Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2004-04-09 22:01:28    
Barua za wasikilizaji wetu 11/4/2004

cri

                  

    Msikilizaji wetu Abdalla Said Abdalla wa sanduku la posta 77355, Dar es Salaam, Tanzania ametuletea barua ikianza kwa salamu kwa watangazaji wa idhaa ya Kiswahili ya Radio China, akitegemea kuwa barua yake itatukuta tukiwa wazima wenye afya tele huku tukiendelea na ujenzi wa taifa, na anasema anamuomba mungu atuzidishie tuzidi kuendelea.

    Anasema anatoa shukrani zake nyingi kutokana na zawadi tuliyomtumia, anashukuru na amefurahishwa kuona jinsi gani tunavyowajali wasikilizaji wetu. Anasema pia ingawa ni mara yake ya kwanza kuomba urafiki kwetu na tulimkubali bila pingamizi na kumtumia zawadi. Anasema tena ahsanteni sana. Na cha zaidi kilichompa bashasha na hamu ya kujibu barua yetu ni kutokana na urahisi tuliompa wa kumletea bahasha na si bahasha peke yake bali ikiwa na malipo tayari ya stempu. Anasema Hongereenii!! Cha zaidi anachoomba ni kwamba angependelea tuzidishe kuwa karibu naye kwa kumtumia alau barua mara kwa mara .

    Msikilizaji wetu mwingine Kuleba Robert Kadidi wa sanduku la posta 708, Kahama Shinyaga, Tanzania anasema katika     barua yake kuwa anapenda kuwa msikilizaji wetu na pia kufuatilia mambo mbalimbali kuhusu nchi ya China. Anasema anatuambia hivyo kutokana na barua aliyoipata Agosti 2002 iliyokuwa inaeleza kuhusu kutuletea makala tano zinazohusu masuala mbalimbali ya China.

    Anasema anasikitika kuwa hakuweza kuyajibu yale maswali kumi na mbili tuliyoyauliza mwaka huo (2002) kutokana na kutokuwa na mwanga wowote kuhusu China. Lakini hivi sasa anapenda kutujulisha kuwa kuanzia hivi sasa atakuwa msikilizaji wetu mkubwa na mfuatiliaji wa karibu kuhusu mambo ya China ya leo, iwapo atatumiwa vitu hivyo alivyoomba. Hata hivyo anasema kuwa amejaribu kuyajibu maswali hayo kwa kutumia ufahamu wake. Hivyo anaomba tumjulishe ni kiasi gani amepata au amekosa. Na anatutakia kazi njema zenye mafanikio.

    Msikilizaji wetu Mbarouk Msaba wa sanduku la posta 52483, Dubai, U.A.E ametuletea barua akisema kuwa, angependa kueleza maoni yake kuhusu thamani ya kuhifadhi historia na utamaduni wa kale nchini China. Anasema China ni moja kati ya mataifa machache mno hapa ulimwenguni, ambayo yamekuwa yakichukuliwa kuwa ni yenye historia ndefu ya zaidi ya miaka 5000 iliyopita katika maendeleo na ustaarabu wa binadamu.

    Hata hivyo lakini, yote hayo yamekuwa yakitegemea sana juhudi kubwa kabisa zinazochukuliwa na serikali ya Jamhuri ya watu wa China, katika kuhifadhi kwa makini na uangalifu mkubwa wa maeneo yote ya China, ambayo ina ukubwa wa zaidi ya kilomita milioni 9 na laki 6 za mraba na kuifanya China iwe ni nchi ya tatu kwa ukubwa duniani na ya kwanza yenye idadi kubwa ya watu hapa duniani.

    Anasema, sehemu kuu za kihistoria kama vile "Ukuta Mkuu", "Kasri la Kifalme" mjini Beijing, "Kasri la Budara" mjini Lahsa mkoani Tibet, na "Pango la Mogao" mkoani Gansu ni baadhi ya mifano michache tu ya maeneo ya kihistoria yaliyohifadhiwa vyema nchini China. Maeneo ya kimaumbile yenye mandhari nzuri za kuvutia kama vile "mabonde ya mto Li-Jiang" kusini mashariki mwa China, "Ziwa Qinghai" mkoani Qinghai, "Eneo la Mongolia ya ndani" kaskazini magharibi mwa China ni moja kati ya vivutio vikubwa vya kimaumbile vinavyoweza kupatikana nchini China vikiwa katika hali yake ya kiasili.

    Anasema nayo "mabaki ya sanamu za askari na farasi wa mfalme Qin Shihuang" ambazo zinaaminika kuwa na umri wa miaka 2300 zimekuwa ni moja wapo ya vitu vya kustaajabisha sana mbele ya macho ya watu wa kawaida, wasomi, viongozi wakuu wa nchi na hata wafalme na watawala mbalimbali kote ulimwenguni, ambao wamekuwa na shauku kubwa ya kujionea kwa macho yao urithi huo wa ajabu na wenye kuvutia sana ulioachwa na Wachina wa enzi mbali mbali na tawala tofauti.

    Bwana Msabaha anasema, vile vile kuendelea kwa maisha ya kitamaduni miongoni mwa makabila 56 ya kichina katika mikoa na majimbo mbali mbali nchini China, kumesaidia sana kuhifadhi thamani halisi ya mila, desturi na tamaduni za kijadi za kichina, jambo ambalo limekuwa likitoa mandhari halisi ya mifumo ya kimaisha iliyokuwepo nchini humo, tangu enzi za zamani.

    Bwana Msabah anasema mwisho angependa kutoa shukrani zake za dhati kwa Radio China Kimataifa kwa kuandaa makala maalumu zilizohusu vivutio vya utalii na kihistoria magharibi mwa China hapo mwaka jana, kama ni shindano la "Chemsha Bongo" kwa wasikilizaji wake, kwa vile makala hizo ziliwasaidia sana kuongeza ujuzi kuhusu kutambua thamani kubwa ya kihistoria na kimaumbile nchini China, kwani yeyote atakaye kusikiliza au kuzisoma makala hizo, basi hatasita kupata msisimko mkubwa uliojaa mvuto wa kuipenda nchi ya China.

    Bwana Mbarouk Msabah anasema, ni matarajio yake makubwa kwamba Radio China Kimataifa itaendelea kuwaandalia wasikilizaji wake vipindi na makala mbalimbali zitakazoweza kuwaelimisha mengi kuhusu China, kama vile ilivyofanya kwa mwaka uliopita.

    Tunamshukuru kwa dhati Bwana Mbarouk Msabah ambaye kila mara anatuandikia barua za kututia moyo kuendelea na juhudi za kufanya vizuri vipindi vyetu.

    Na msikilizaji wetu Kilulu Kulwa wa sanduku la posta 161, Bariadi, Shinyanga, Tanzania anasema katika barua yake kwamba, yeye msikilizaji wetu hajambo kabisa anaendelea na shughuli za ujenzi wa taifa la Tanzania, na bila kusahau kusikiliza vipindi na matangazo ya Idhaa ya kiswahili ya Radio China Kimataifa ambayo husikika pia kupitia Shirika la Utangazaji la Kenya maarufu KBC. Wanashukuru sana kwa ushirikiano huo kati ya CRI na KBC.

    Anasema pia wanafurahi kwamba hivi sasa matangazo yetu yanaweza kupatikana kupitia tovuti ya www.cri.com.cn ambapo katika tovuti hiyo mtu akichagua Kiswahili anafaidika kwa kusoma vipindi vya Idhaa ya Kiswahili ya Radio China Kimataifa kwa njia ya tovuti ya idhaa ya kiswahili. Hayo ni mafanikio makubwa kabisa ya upashanaji habari duniani katika ulimwengu na enzi hii ya maendeleo ya sayansi na teknolojia. Anasema yeye binafsi akiwa msikilizaji wetu wa miaka mingi atazidi kuiunga mkono kwa ukamilifu Radio China Kimataifa, ikiwa ni pamoja na kutoa maoni na ushauri mbalimbali kama itakavyokuwa inafaa.

    Bwana Kulwa anasema, anapenda kutumia nafasi hii kuwashukuru wahariri na watangazaji wote wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI kwa juhudi zao nyingi wanazofanya bila kuchoka ili kuwahudumia wasikilizaji wa idhaa ya kiswahili ya Radio China kimataifa popote walipo Afrika mashariki, Afrika ya kati na kusini hata nje ya bara la Afrika.

    Bwana Kulwa anasema, jambo lililomvutia zaidi katika mwaka uliopita wa 2003 ni pamoja na matembezi yaliyofanywa na mtangazaji wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI Mama Chen na Bwana Du Jiman huko Kisii na Nairobi nchini Kenya, ambapo walifanya semina na wasikilizaji wa CRI nchini Kenya, kwa kweli tukio hilo ni kubwa na lina maana sana hasa katika suala la kujenga mahusiano kati ya watumishi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI na wasikilizaji wake.

    Anasema, walivutiwa sana na matangazo ya Radio ambayo yalielezea kwa ndani na kwa kina zaidi kuhusu safari hiyo ya watumishi wa CRI waliyoifanya kati kati ya mwezi August mwaka uliopita wa 2003. Ni matumaini yake kwamba katika siku za usoni tutaweza kufanya hivyo katika nchi na eneo lingine ili kukutana na wasikilizaji wengi, kuongea nao na kutoa semina kuhusu vipindi na matangazo ana kwa ana wasikilizaji.

    Katika barua yake anasema anapenda kuwashukuru sana watayarishaji wa kipindi cha Sanduku la Barua na hasa Jumapili ya tarehe 8 na tarehe 15 mwezi February mwaka huu wa 2004 ambapo Dada Chen na Ndugu Fadhili Mpunji walinukuu barua zake. Pia anatoa shukurani kwa kupokea barua kadhaa za mfululizo kutoka kwenu ikiwa ni pamoja na zawadi ya picha ya mnyama aina ya kima iliyokatwa na mabingwa wa sanaa wa kichina.

    Anasema hicho ni kielelezo cha urafiki mkubwa tulio nao kati ya wasikilizaji wa Radio China Kimataifa na wafanyakazi wa CRI, hivyo anashukuru sana.

    Msikilizaji wetu Mbarouk Msabah wa sanduku la posta 52483, Dubai, U.A.E ametuletea barua pamoja na picha yake moja akieleza kuwa, "Mfalme kima ni hadhithi ya kuvutia ya kichina"

    Ikiwa mwaka huu wa 2004 ni mwaka wa alama ya mnyama "kima" kwa mujibu wa kalenda ya kijadi ya kichina, kwa kweli kima amekuwa ni mmoja katika wanyama wenye umaarufu mkubwa nchini China.

    Simulizi za hadithi mbalimbali za kikale nchini China, zimekuwa zikielezea mengi kuhusu taswira ya kumtumia kima katika simulizi zake, hata opera maarufu za kichina kama vile "opera ya kibeijing" ambayo ndio opera ya kitaifa ya China, imekuwa ikitumia hadithi kuhusu kima katika uigizaji wake, kama vile hadithi maarufu ya "Mfalme Kima" iliyoandikwa na mwandishi mashuhuri wa kichina katika enzi ya utawala wa Ming Bw. Wu Cheng'en.

    Nilivutiwa zaidi na simulizi za "Mfalme Kima" pale nilipokutana uso kwa uso na mwigizaji wa ngoma za kitamaduni za kichina katika banda la kibiashara la China, kwenye maonesho ya kibiashara ya kila mwaka hapa mjini Dubai yenye kuwashirikisha washiriki kutoka mataifa mbali mbali ya dunia, yaliyoanza tarehe 15 Januari na kumalizika tarehe 15 Februari mwaka huu wa 2004.

    "Samahani Bwana, naomba kupiga picha ya ukumbusho na wewe!" hivyo ndivyo nilivyoanza kumwomba mwigizaji mmoja wa kichina aliyejichora usoni mwake mithili ya sura ya kima kwa rangi nyekundu na nyeupe pamoja na michoro midogo midogo miembamba pembeni yake, huku akiwa amevaa nguo ndefu mpaka chini yenye rangi ya dhahabu na iliyojaa nakshi za kupendeza. "Oh!" muigizaji huyo alishusha pumzi na kucheka, na baadaye kuniambia "Bila ya taabu rafiki yangu", hapo ndipo nilipopata bahati hiyo ya kupiga picha na mwigizaji huyo wa kichina wa hadithi ya "Mfalme Kima" ambaye pamoja na waigizaji wengine, alikuwa akionesha ustadi wake jukwaani mbele ya mamia na maelfu ya watu waliojazana kila siku katika banda la kibiashara la China kwa kipindi chote cha mwezi mzima wa maonesho hayo ya kila mwaka ya kibiashara mjini Dubai.

    Ni wazi kabisa alama ya "Mfalme Kima" ni mojawapo ya alama zinazogombea kuchaguliwa kuwa "nembo" rasmi itakayowakilisha mashindano ya michezo ya Olimpiki ya mwaka 2008 nchini China, hivyo naitakia kila la kheri na mafanikio alama hiyo, ili hatimaye kamati ya China ya kuchagua nembo itakayotumika katika michezo hiyo, itafikia uamuzi wa kuiteua alama ya "Mfalme Kima", kwani kwa kweli itawavutia watu wengi kote duniani, mimi nikiwa mmoja wapo.

    Bwana Mbarouk Msabah ametuelezea hadithi nzuri ya kufurahisha, tuliposoma barua yake na kutazama picha aliyotuletea, tulifurahi sana, na picha yake hiyo ya kupendeza tutaiweka kwenye tovuti yetu, ili kuwafurahisha wasikilizaji wengine wote. Tunamshukuru kweli Bwana Msabah kwa maelezo yake mazuri.

    Katika barua yake nyingine Bwana Mbarouk Msabah pia anasema kuwa, angependa kutoa pongezi zake za dhati kwa uongozi wa Radio China Kimataifa kwa Idhaa hii ya Kiswahili kutokana na kuanzisha kwa tovuti yake hapo mwishoni mwa mwaka jana.

    Anasema, kwa kweli anashindwa hata kuielezea furaha yake kuhusu jambo hilo, kwani baada ya kuitembelea tovuti hiyo katika mtandao wa Internet alivutiwa nayo sana licha ya kwamba alikuwa akiyapata matangazo yetu hapo kabla kwa kutumia tovuti ya CRI on line Radio 4U.

    Anasema, njia hiyo ya kuanzisha tovuti maalumu kwa ajili ya Idhaa ya Kiswahili itawasaidia sana wasikilizaji wetu wanaoishi nje ya eneo la Afrika Mashariki na Kati kuweza kuyasikiliza matangazo yetu katika hali ya usikivu mzuri na wakati mwafaka kutokana na shughuli zao za kikazi, kwani hata akiwa kazini hutembelea tovuti yetu na kusikiliza vipindi vyetu pamoja na kusoma makala mbalimbali ambazo zinakuwepo ndani ya tovuti hiyo.

    Kwa njia hiyo, bila shaka yoyote Radio China Kimataifa itazidi kupata umashuhuri na kuweza kuwafikia wasikilizaji wengi zaidi kila pembe ya dunia ambako wazungumzaji wa lugha ya Kiswahili wanapatikana. Yeye akiwa miongoni mwa wasikilizaji wetu kwa zaidi ya miaka 16 sasa angependa kutoa shukrani zake nyingi kwetu kutokana na juhudi zetu za kukuza urafiki, maelewano na udugu kati ya China na Mataifa mengine, kwani Radio China Kimataifa daima imekuwa ni daraja linalowaunganisha Wachina na Walimwengu kwa misingi ya kuleta uwelewano kwa watu tofauti.

    Mwisho angependa kuwasilimia Dada Chen, Bw. Fadhili Mpunji pamoja na watangazaji wote wa Radio China Kimataifa. Na sisi tunamshukuru sana kutembelea tovuti yetu kwenye mtandao wa internet. Na kutokana na nguvu kazi ambazo bado hazijatosha katika idhaa yetu, bila shaka bado kuna dosari kadhaa katika tovuti yetu, hata kuna makosa fulanifulani katika tafsiri zetu, ni matumaini yetu kuwa Bwana Mbarouk Msabah na wasikilizaji wetu wengine watatoa maoni na mapendekezo ya kutusaidia kufanya vizuri zaidi tovuti yetu ili kuwavutia zaidi wasikilizaji.

    Tunapenda kuwakumbusha tena wasikilizaji wetu kuwa, tarehe 26 Aprili itakuwa siku ya maadhimisho ya miaka 40 tangu kuanzishwa kwa uhusiano wa kibalozi kati ya China na Tanzania, kuanzia tarehe 23 hadi 29 mwezi huu tutawaletea wasikilizaji wetu kipindi maalum cha maadhimisho ya miaka 40 tangu kuanzishwa kwa uhusiano wa kibalozi kati ya China na Tanzania. Msikose kutusikiliza.

    Hadi hapo ndio kwa leo ndio tumekamilisha kipindi hiki cha sanduku la barua ni watangazaji wenu Chen na Fadhili Mpunji tunawaaga hadi jumapili ijayo wakati kama huu kwaherini.

Idhaa ya Kiswahili 2004-04-11