Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2004-03-24 11:16:05    
Ugonjwa wa kifua kikuu, adui mkubwa kwa afya ya binadamu

cri
    Leo, tarehe 24, Machi ni siku ya kifua kikuu duniani.

    Kutokana na takwimu zisizokamilika, hivi sasa kuna wagonjwa wa kifua kikuu wapatao milioni 20 duniani. Na kila mwaka, idadi ya watu wanaoambukizwa ugonjwa huo inaongezeka kwa milioni 8 na watu wapatao milioni 2 wanakufa kila mwaka kwa ugonjwa wa kifua kikuu. Ugonjwa huo wa kuambukiza ambao umekuwepo toka enzi za kale umerudi tena na kuwa adui mkubwa kwa afya ya binadamu.

    Ugonjwa wa kifua kikuu umekuwepo tangu zamani sana. Wanasayansi waligundua dalili za ugonjwa huo katika maiti za misri zilizohifadhiwa za miaka elfu 6 iliyopita. Katika historia, ugonjwa huo uliambukiza watu wengi na kuleta vifo vingi.

    Tarehe 24, Machi miaka 120 iliyopita, daktari wa Ujerumani Bw. Robert Kohe aligundua virusi vya kifua kikuu. Hii ilikuwa ni hatua kubwa ya kuelekea ushindi kwa binadamu katika mapambano dhidi ya ugonjwa huo yaliyoendelea kwa maelfu ya miaka. Hadi kufikia miaka ya 40 na 50 ya karne iliyopita, madawa mazuri ya kutibu ugonjwa wa kifua kikuu yalikuwa yamepatikana.

    Hata hivyo, ugonjwa huo bado haujaangammizwa mpaka hivi sasa, kwa kuwa, wagonjwa wengi wanashindwa kutumia madawa hayo ambayo ni ghali, hadi kupona kabisa. Wataalamu wamefafanua kuwa, iwapo madawa yatatumika kwa mfululizo kwa miezi 6 hadi minane ya kwanza baada ya maambukizi, asilimia 95 ya wagonjwa wanaweza kupona kabisa, na hawataweza kuwaambukiza wengine. La sivyo, virusi vya kifua kikuu vitakuwa sugu katika kupambana na madawa, ambapo ni vigumu sana kwa wagonjwa kupona kabisa. Aidha, wagonjwa wa namna hii wanaweza kuambukiza watu wengine virusi vya kifua kikuu vilivyo sugu kwa madawa, hivyo kuleta athari mbaya zaidi.

    Hivi sasa, maeneo yaliyoathiriwa vibaya na ugonjwa wa kifua kikuu ni mabara ya Asia na Afrika, hususan Asia, inachukua theluthi mbili ya wagonjwa wa kifua kikuu duniani.

    Hali ya kuongezeka kwa idadi ya watu wenye ugonjwa huo inasababishwa na sababu kadhaa kubwa, zikiwemo ya kwanza, nchi nyingi zinakosa mpango wa kupambana na ugonjwa wa kifua kikuu katika kudhibiti uenezi wake, ambapo wagonjwa wengi wanashindwa kutibiwa mpaka wapone kabisa, hali ambayo imesababisha kuwepo kwa virusi sugu vya kifua kikuu. Sababu ya pili ni maambukizi mabaya ya kifua kikuu pamoja na ukimwi. Watu wanaoishi na virusi vya maradhi hayo mawili wanakabiliwa na hatari zaidi ya kuugua kifua kikuu mara 30 hadi 50 kuliko watu wanaoishi na virusi vya kifua kikuu peke yake. Na sababu kuu ya tatu ni kuwa, maendeleo ya miji, mazingira yanayoharibika, umaskini, wimbi la wakimbizi, vita na mapigano pamoja na watalii wanaotembea duniani, hayo yote yamechangia kuenea kwa ugonjwa wa kifua kikuu.

Idhaa ya Kiswahili 2004-03-24