Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2004-04-13 15:40:18    
Bw. Xi Shu na Duka Lake la Vitabu

cri
Bw. Xi Shu, ana umri wa miaka 41, hapo mwanzo alikuwa ni mwalimu na alijulikana kwa sanaa zake za kuandika maneno ya Kichina. Mwaka 1985 hakuridhika na kazi yake ya ualimu katika shule ya sekondari, aliacha kazi hiyo na kuja Beijing. kwa kutegemea sanaa yake ya kuandika maneno ya Kichina alifanya maonesho ya sanaa yake kwa kushirikiana na marafiki zake. Kutokana na msaada wa watu wengine maonesho yake yalifanikiwa vizuri. Vyombo vingi vya habari vilitangaza habari kuhusu maonesho hayo, na yeye mwenyewe akiwa na umri wa miaka 22 wakati huo akawa maarufu. Tokea hapo alianzisha shule ya sanaa ya kuandika maneno ya Kichina kuwafundisha wapenda sanaa hiyo.

     Mwaka 1995 Bw. Xi Shu alianza kushughulika na kufungua duka la vitabu kwa kutumia pesa alizopata kutokana na kufundisha sanaa ya kuandika, na kuanzisha duka lale la kwanza mjini Beijing. Wakati huo maduka binafsi ya vitabu yalikuwa mengi, ushindani kati ya maduka ya vitabu ulikuwa mkali. Kuhusu sababu ya kuanzisha duka la vitabu, Bw. Xi Shu alieleza, "Sababu ya kufungua duka la vitabu, kwanza ni kuwa mimi naipenda shughuli hiyo. Tokea utotoni mwangu nilipenda kusoma vitabu, na kuanzia mwaka 1984 nilishikwa na hamu ya kufungua duka la vitabu. Sababu ya pili ni kuwa mwaka 1995 na 1996 niligundua kwamba shughuli za soko la vitabu hazikuwa zimestawi, hii ilikuwa na maana kuwa shughuli hizo zilikuwa na nafasi kubwa za kuendelea

    Mwaka 1997 Bw. Xi Shu alianza kutayarisha kufungua maduka mengine ya vitabu na kufikia mwishoni mwaka huo alikuwa na maduka zaidi ya 100 nchini China. Mwaka 2000 aliunganisha mauzo ya vitabu pamoja na internet, na kupitia internet aliuza na kutoa uhakiki kuhusu vitabu fulani vizuri. Hivi sasa amekuwa na maduka 620 ambayo yametapakaa katika sehemu mbalimbali nchini China, na Bwana huyo amekuwa "mtu wa kwanza kufanya shughuli binafsi za mauzo ya vitabu". Bw. Xi alisema, "Mimi ni mtu mwenye matumaini na ukaidi. Ninaposema mwenye matumaini nina maana matumaini yangu ndio nguvu za kunisukuma, nasema ukaidi nikiwa na maana kuwa hata matatizo yakiwa makubwa kiasi gani, mimi siku zote sikubali kushindwa. Lakini matumaini pia ni mtazamo sahihi, juhudi fulani ukitaka kuzifanikisha lazima uwe na mtazamo sahihi kuhusu mustakbali wa juhudi zako, kwa hiyo natilia maanani kuchunguza hali ya jamii takayokuwa hapo baadaye na kutafuta nafasi ya kuanzisha juhudi zangu. Naona sijafanikiwa sana lakini sikufanya makosa ya mwelekeo wa kuelekeza juhudi zangu katika miaka mingi iliyopita."

    Baada ya kufungua duka la vitabu, alianzisha jarida la "Vitabu Vizuri"na klabu ya wasomaji. Ili kuwashirikisha wanachama wa klabu yake, aliwaalika wasomi zaidi ya 100 kufafanua vitabu na kutoa mapendekezo ya vitabu vizuri.

    Bw. Xi Shu amekuwa bosi kutoka mwalimu wa shule ya sekondari, lakini anaona kuwa mabadiliko hayo yanatokana na matumaini yake ya maendeleo ya utamaduni. Yeye hapendi watu wamwite bosi, anaona kwamba yeye ameunganisha matumaini yake pamoja na upendo wake, na anaona kusoma vitabu ni sehemu yake muhimu katika maisha yake. Alisema, "Kusoma vitabu ni desturi katika maisha yangu, naona furaha kusoma na naridhika na maisha yangu kwa kusoma. Nisiposoma vitabu naona kichwa changu ni kitupu na maisha yanapoteza ladha. Zaidi ya hayo, mtu hawezi kupata maendeleo bila kusoma, hasa katika zama hizi ambapo jamii inabadilika haraka, mtu lazima awe na fikra mpya, dhana mpya na elimu mpya, la sivyo hatafanikiwa chochote."

    Bw. Xi Shu alisema, hajaridhika na hali yake ya sasa, matumaini yake ni mengi yakiwa ni pamoja na kujiunga na shughuli za upashanaji habari na nyanja ya michezo ya televisheni na filamu. Kwani anaona kuwa hivi sasa mazingira ya kuendeleza utamaduni nchini China ni mazuri sana.

Idhaa ya kiswahili 2004-04-13