Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2004-03-10 10:00:10    
Bw. Song Fengnian, mbunge mkulima wa Bunge la Umma la China 

cri
    Nje ya mji wa Zhengzhou, ambao ni mji mkuu wa mkoa wa Henan uliopo katikati ya China, kuna kijiji kiitwacho Song Zhai. Ukifanya matembezi katika kijiji hicho, utajikuta katika makazi safi, maeneo yenye nyasi na wakazi wenye furaha, hali ambayo ni sawa na ile inavyoonekana mijini. Lakini kijiji hicho zamani kilikuwa ni maarufu kwa uchafu na umaskini, na mabadiliko yake makubwa ya namna hii yametokana na juhudi za mbunge wa bunge la umma la taifa aitwaye Song Fengnian.

    Bw. Song Fengnian mwenye umri wa miaka 57 ni mkazi wa kijiji cha Song Zhai. Yeye ni mrefu, na anapoongea hupenda kuangalia mbele akifanya macho yake madogo. Anapendelea mavazi ya kimagharibi na sanaa ya maandiko ya Kichina, na anaonekana kama wakulima wenzake. Mbunge huyo alimwambia mwandishi wetu wa habari kuwa, ameandaa mswada wa kupambana na umaskini kwa ajili ya mkutano wa Bunge la Umma la China wa mwaka huu.

    "Kwa maoni yangu, haifai kuwapatia misaada watu maskini tu bali serikali ingewasaidia zaidi watu wanaokumbwa na maafa. Sifurahii serikali siku zote kuwasaidia watu maskini, naona kuwa, hii ni njia ya muda tu ya kutatua suala la umaskini. Inapaswa kuisaidia sehemu moja ili imudu kutatua matatizo yake kwa kutegemea mazingira na hali ilivyo. Maana yake ni kwamba, tayari nimejenga barabara na kuboresha mazingira, halafu nakuacha wewe mwenyewe ujitafutie pesa kwa kuchapa kazi. Hii ndiyo mbinu ya kupambana na umaskini. Kwa hiyo, ninataka serikali itofautishe hatua za kuondoa umaskini na kutoa misaada kwa watu wanaokumbwa na maafa."

    Bw. Song amekuwa na maoni hayo kutokana na mambo aliyoshuhudia mwenyewe wakati alipowaongoza wanakijiji wenzake wa kijiji cha Song Zhai kupambana na umaskini.

    Mwanzoni, Song Zhai kilikuwa kijiji maarufu kwa umaskini wake nje ya Zhengzhou, mji mkuu wa mkoa wa Henan. Katika sehemu hiyo, kuna msemo usemao, "Usimruhusu binti yako aolewe na mvulana wa Song Zhai". Siku nenda siku rudi, wakulima wa kijiji cha Song Zhai walikuwa wanategemea mashamba machache yasiyo na rutuba pamoja na misaada ya serikali. Lakini Bw. Song Fengnian aliyezaliwa katika kijiji hicho hafurahii maisha yenye umaskini waliyonayo wazee wa huko. Tokea mwanzoni mwa miaka ya 80 ya karne iliyopita, akiwa mkuu wa kijiji hicho, Bw. Song pamoja na wanakijiji wenzake walianza kujitafutia mbinu za kuchuma pesa.

    Kwa kutegemea sera nzuri zilizotolewa na serikali ya China ilipoanza kufanya mageuzi na kufungua mlango kwa nje, Bw. Song Fengnian alilenga masoko ya mijini. Chini ya uongozi wake, wakulima wa kijiji cha Song Zhai walianza kupanda miti ya matunda yenye sifa nzuri kama vile zabuni, walinunua malori na kujishughulisha na biashara ya uchukuzi wa mbao, walianzisha kiwanda cha kutengeneza samani ambazo zilikuwa zinanunuliwa na wakazi wa mijini. Walipogundua kuwa kulikuwepo aina chache za rangi za kupaka kwenye samani, walijenga kiwanda cha kutengeneza rangi, na walipoona kuwa, viwanda vingi vinakosa sehemu za kujenga karakanaka mijini, walianza kuvutia mitaji ya viwanda hivyo kwa kutumia mashamba yasiyotumika. Kadiri uchumi wa China unavyoendelea, ndivyo biashara za kijiji cha Song Zhai zinavyopamba moto siku hadi siku, na maisha ya wanakijiji pia yanaboreshwa. Hivi sasa wasichana wengi warembo wanapendelea kupata wachumba kutoka katika kijiji hicho.

    Bw. Song Fengnian alimwambia mwandishi wa habari kuwa, hivi sasa wastani wa pato la wanakijiji wa Song Zhai kwa mwaka ni Renminbi Yuan elfu 6 (sawa na dola za kimarekani 730), mbali na mashamba, thamani ya mali zisizohamishika za kijiji hicho imezidi Yuan bilioni moja (sawa na dola za kimarekani milioni 120). Kijiji hicho kilichokuwa maarufu kwa umaskini hapo mwanzoni, sasa kimebadilika kuwa kijiji tajiri ambacho watu wengi wangependa kuhamia.

    "Maisha ya watu yamekuwa yakibadilika hatua kwa hatua. Mwanzoni katika kijiji chetu, kulikuwa na wakulima zaidi ya 600. Na hivi sasa, mbali na wanakijiji, pia kuna watu wapatao elfu 5 walioajiriwa na viwanda vya kijiji."

Hivi sasa Kijiji cha Song Zhai kimepata fedha. Bw. Song na wenzake wamejenga nyumba mpya na kupanda miti kwa ajili ya kuinua kiwango cha maisha ya wanakijiji. Walijenga majengo 19 yenye jumla ya seti 700 za makazi ambazo tayari zina simu, mfumo wa joto na huduma ya television (cable), na chini ya majengo hayo, kuna shule, shule za kuwatunza watoto wadogo, maduka, hospitali na klabu.

    Bw. Song alisema, kutokana na jitihada za miaka ya hivi karibuni, amepata maoni kuwa, sehemu yenye umaskini ikitaka kujiendeleza, inapaswa kujitafutia mbinu za kupata pesa badala ya kutegemea tu misaada ya serikali. Alifafanua kuwa, kuwapa pesa watu waliopo sehemu maskini hakuna maana sana, bali kunawafanya wawe na tabia mbaya ya kusubiri, kutegemea na kuomba misaada. Alipendekeza kuwa, serikali ingechukua hatua nyingine zikiwemo kujenga barabara na kujenga mtandao wa umeme kwa kuboresha mazingira ya sehemu hiyo, na kuwaacha wenyeji wajiendeleze wenyewe.

    Mbunge huyo alimwambia mwandishi wetu wa habari kuwa, amejifunza mengi katika miaka iliyopita alipokuwa akiwaongoza wanakijiji wenzake kutafuta pesa. Alisema, matokeo yake makubwa ni kuwa, wanakijiji wanamchukulia kama jamaa yao, jambo ambalo linamfurahisha sana. Alitoa mfano mmoja kuwa, siku moja alikumbwa na ugonjwa mbaya wa moyo, alipaswa kufanyiwa upasuaji mkubwa, lakini alikosa pesa. Wanakijiji wenzake walipopata habari hiyo, waliuza mayai na nafaka ili kupata fedha za kumsaidia.

    Mwaka 1998, Bw. Song Fengnian alichaguliwa kuwa mbunge kwa mara ya kwanza. Na kuanzia hapo, mbali na kushughulikia shughuli za kijiji chake cha Song Zhai, anawatembelea wakulima wa vijiji vingine, akisikiliza matatizo yao na kuyashughulikia kwa makini. Kuna mifano mingi: mkulima mmoja wa mkoa wa Henan na kada wa kijiji chake walikuwa na migongano, Bw. Song alizungumza na kada huyo na kutatua migongano hiyo papo hapo; mkulima mwingine alinunua madawa bandia ya kuua vijidudu, Bw. Song alimsaidia kuokoa hasara zake.

    Baada ya kuchaguliwa kuwa mbunge wa taifa, Bw. Song Fengnian alikuwa ametembelea vijiji vyote vilivyopo karibu. Hivi sasa, mbunge huyo ni maarufu sana kwa kuwasaidia wakulima katika kuondoa matatizo yao, na wakulima wanafurahia kumtafuta ili kupata msaada wake.

    Hata hivyo, mbunge huyo mkulima, yeye mwenyewe alisema hakumbuki kuwa amewasaidia wakulima wengapi. "Sikumbuki majina na idadi ya watu. Nikiwa mbunge wa taifa, ni wajibu wangu wa kujitoa kushughulikia mambo ya namna hii. Nikiwa na uwezo wa kuwasaidia, nitawasaidia kutatua matatizo. Ninafurahia kuwa mbunge, pia nina nia ya kuwa mbunge mzuri. Wachina wenye umri kama wangu wanafanana kwa kuwa, tokea utotoni mwetu, tulifundishwa kuwa tunatakiwa kuwahudumia wananchi, hivyo siwezi kubadilisha tabia hii hata hivi sasa."

    Mwaka jana, Bw. Song kwa mara nyingine tena alichaguliwa kuwa mbunge wa taifa. Alisema kuwa, maendeleo ya sehemu ya vijijini hayawezi kupatikana bila mchango wa wakulima. Akiwa mbunge mkulima, inambidi kusikiliza maoni ya wakulima wengi.

Idhaa ya Kiswahili 2004-03-11