magharibi mwa China, Mkoa wa Mongolia ya Ndani uliopo kaskazini mashariki mwa China na Mkoa wa Xinjiang uliopo magharibi mwa China. "Kumbukumbu za Utamaduni wa Dola la Kifalme la Dian" zinaonesha utamaduni wa Dola la Dian uliopotea katika historia ndefu. Mkuu wa Makumbusho ya Kitaifa ya China Bibi Wang Yonghong anaeleza, "Dola la Kifalme la Dian lilikuwa halina maandishi, na maelezo kuhusu dola hilo pia ni machache sana katika nyaraka za zamani, utamaduni wake umepotea katika historia ndefu. Lakini vitu hivi vilivyofukuliwa vimedhihirisha wazi utamaduni wake mbele ya watu wa sasa."

    Dola la Kifalme la Dian lilikuwa ni nchi iliyokuwepo kwa kipindi cha miaka mia 6 hivi kuanzia karne ya tano kabla ya kuzaliwa Kristo hadi karne ya kwanza baada ya kuzaliwa Kristo. Dola hilo lilikuwa katika mkoa wa Yunnan wa sasa, na lilikuwa kubwa kabisa kati ya madola zaidi ya kumi ya makabila madogo madogo kusini magharibi mwa China. Kutokana na hali mbaya ya kijiografia na mawasiliano dola hilo lilikuwa likitengwa na sehemu nyingine za ndani ya China. Kwa mujibu wa kitabu cha "Rekodi ya Historia" kilichoandikwa na mwanahistoria maarufu wa enzi za kale Sima Qian, katika karne ya pili K.K. mfalme wa Enzi ya Han, nchi kubwa iliyokuwa ndani ya bara, Han Wudi, aliwahi kutuma mjumbe wake kwenye dola hilo. Mfalme wa Dola la Dian alimwuliza mjumbe, "Je, dola langu Dian na lenu Han lipi ni kubwa?". Hilo ni swali la kuchekesha, kwani dola la Han lilikuwa ni kubwa mno likilinganishwa na dola la Dian. Kwa sababu ya kutokuwa na maandishi, hadi kufikia karne ya kwanza B.K. utamaduni wa dola hilo ulikuwa umepotea kabisa.

    Katika maonesho hayo vitu 179 vinaoneshwa, na kati ya vitu hivyo vinavyovutia zaidi ni vyombo vya shaba nyeusi. Dola la Kifalme la Dian lilikuwa mkoani Yunnan, ambapo kuna utajiri wa madini ya shaba na risasi na utajiri huo ulileta utamaduni wa dola hilo katika matengenezo ya vyombo vya shaba nyeusi, sanaa za vyombo vyake hata sasa zinastaajabisha. Kutokana na maelezo, vyombo vya shaba nyeusi vilivyofukuliwa katika mkoa huo vinapatikana zaidi ya elfu 10 vya aina zaidi ya 90. Naibu mkuu wa Makumbusho ya Kitaifa ya China Bw. Dong Qi anaona kuwa utamaduni wa Dola la Kifalme la Dian ni utamaduni wa shaba nyeusi. Alisema, "Hapa duniani, utamaduni wa vyombo vya shaba nyeusi katika zama za kale nchini China ni maarufu sana, hasa vile vya enzi za Shang na Zhou, lakini vyombo vya shaba nyeusi vya Dola la Dian vinachukua nafasi kubwa katika utamaduni wa China."

    Kati ya vyombo hivyo vinavyooneshwa, kuna silaha, ala za muziki na vyombo vya kutumika katika maisha pamoja na mapambo, na kwenye vyombo hivyo ilichorwa michoro ya binadamu, wanyama, mimea, uwindaji, ufugaji, vita, matambiko na ngoma. Michoro hiyo ni kama maelezo kuhusu zama zile.

    Ufundi wa kutengeneza vyombo hivyo ni wa ajabu. Kwa mfano, kati ya vitu vilivyooneshwa kuna meza moja ya shaba yenye sura za ng'ombe na chui, kimo cha meza hiyo ni sentimita 40 na urefu 70, miguu ya meza ni ya miguu ya ng'ombe, na uso wa meza ni mgongo wa ng'ombe kwa umbo la yai, chui aliyesimama aking'ata mkia wa ng'ombe na miguu yake minne ikimkamata matako ya ng'ombe, tumbo la ng'ombe ni nafasi tupu na ndani yake amejificha ndama. Meza hiyo ilibuniwa kwa mawazo ya ajabu na wanyama hao wanaonekana kama walivyo hai. Hii ni sanaa isiyo ya kawaida katika vyombo vya shaba nyeusi.

    Kuhusu michoro iliyochorwa kwenye vyombo hivyo, mtazamaji Bw. Yu Wenqing aliwaambia waandishi wa habari, akisema, "Sikutegemea vyombo vizuri kama hivi vingefukuliwa katika mkoa wa Yunnan, kweli ni ajabu, watu wa Dola la Dian waliweza kutengeneza vyombo hivi vizuri hata kabla miaka elfu mbili iliyopita!"

    Miongoni mwa vitu vilivyooneshwa kuna mhuri mmoja wa dhahabu. Kutokana na maandishi ya kitabu cha "Rekodi ya Historia", mfalme wa Enzi ya Han aliwahi kuwapa wafalme wa madola mawili mihuri ya dhahabu baada ya kuyateka madola yote yaliyoko kusini magharibi mwa China. Huu ni mhuri mmojawapo uliofukuliwa mwaka 1956, umehakikisha kilichoandikwa katika kitabu cha "Rekodi ya Historia", lakini mhuri mwingine hadi sasa bado haujagunduliwa. Kwa hiyo mhuri huo ni wa thamani sana.

    Miongoni mwa vitu vilivyooneshwa pia vimedhihirisha uhusiano wa dola hilo na sehemu nyingine za Asia. Kwa mfano, michoro kwenye sahani moja yenye wacheza ngoma wawili, nao wana sura zenye pua ndefu, macho ya kuzama, mavazi na mapambo yaonekana ni watu waliotoka Asia ya magharibi.

   Maonesho ya vyombo vya shaba nyeusi vya Dola la Kifalme la Dian yanaeleza jamii, historia na sanaa zilivyokuwa katika dola hilo. Sehemu lilipokuwepo Dola hilo yaani mkoa wa Yunnan pia ni sehemu ya ajabu hadi sasa, kwa hiyo inavutia watalii wengi nchini na kutoka nchi za nje.

Idhaa ya Kiswahili 2004-03-07