|
Sanaa ya vichongo vidogo ina historia ndefu sana nchini China. Mapema Enzi ya Zhou ya Magharibi ya karne ya 11-8 K.K, katika masalio ya mifupa ya wanyama iliyochongwa maneno kulikuwa na ramli ambayo haikuweza kusomwa haraka kwa kikuzi cha mara tano. Katika Enzi ya Ming (1368-1644) na Enzi ya Qing (1616-1911), wataalamu wengi wa vichongo vidogo walijitokeza nchini China, na kuuachia ulimwengu sanaa yenye thamani kubwa. Kwa kawaida, ufundi wao ulirithiwa kutoka kwa wazazi kwenda kwa watoto au kutoka kwa walimu kwenda kwa wanafunzi.
Bwana Guo Wenan, mtaalamu wa vichongo vidogo aliingia Kiwanda cha Michongo ya Jade ya Bengbu alipokuwa na umri wa miaka 13. Mchongo wa "Farasi Akanyaga Juu ya Mbayuwayu Anayeruka" ulimpatia umaarufu mkubwa. Baada ya kufunga pingu za maisha na Bi Yang Xiaozhu, ambaye vilevile alikuwa fundi wa kuchonga, alianza kujifunza vichongo vidogo vya meno ya ndovu kutoka kwa baba mkwe wake, ambaye alizaliwa katika familia ya wachongaji wa vichongo vidogo. Kwa miaka mingi sasa, Bw. Guo anakumbuka vizuri ushauri wa mwalimu wake, "Jifunze vizuri ufundi wa msingi na fanya kazi kwa bidii kuliko watu wengine." Bw. Guo alisanifu vichongo vidogo vya hali ya juu, k.v. "Kugombanisha Kondoo", "Farasi Anayesimama", picha za viongozi mashuhuri na watu wa kale.
Bw. Guo alisanifu kichongo kidogo kiitwacho "Chupa na Minyororo", ambacho kilipewa sifa kubwa katika maonesho kadhaa ya nchini na ya ng'ambo. Chupa hiyo ilichongwa kwenye kipande cha pembe ya ndovu chenye ukubwa wa milimita 10×7. Mtu hawezi kuiona nakshi ya chupa hiyo mpaka atumie kikuzi. Kila upande wa chupa kuna mnyororo wa duara, juu ya chupa ziko duara tatu za minyororo na maneno ya "Maisha marefu" yaliyochongwa. Upande mmoja wa chupa una mchoro wa babu anayepanda kungulu, kijana anayeongoza kungulu huyo, kijana anayeshika fimbo ya babu na kijana anayechukua pera. Ulingano wa urefu wa watu hao wanne ni sahihi. Upande mwingine wa chupa una maneno yaliyochongwa na marehemu baba mkwe wa Bw. Guo yasemayo "Maisha ni marefu kama umri wa milima; baraka ni kubwa kama ukubwa wa bahari."
Vichongo vya Bw. Guo vimependwa sana na masogoro wa nchini na wa ng'ambo. Kikundi cha kupiga picha za filamu za televisheni kutoka Taiwan kilifanya matembezi na kupiga picha za filamu ya kuujulisha ulimwengu ufundi wa Bw. Guo; Mji wa Utamaduni wa Kimataifa uliopo mjini Qinhuangdao umefungua banda maalumu la kuonesha vichongo vidogo vya Guo; Idara ya utamaduni ya Japani ilimwalika Bw. Guo kwenda Japani kufanya maonesho.
Idhaa ya kisawahili 2004-03-16
|