Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2004-03-29 15:38:45    
Wasanii wa Kike Nchini China

cri
    Siku chache zilizopita wasanii kadhaa wa kike walifanya maonesho ya sanaa mjini Beijing. Sanaa zilizooneshwa zilikuwa ni pamoja na picha za kuchorwa na sanamu za kuchongwa. Sanaa hizo zilionesha jinsi wasanii hao wanavyoiona dunia ya leo na maisha ya binadamu kutokana na mtizamo wa wanawake.

    Kuanzia miaka ya 90 ya karne iliyopita, sanaa za wanawake ziliibuka na kuvutia zaidi katika uwanja wa sanaa. Kutokana na jinsi mtizamo wa wanawake wasanii hao wanaonesha jinsi wanavyoiona dunia na jinsi maisha ya binadamu yalivyo.

    Wasanii wa kike walioshiriki katika maonesho hayo wote walizaliwa katika miaka ya 70, na wengi walipata elimu ya kutosha katika vyuo vikuu vya uchoraji. Kutokana na kuupenda usanii, walichagua kazi ya kujiajiri ili wawe na uhuru wa kutumia muda wao. Mkuu wa Jumba la Maonesho ya Uchoraji mjini Beijing, Bibi Shang Fang alipowazungumzia wasanii hao alisema, "Wasanii wa kike sasa wako katika kipindi cha maendeleo ya haraka, kutokana na mtazamo wa wanawake wanaonesha fikra zao za sasa zilizo tofauti na za zamani. Na baadhi yao wanajulikana hata katika nchi za nje. Sanaa zao ziko katika safu ya mbele katika sanaa zote ikiwa ni pamoja na za wanaume."

    Mchoraji wa kike Zhou Yan alichora picha yenye watu wadogo wadogo waliomo ndani na chupa ndogo zinazoelea majini, aliipa picha hiyo jina la "Kuelea". Alisema, watu wadogo wadogo aliowachora ni wanawake wa zama hizi jinsi walivyobanwa na mazingira na jinsi walivyokosa uhuru wa kujiamulia mambo. Chupa zinaelea baharini. Wanawake wanapaswa kufikiri mambo mengi kuliko wanaume, na miiko waliyowekewa ni mingi kuliko wanaume, wanahitaji kutunzwa  na kulindwa na wanatamani kupata watu wa kuwaelewa. Lakini hali ilivyo ni kwamba dunia ni kubwa na mambo hubadilika badilika, hali hiyo inawafanya wasiwe na amani mioyoni. Maisha yao yalitiwa ndani ya chupa ndogo ambazo zinaelea baharini zikipigwa na mawimbi makali, na wakati wowote chupa hizo zingeweza kuvunjika.

    Picha aliyochora Ye Nan kwa jina la "Ukiwa" ni picha inayoweza kumtia huzuni mtazamaji, ni picha ambayo inaonesha fikra nzito kuhusu maisha ya biandamu yalivyo. Ye Nan aliwahi kuishi na kujifunza uchoraji kwa miaka 7 nchini Russia, lakini alipokuwa akifundishwa mwalimu wake alifariki dunia, na wakati huo ndipo Russia ilipokuwa katika mabadiliko makubwa ya kisiasa, maisha yalimwia magumu na yenye ukiwa. Picha yake hiyo ilipata tuzo ya Chuo Kikuu cha Uchoraji cha Russia na imehifadhiwa katika makumbusho ya uchoraji ya Russia.

    Wang Peng ni msanii wa uchongaji wa sanamu. Kutokana na mtazamo wa wanawake alichunguza kila kipindi cha maisha ya binadamu, ana fikra zake mwenyewe kuhusu vijana na pia ana wasiwasi kuhusu watoto. Sanamu yake "Udhibiti" inaonesha utunzaji kwa mtoto wake huku akitaka mtoto wake amtii. Na sanamu yake nyingine aliyoipa jina la "Mwanamke Mdogo" inaonesha jinsi anavyouona ulimwengu. Wang Peng alisema, wafanyakazi wa kike siku zote wanazongwa na kazi. Alisema, "Mara nyingi nawakuta wanawake wakiharakisha kwenda kazini na huku mawazo yao yakiwa mbali. Watoto wanakuwa kama kitu kilichosahauliwa kifuani mwao." Alisema kuwa katika hali kama hiyo siku nenda siku rudi, watapuuza mambo mengi mazuri na muhimu.

    Picha kwa jina la "Watoto wa Kiume na wa Kike" na "Mvua Itanyesha" ni picha za aina nyingine kabisa ambazo zimechorwa kwa mchanganyiko wa mtindo wa Kimashariki na wa Kimagharibi. Mchoraji wa picha hizo Wang Tiantian aliwahi kuishi mjini New York, ana mtizamo wake mwenyewe kuhusu jamii iliyostawi kwa utajiri wa biashara. Picha yake nyingine "Nguo", inaonesha wanawake waliotamani ufahari kwa kupata nguo safi, sketi ya fahari, mkoba wa bei ghali na vitu vingine vya anasa, lakini kwenye mkoba mchoraji alichora tundu akionesha tamaa zake nyingi hazitakuwa na mwisho, mwishoni atabaki na upweke baada ya kuridhika na vyote alivyotaka.

    Shen Ling ni mchoraji jasiri. Picha yake "Niangalie" inaonesha mapenzi ya wanaume na wanawake. Miaka 9 iliyopita mchoraji huyo alipokuwa mama, maisha yake yakabadilika. Baada ya kuwa mama amekuwa na mtazamo mpya katika kuangalia mambo. Bi. Shen Ling alisema, "Wanawake lazima wawe na heshima, wawe na haki ya uhuru wao, ni tofauti kati ya mambo wanayotilia maanani na wanaume, ukiwa na msimamo wa kukubali tofauti hiyo katika kuangalia dunia hii kwa mtizamo wa wanawake, basi utakuwa na fikra nyingine, hii ndio maana ya kuweko kwa wanawake duniani na pia ni hoja ya wanaume kuwa na heshima kwa wanawake, wanawake haifai kuacha tabia zao za asili" Shen Ling alisema, wanawake wa zama hizi wana bahati nzuri, hawabaguliwi, bali akiwa mchoraji wa kike anaheshimiwa katika jamii.

    Mchoraji mwingine Zhag Yonghong ni mchoraji mpole, katika picha zake nyingi zinaonesha wasichana wasio na miiko wenye furaha tele ya kitoto. Alisema, "Kuchora picha ni kama kuzaa mtoto, baada ya "mtoto kuzaliwa" utaitunza kwa macho ya watazamaji kuisaidia kukua."

    Maonesho ya sanaa za wanawake yanavutia watazamaji wengi. Ingawa wasanii wa kike sio wengi sana katika zama zetu lakini ni kundi la wasanii ambalo haifai kupuuzwa machoni mwa watu.

Idhaa ya kiswahili 2004-03-29