Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2004-04-04 21:54:58    
Barua za wasikilizaji wetu 4/4/2004

cri
    Msikilizaji wetu Mutanda Ayub Sharriff ametuletea barua akisema kuwa, hana budi kutupongeza kwa matangazo ambayo yamezidi kupamba moto. Haswa habari za kutoka kote duniani na kipindi cha sanduku la barua kimekuwa cha kuelimisha mno. Anasema anaendelea kujifunza mengi kutoka kwa mashabiki wengine kutoka nchi mbalimbali.

    Anasema vilevile anatuma salamu za ijumaa njema na siku ya pasaka kwa wakristo wote kupitia idhaa ya kiswahili ya Radio China kimataifa, ingawa hapo Kenya huu ni msimu wa upandaji wa mimea kama mahindi, mtama, wimbi, maharagwe, soya na kadhalika. Wakristo hawana budi kujiandaa kusherehekea sikukuu ya pasaka ambayo huwa ni ukumbusho wa kufa na kufufuka kwa Yesu Kristo. Kwani inafahamika kuwa alikufa siku ya ijumaa na akafufuka siku ya jumapili ndiyo sababu huko Kenya hii siku huwa ni sikukuu.

    Anasema sherehe hii ambayo husherehekewa kila mwaka kati ya mwezi wa tatu na wa nne. Kwa mwaka huu itakuwa tarehe 9 na tarehe 12 Aprili mwaka 2004. Kwa siku hiyo wakristo hubeba matawi ya miti wakizunguka kati ya miji kama ishara ya kukumbuka ama kumbukumbu ya siku hiyo. Kwa hivyo Bwana Sharriff anasema ombi lake ni kwamba ikiwezekana hii barua iweze kusomwa kabla ya siku hiyo ili wasiofahamu waweze kujua.

    Tunamshukuru Bwana Sharriff kutuletea habari kuhusu siku ya pasaka na namna wakenya walivyosherehekea siku hiyo.

    Msikilizaji wetu Mbarouk Msabah wa Dubai United Arab Emirates ametuletea barua akisema kuwa, marehemu Deng Xiaoping ni kiongozi anayekumbukwa sana sio tu nchini mwake China bali pia kote duniani, kutokana na fikra, mawazo na busara zake kubwa za kulifanya Taifa la China kuwa ni moja kati ya mataifa makubwa ya kiuchumi na kimaendeleo hapa duniani.

    Anasema amekuwa akivutiwa sana na mfumo wa kiuchumi wa China ambao mzee Deng Xiaoping aliuanzisha mwishoni mwa miaka ya 70 na kujulikana kama "Kuzifungulia mlango nchi za nje" ambao bila shaka yoyote umesaidia sana katika kukuza maendeleo ya kiviwanda, kisayasi na kiteknolojia na kuinua hali ya kibiashara nchini China, chini ya juhudi kubwa za wananchi wenyewe wa China.

    Bwana Msabah anasema, ikiwa tutazingatia kwa makini, tutaona kwamba sababu kuu ya kusambaratika kwa mataifa mengi ya Ulaya mashariki yaliyokuwa yakifuata siasa za kikomunisti mwishoni mwa miaka ya 80 na mwanzoni mwa miaka ya 90, kulitokana na hali mbaya za kiuchumi ambazo zilipelekea wananchi wengi wa nchi hizo kutoridhika na viongozi wao. Lakini hekima za Mzee Deng Xiaoping zilizoona mbali, kuhusu kuboresha hali za kimaisha kwa wananchi wake, kwa kutilia maanani sana swala la kupiga hatua mbele kiuchumi ndio msingi wa kulifanya taifa la kikomunisti la China kuendelea kusimama imara na hata kufikia kiwango cha kuweza kushindana na mataifa makuu ya kiuchumi duniani kama vile Marekani, Japan, na Ujerumani na hayo yalithibitika pale China ilipopokelewa kwa mikono miwili kujiunga katika jumuiya ya kiuchumi duniani WTO.

    Anasema, vilevile uongozi wa Mzee Deng Xiaoping ulisaidia sana kuyarejesha maeneo ya Hong kong na Makao katika nchi yao ya asili, kwa kubuni mfumo mpya wa kisiasa na kiuchumi uitwao "Nchi moja mifumo miwili" ambapo maeneo hayo yameweza kupata fursa ya kujiendesha wenyewe kwa mifumo tofauti na ile ya China Bara, jambo ambalo linaweza kuhesabiwa kama ni moja kati ya mafanikio makubwa ya kisiasa ya Bwana Deng Xiaoping.

    Bwana Msabah anasema, kwa kweli fikra na busara za Mzee Deng Xiaoping ambaye daima alikuwa na malengo ya kuirejesha China kuwa ni taifa moja kubwa lenye nguvu za kiuchumi, kisiasa na kimaendeleo hapa duniani ni jambo la kujivunia sana kwa wananachi wa China, kwa kupata kiongozi shupavu, jasiri, hodari na mwenye hekima kama huyo.

    Anasema kuna mengi sana ambayo Mzee Deng Xiaoping aliyaasisi kwa malengo ya kuifanya China inawiri kama maua yaliyopandwa katika bustani kubwa iliyojaa miti yenye kustawi na kutoa mandhari ya kupendeza machoni pa watu. Leo hii China imekuwa mstari wa mbele katika kuzalisha bidhaa mbalimbali ambazo zinahitajiwa na watu wote duniani.

    Bwana Mbarouk Msabah anasema mwisho angependa kutoa shukrani zake maalum kwa Radio China kimataifa kutokana na juhudi zake kubwa za kuwaelezea wasikilizaji wake mengi kuhusu siasa za kishujaa za Mzee Deng Xiaoping ambazo zimezaa matunda makubwa ya mafanikio nchini China kupitia vipindi na makala zake mbalimbali, pamoja na kuwatumia wasikilizaji wake majarida na vitabu tofauti ambavyo vinazungumzia ufanisi mkubwa wa siasa za Mzee Deng Xiaoping katika uongozi nchini China. Anasema, tunamwombea malazi mema huko aliko na daima tutamkumbuka na kumheshimu sana.

    Msikilizaji wetu Gullam Haji Karim wa Sanduku la posta 504 Lindi Tanzania ametuletea barua akisema kuwa, kila siku anaendela kusikiliza bila kukosa matangazo ya idhaa ya kiswahili ya Radio China kimataifa kuhusu vipindi vizuri na vyenye faida kwa mfano maelezo baada ya habari ambayo hutoa maelezo ya jambo muhimu kwa siku nchini China au sehemu yoyote duniani.

    Anasema siku ya jumapili 14/3/2004 katika kipindi cha sanduku la barua amesikia barua yake ikisomwa , amefurahi sana, kila baura ya msikilizaji ikisomwa anapata hamu ya kuandika barua nyingine, amepokea barua katika sanduku la barua yake ya Zanzibar, kuanzia barua hii anaomba barua na vifurushi vyote vitumie kwa anuani mpya kwa sasa. Amerudi Zanzibar kwa muda mfupi, lakini atarudi mkoa wa kusini wa Tanzania bara, Lindi na atakuwa akiishi huko kwa muda mrefu, atabaki kusikiliza matangazo na kuandika barua na kutoa maoni kuhusu vipindi na matangazo ya idhaa ya kiswahili ya Radio China kimataifa.

    Wasikilizaji wapendwa, sasa tunataka kuwaarifu kuwa, tarehe 26 Aprili itakuwa siku ya miaka 40 tangu kuanzishwa kwa uhusiano wa kibalozi kati ya China na Tanzania, kuanzia tarehe 23 hadi tarehe 29 mwezi huu tutawaletea kipindi maalum cha maadhimisho ya miaka 40 tangu kuanzishwa kwa uhusiano kati ya China na Tanzania, karibuni msikose kutusikiliza, na pia tunawakaribisha wasikililzaji wetu kutuletea makala kuhusu maadhimisho ya siku hiyo.

Idhaa ya Kiswahili 2004-04-04