Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2004-04-15 17:31:10    
Soko la ajira nchini China kwa wahitimu wa vyuo vikuu

cri

Wahitimu wa vyuo vikuu vya China wanashiriki kwenye shughuli za kutafuta nafasi za ajira. 

    Tokea mwishoni mwa miaka ya 80 ya karne iliyopita, serikali ya China ilifuta hatua kwa hatua sera ya kuwapa ajira wahitimu wa vyuo vikuu. Na katika muda huu, vyuo vikuu vya China viliongeza kuwaandikisha wanafunzi, na idadi ya wahitimu wa vyuo vikuu pia iliongezeka haraka. Kadiri ushindani katika soko la ajira unavyozidi kuwa mkali miongoni mwa wahitimu wa vyuo vikuu, mawazo yao kuhusu mambo ya ajira yanavyobadilika, na mawazo ya kujitafutia ajira yameimarika.

    "Mimi naitwa Li Chengyao. Nasoma lugha ya Kipoland katika Chuo kikuu cha lugha za kigeni cha Beijing. Nimechagua taaluma hiyo kwa sababu navutiwa na lugha na fasihi za Poland. Mbali na lugha hiyo yenyewe, pia najifunza ujuzi mwingine, kwa vile si rahisi kupata ajira zinazohusiana na lugha ya Kipoland."

    Hayo ni maelezo ya Bw. Li Chengyao akitumia lugha ya Kipoland kwa kujitambulisha. Hadi ifikapo mwezi Julai, mwaka huu, kijana huyo atamaliza masomo yake ya taaluma ya lugha na fasihi za Poland katika Chuo kikuu cha lugha za kigeni cha Beijing. Miongoni mwa idadi kubwa ya wahitimu wa vyuo vikuu, yeye na wenzake wanaonekana ni maalumu, kwa vile somo lao si somo linalopendwa na watu wengi kwa hivi sasa nchini China. Kwa hivyo, zipo nafasi chache za ajira zinazowafaa katika soko la ajira, kwa kuwa, hivi sasa hakuna viwanda au makampuni ambayo yanahitaji watu wanaofahamu lugha ya Kipoland. Kuhusu suala la ajira, kijana huyo alieleza wasiwasi wake, akisema,

    "Sisi tunajifunza lugha ambayo inatumika na watu wachache. Kutokana na ufinyu wa matumizi ya lugha hiyo, viwanda na makampuni mengi hayatufai, hali ambayo inatupa shida kubwa wakati wa kutafuta ajira. Nilishiriki kwenye usaili na shughuli kadhaa za kutafuta nafasi za ajira, ambapo niliwasilisha utambulisho wangu kwa viwanda na makampuni kadhaa, lakini mpaka hivi sasa, sijapata jibu lolote."

    Wasiwasi wa Bw. Li Chengyao umeonesha hali halisi ya soko la ajira la China kwa hivi sasa kwamba, kwa kuwa uchumi wa China upo katika kipindi cha kujiendeleza haraka, soko la ajira linahitaji sana watu wenye ujuzi kuhusu usimamizi wa kiuchumi, mauzo, teknolojia za kompyuta na lugha zinazotumika sana kama vile lugha ya Kiingereza. Kwa hiyo, wahitimu wa masomo hayo wanapata fursa nyingi zaidi za kuchagua ajira, lakini kwa Bw. Li Chengyao na wenzake wanaojifunza lugha za kigeni zinazotumika na watu wasio wengi bado hawana nafasi kubwa kwa hivi sasa.

    Hata hivyo, alipoulizwa na mwandishi wetu wa habari kuwa, kama anatarajia serikali itarudisha sera ya kuwapa ajira wahitimu wa vyuo vikuu? Kijana huyo alitoa jibu la hapana.

    "Kwa maoni yangu hakuna haja ya kufanya hivyo. Kwa vile, sasa tumeingia katika uchumi wa soko huria, ambapo ushindani unaonekana popote nchini. Kwa hiyo, tunatafuta nafasi za ajira tunazopenda kwa kutegemea uwezo wetu wenyewe, hili ni jambo lenye manufaa."

    Bw. Li Chengyao alisema kuwa, kupata ujuzi maalumu kuhusu somo moja ni vizuri kwa mtu mmoja kujiendeleza katika siku zijazo. Alieleza imani yake kuwa, kadiri China inavyozidi kufungua mlango wake, watu wanaofahamu lugha za kigeni, mfano wa lugha ya Kipoland watapata fursa ya kutumia ujuzi wao. Na kwa maoni yake, kubadilika kwa sera ya ajira kwa wahitimu wa vyuo vikuu vya China, si kama tu kumewapa shinikizo, bali pia kumewahimiza wajifunze ujuzi mwingine mbali na masomo yao, kwa hiyo wanaweza kuwa na uwezo mkubwa zaidi.

    Majibu ya namna hii yanawakilisha mawazo ya wahitimu wengi wa vyuo vikuu hapa nchini China. Kwa upande mmoja, wanakabiliana na hali ngumu ya upatikanaji wa ajira, na kwa upande mwingine, katika hali hii, wanabadilika kuwa na mawazo imara ya kujitegemea, na kuonesha thamani yao kwa uwezo na jitihada kubwa.

    Hivi sasa, katika miji mikubwa ya China, mfano wa Beijing, Shanghai na Guangzhou, kuna wahitimu wa vyuo vikuu waliotoka mikoa na miji mingine. Watu hao wanaitwa "wahangaikaji", na maisha yao yanawakilisha wahitimu wengi wa vyuo vikuu. Wamepewa jina hilo "wahangaikaji" kutokana na hali ya maisha yao kwamba, wanahitimu kutoka kwa vyuo vikuu visivyo maarufu, wanatoka familia ya kawaida na hawana jamaa katika miji hiyo mikubwa wanaoweza kuwategemea. Baada ya kuingia katika miji ambayo ni migeni kabisa kwao, mwanzoni maisha yao yakawa ni magumu, baadhi yao wanakuwa hawana hata makazi ya kudumu. Katika miji mikubwa, pia wanakabiliwa na kodi kubwa ya nyumba na gharama za juu za maisha ya kila siku, kwa hiyo, kwa kawaida watu kadhaa wanapangisha nyumba moja. Kwa nini wamechagua maisha ya namna hii? Kwa sababu wanathamini zaidi nafasi nyingi za ajira na fursa za kujiendeleza zinazotolewa na miji mikubwa. Kwa maoni yao, kiasi cha mapato katika muda mfupi si muhimu sana, na hatua ya serikali kufuta sera ya kuwapa ajira wahitimu wa vyuo vikuu inawapa fursa nyingi zaidi za kujiamulia kuchagua ajira, hatua hiyo pia imefanya wawe na upeo wa mbali zaidi na kujiamini zaidi.

    Bibi Wanglin ni mmoja wa waliopo katika kundi hilo la "wahangaikaji". Msichana huyo alihitimu kutoka kwa Chuo kikuu cha radio na televisheni cha Shenyang, kilichopo sehemu ya kaskazini mashariki ya China. Hali ya uchumi wa familia yake si mbaya. Aliposoma katika chuo kikuu, alikuwa anafanya kazi yenye malipo mazuri baada ya masomo. Baada ya kuhitimu kwake, kutokana na masomo na uzoefu wake wa ajira, ilikuwa si vigumu kwake kutafuta nafasi ya ajira yenye malipo mazuri katika maskani yake. Lakini alikuja Beijing, mji mkuu wa China. Hivi sasa, yeye na wenzake watatu wanaotoka maskani kwao wanaishi katika nyumba moja ndogo ya kukodishwa yenye mita 40 za mraba. Katika miezi kadhaa iliyopita, alishiriki katika shughuli za kutafuta nafasi za ajira kwa zaidi ya mara 10, pia amefanya usaili katika viwanda vipatavyo 10, lakini bado hajapata nafasi ya ajira inayomfaa. Pamoja na hayo, Bibi Wang Lin ana imani kubwa kwa mustakabali wake. Alieleza kuwa, anapochagua ajira, anazingatia maendeleo ya sekta iliyopo nafasi ya ajira katika siku zijazo.

    Alisema, "Naona si lazima uwe umehitimu kutoka kwenye vyuo vikuu maarufu au wewe ni wenyeji ndio uweze kupata nafasi nzuri ya ajira. Bali cha muhimu zaidi ni uwezo wenyewe. Sasa nina uhuru mkubwa wa kuchagua nafasi ya ajira na katika mji huu mkubwa pia kuna fursa nyingi. Kuna mambo mengi ambayo huwezi kujifunza katika chuo kikuu. Lakini iwapo unachapa kazi, hakika thamani yako itatambuliwa na wengine. Kwa nafasi yangu ya kwanza ya ajira, nazingatia zaidi nini nitaweza kujifunza kutokana na kazi hiyo na uzoefu gani nitaweza kukusanya kutokana na kazi hiyo. Kwa hivyo, napendelea kazi yenye mustakabali mzuri, sijali malipo duni ya hivi sasa au ugumu wa kazi hiyo."

    Tofauti na Bw. Li Chengyao na Bibi Wang Lin, Bibi Deng Hua alihitimu kutoka kwa chuo kikuu maarufu cha Fudan cha Shanghai, ambapo alichukua kozi ya usimamizi wa mambo ya kifedha. Hivi sasa, anafanya kazi katika kampuni ya uhasibu ya Ernst&Young, ambayo ni moja kati ya makampuni manne makubwa ya uhasibu ulimwenguni. Msichana huyo ni mmojawapo kati ya wanafunzi waliohitimu kutoka kwa vyuo vikuu maarufu nchini China, na mabadiliko ya sera ya ajira yanawanufaisha zaidi. Kwa vile, wana sifa kubwa katika masomo yao, hivyo wana uhuru zaidi katika kuchagua mazingira ya kazi na mishahara inayotolewa na makampuni na viwanda tofauti. Bibi Deng Hua alisema,

    "Iwapo serikali inaendelea na sera ya kuwapa ajira wahitimu wa vyuo vikuu, hakika matokeo yake yatakuwa si mazuri tofauti na ilivyo hivi sasa. Sera ya hivi sasa ni ya ushindani wenye usawa, ambayo inatoa fursa kwa watu wenye uwezo wa kujitafutia nafasi nzuri za kazi, na inaweza kutuhimiza tujifunze mambo mengi bila kusita. Wahitimu wa vyuo vikuu na upande wa waajiri wote wanaweza kufanya chaguo, jambo ambalo linazipa pande hizi mbili changamoto, hiki ni kitu muhimu na cha lazima kwa vijana, na pia kinachangia uhai wa jamii. Hii ni aina ya changamoto, pia ni shinikizo ama kwa viwanda na makampuni, ama kwa jamii, au kwa sisi vijana, ambayo inatusukuma mbele bila kusimama."

    Bibi Deng Hua pia alimwambia mwandishi wa habari kuwa, kutokana na ushindani wa hivi sasa, hata watu wenye uwezo mkubwa hawawezi kufanya uzembe hata kidogo. Kwa kuwa, unapofanya kazi, unakutana na washindani wengine mara kwa mara ambao ni hodari katika mambo tofauti. Na huwezi kwenda sambamba na mahitaji ya kazi bila kujifunza siku hadi siku.

Idhaa ya Kiswahili 2004-04-15