Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2004-03-26 19:57:19    
Ukuta Mkuu wa China

cri
    Mwaka 1985 serikali ya China ilijiunga na "Mkataba wa Urithi wa Dunia", na mwaka 1987, kumbukumbu 6 za urithi wa China ikiwa ni pamoja na Ukuta Mkuu na Kasri ya Kifalme ya China viliwekwa kwenye orodha ya urithi wa dunia, hadi sasa kumbukumbu 29 za urithi wa China zimeorodheshwa katika urithi wa dunia, idadi hiyo imeifanya China kuwa ya nchi ya tatu duniani kuwa na kumbukumbu nyingi za urithi.

    Ukuta Mkuu unasifiwa kama ni "moja katika maajabu saba ya dunia", ni mradi mkubwa ambao ulijengwa kwa miaka mingi na kazi kubwa duniani katika ujenzi wa ngome zote za kuzuia maadui katika zama za kale. Ukuta huo una urefu wa zaidi ya kilomita 7,000 nchini China.

    Historia ya ujenzi wa ukuta huo inaweza kufuatiliwa hadi karne ya 9 kabla ya Kristo. Katika kipindi cha "Madola ya Kivita" kilichokuwa kati ya mwaka 770 na 476, madola yalikuwa yakipigana vita na kila moja likitaka kuliangamiza lingine ili kupata utawala wa China nzima, kutokana na sababu hiyo kila dola lilijenga ukuta milimani kwenye mipaka ili kuzuia mashambulizi ya maadui. Mwaka 221 kabla ya Kristo, mfalme Qin Shihuang aliiunganisha China nzima, kisha akaziunganisha kuta zote zilizojengwa na madola hapo awali na zikawa ukuta uliopo milimani kwenye sehemu ya kaskazini ili kuzuia askari wenye farasi wa kabila la wafugaji walioishi nje ya sehemu ya kaskazini, wakati huo ukuta huu ulikuwa na urefu wa kilomita zaidi ya elfu 5. Baada ya Enzi ya Qin, Enzi ya Han ilirefusha ukuta huo na kuufanya kuwa na kilomita zaidi ya elfu 10. Katika miaka zaidi ya elfu mbili, kila enzi ilizidi kuongeza urefu na kuufanya ukuta huo kuwa na kilomita elfu 50, urefu ambao unaweza kuizunguka dunia kwa zaidi ya duara moja kwa kufuata ikweta.

    Siku hizi watu wanapotaja "ukuta mkuu" huwa wanalenga ukuta uliojengwa katika Enzi ya Ming, enzi iliyokuwa kati ya mwaka 1368 na 1644 baada ya Kristo. Ukuta huo unaanzia sehemu ya Jiayuguan, mkoani Gansu magharibi mwa China hadi kwenye ukingo wa mto Yalujiang, mkoani Heilongjiang mashariki mwa China, urefu wake ni kilomita elfu saba na mia tatu ukipita mikoa na miji tisa.

    Ukuta huo uliojengwa milimani unapita sehemu za jangwa, mbuga za majani na ardhi oevu, unainuka na kushuka, unapindapinda, ukionesha vya kutosha akili za wahenga wa China. Nje ya ukuta ni magema, ukuta na magema yanasaidiana kuzidisha kinga. Katika zama za kale, maadui wakitaka kuparamia magema makali na kufikia kwenye ukuta na kufanya mashambulizi kwa kubinua shingo nyuma ilikuwa ni vigumu na pengine haikuwezekana.

    Ukuta ulijengwa kwa matofali makubwa na mawe makubwa kwa nje, na ndani ulijazwa kwa udongo na kokoto, kimo chake ni mita 10 na upana wa mita 5, upana huo ni wa kutosha kwa ajili ya askari kufanya vita na kupeleka mahitaji ya vita kama chakula na silaha. Kwa upande wa ndani ukuta huo una ngazi za mawe na mapango kurahisisha kupanda na kushuka ukutani. Kila baada ya safari fulani hujengwa dungu kwa ajili ya kuwekea silaha, chakula na kupumzika kwa askari, maadui wakija moto huwashwa juu ya dungu hizo ukitoa mwanga na moshi kupasha habari.

    Katika zama za leo ingawa ukuta huo hauna maana katika mambo ya kijeshi lakini ujenzi wake unastaajabisha sana.

    Kwa mbali ukuta huo unaonekana wenye fahari na taadhima, unapindapinda kama nyoka mkubwa kwenye migongo ya milima. Kwa karibu unaonekana umejengwa kwa makini na werevu juu ya majabali, na dungu za kuwashia moto zinazounganisha ukuta huo kila baada ya urefu fulani zinaonesha uhodari mkubwa wa wajenzi.

    Ukuta huo licha ya kuwa na maana muhimu katika historia, pia una maana katika utalii. Nchini China watu husema "Asiyefika kwenye Ukuta Mkuu sio jabari", watalii wa nchini na wa nchi za nje huona fahari kufika kwenye ukuta huo hata viongozi wa kitaifa wa nchi za nje, na watalii huwa wengi siku zote.

    Kwa kweli Ukuta Mkuu umelowa jasho na damu za wahenga wa China na pia ni matokeo ya akili za mababu wa China. Ukuta huo umepita miaka zaidi ya elfu moja bila kuanguka, sifa yake haijapotea, umekuwa ni ishara ya taifa la China. Mwaka 1987 ukuta huo uliorodheshwa kwenye Urithi wa Dunia kwa jina la "ishara ya taifa la China".

Idhaa ya kiswahili 2004-03-25