Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2004-04-15 17:31:04    
Ujumbe wa viselula, njia mpya ya mawasiliano

cri
    Bw. Wu Qinggang ni kijana mwenye umri wa miaka 25, na ni mhandisi wa kampuni moja ya teknolojia ya hali ya juu hapa jijini Beijing. Siku moja miezi sita iliyopita, majira ya saa 2 usiku, alikuwa anasoma tovuti mbalimbali kwenye Internet. Katika tovuti moja iliyotangaza habari za kutafuta marafiki, Bw. Wu alivutiwa na jina moja lililosajiliwa kama "mwezi wa kale" pamoja na nambari ya simu yake ya mikononi. Wakati huo huo, kijana huyo alikuwa na wazo moja, kwamba anaweza kumsalimia kwa kumpelekea ujumbe kupitia simu ya mikononi. Muda si mrefu baadaye, Bw. Wu alipata majibu kutoka kwa rafiki huyo asiyemfahamu hata kidogo. Akiwa ndani ya basi kuelekea nyumbani, walianza mazungumzo kupitia ujumbe wa viselula, ambapo Bw. Wu aliona kuwa, safari ya saa moja kuelekea nyumbani ilionekana imefupishwa, na alihisi kuburudika kwa kiasi baada ya kazi ya siku nzima.

    Hadhithi hiyo haikuishia hapo tu, bali Bw. Wu na rafiki huyo anayejiita "mwezi wa kale" wakawa mume na mke baada ya miezi sita.

 

    Bw. Wu ananiambia kuwa, kuanzia siku hiyo, walikuwa wanawasiliana mara kwa mara kupitia ujumbe wa viselula, kiasi kwamba mazungumzo hayo maalumu yaliendelea hadi usiku wa manane baadhi ya wakati. Anasema, "Tulikuwa tunavutiana katika mazungumzo, ingawa haikupita muda mrefu, lakini tuliona kuwa tumekuwa karibu sana. Katika kipindi hiki, nilikuwa natuma ujumbe zaidi ya 100 kwa wastani wa kila siku."

    Kwa kupitia ujumbe wa viselula, Bw. Wu alifahamisha kwamba, mtu huyo anayejiita "mwezi wa kale" ni msichana, na jina lake la kweli ni Qin Yue. Anaishi katika mji wa Taiyuan, umbali wa kilomita 500 kutoka Beijing, anapokaa Bw. Wu. Wiki mbili baadaye, walikutana katika kituo cha treni cha mji wa Taiyuan, ambapo walipendana papo hapo.

    Kwa vile wanaishi katika miji tofauti, wanashindwa kukutana kila siku, gharama ya simu ya masafa marefu ni kubwa, hivyo ujumbe wa viselula ukawa njia mwafaka ya mawasiliano kwa wapenzi hao, kutokana na sifa zake za kutuma na kupokea mara moja pamoja na gharama nafuu. Bw. Wu anakumbusha kuwa, alikuwa anakwenda msalani akiwa na kiselula chake.

    Qin Yue ni msichana mwangalifu sana. Alinakili ujumbe wao mmoja baada ya mwingine kwenye daftari, na katika kipindi cha nusu mwaka, amekuwa na daftari tatu kubwa. Anaeleza kuwa, katika siku zile, popote alikwenda alikuwa na kiselula, daftari na karamu. Anasema kuwa, hizo ni hazina zake za mapenzi.

    "Kiselula kina ukubwa wa kiasi wa kuhifadhi ujumbe, iwapo ukubwa huo umejaa, unapaswa kufuta baadhi kwa ajili ya kupokea mwingine. Naona kila ujumbe anaotuma ni mzuri na kuthaminika. Mapenzi yanatutia moyo, ambapo baadhi ya maneno hatuwezi kuyapata kimawazo katika hali ya kawaida, lakini tunaweza kuongea kupitia ujumbe wa viselula."

    Vijana hao wawili wamefunga ndoa kutokana na ujumbe wa viselula, ingawa matukio ya namna hii ni machache sana, lakini katika China ya hivi leo, ujumbe wa viselula hutumika sana na watu katika kuwasiliana na kusalimiana. Mathalan, katika sikukuu ya Spring, ambayo ni mwaka mpya wa kalenda ya Kichina, idadi ya ujumbe iliwahi kufikia milioni 100 kwa siku. Takwimu zinaonesha kuwa, mwaka 2002, jumla ya ujumbe wa viselula ilikuwa bilioni 90, na idadi hiyo ilizidi bilioni 150 mwaka 2003. Tunaweza kusema kuwa, takriban kila mteja wa kiselula wa China amepeleka au kupokea ujumbe.

    Hali hii imetokana na hali ya viselula kupatikana nchini kote. Tukitembea mijini hapa nchini China, tunashuhudia watu wengi wenye viselula, kiasi kwamba baadhi ya watu wanaofuatilia mitindo wamebadilisha viselula vyao mara kadhaa. Ujumbe ukiwa aina moja ya huduma za viselula sasa umegeuka kuwa njia ya mawasiliano inayopendwa na watu wengi.

    Katika hali hii, makampuni ya simu ya China yametoa huduma mbalimbali za ujumbe. Aina moja ya huduma inayojulikana kama "M-Zone" ilitolewa mwaka jana nchini China, ambapo mteja hulipa Renminbi Yuan 20 tu kwa mwezi, sawa na dola 2 za kimarekani, anaweza kupeleka ujumbe 300. Hivyo, kwa wastani kila ujumbe hugharamia centi 7 tu, lakini hapo awali, gharama yake ilikuwa centi 10 au 15.

    Bw. Gao Ran ni miongoni mwa wapenzi wa huduma hiyo, anatoa maoni yake, akisema, "Sasa natumia kadi ya 'M-Zone', naweza kupeleka ujumbe wakati wowote. Nikipata hadithi, vichekesho na habari mpya, nawatumia marafiki na jamaa zangu kwa wakati. Kwa mfano, wanafunzi wenzangu wanakaa katika sehemu tofauti hapa nchini. Nikiwapigia simu, ni gharama kubwa. Kuwapelekea ujumbe wa viselula, kunagharimia centi 7 tu, lakini naweza kuwasalimia. Licha ya umbali kati yetu, naweza kuwapata. Ujumbe wa viselula unafanya kazi kubwa zaidi kuliko njia nyingine za mawasiliano."

    Ujumbe wa viselula pia umetoa nafasi ya mawasiliano kati ya watu wasiofahamiana. Bibi Wang Fang ni mwandishi wa habari, alieleza mafanikio yake alipoweza kumhoji mwimbaji maarufu kwa kupitia ujumbe wa viselula. Baada ya kupata nambari ya simu ya kiselula ya mwimbaji huyo, Bibi Wang alimpelekea ujumbe. "Niliona siwezi kumpigia simu mara moja, sitaki kumsumbua, pia hatapokea simu yangu kwa vile hatambui nambari yangu. Kwa hivyo, nilimpelekea ujumbe kupitia viselula. Katika ujumbe huo, nilijitambulisha, na kumwelezea programmu yangu na maswali ninayotaka kumhoji, pamoja na namna ya kunipata. Baada ya saa mbili, alinipigia simu, na kusema amekubali mahojiano."

    Hivi sasa, ujumbe wa viselula umekuwa njia rahisi ya mawasiliano kati ya Wachina. Mbali na hayo, umeingia katika maeneo mbalimbali ya maisha. Katika siku za baadaye, labda tutaweza kuutumia katika kununua tikiti za filamu na maua, kulipia ada za simu, maji na umeme. Katika enzi hii ambapo sayansi na teknolojia huendelezwa kila wakati, je, kuna kitu kisichowezekana?

Idhaa ya Kiswahili 2004-04-12