Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2004-04-18 19:44:48    
Shenyang inajitahidi kutoa nafasi nyingi za ajira

cri
    Mji wa Shenyang ulioko sehemu ya kaskazini mashariki ya China, ni kituo cha zamani cha viwanda nchini China. Katika miaka hiyo miwili, mji huo ulitoa ajira karibu kwa wafanyakazi wote waliopunguzwa kutoka viwanda vya serikali kwa njia ya kuongeza nafasi za ajira, kuwahamasisha watu kujiajiri, kutoa mafunzo ya kazi na sera zenye nafuu. Hivi sasa uzoefu wao umekuwa mfano wa kuigwa kwa sehemu nyingine nchini katika utatuzi wa suala la ukosefu ajira kwa wafanyakazi waliopunguzwa kutoka kwenye viwanda vya serikali.

    Shenyang ni mji mkuu wa mkoa wa Liaoning ulioko sehemu ya kaskazini mashariki ya China. Mji huo una viwanda vikubwa na wastani makumi kadhaa vya zamani, na ulijulikana sana nchini China kwa wingi wa viwanda vya serikali na kutoa mchango mkubwa kwa pato la taifa. Lakini katika miaka ya hivi karibuni, mji huo pia umejulikana kwa kuwa na idadi kubwa ya wafanyakazi waliopunguzwa kutoka kwenye viwanda vya serikali na kubeba mzigo mkubwa wa jamii. Sababu muhimu kufikia hatua hiyo ni kwamba katika kipindi cha katikati na mwisho mwa karne iliyopita, ili kuviwezesha viwanda vya serikali kupunguza mzigo wake na kuwa na nguvu ya kutosha ya kufanya mageuzi ya teknolojia na kuvumbua bidhaa za aina mpya, mji huo ulifanya marekebisho makubwa na kuanzisha mfumo mpya wa uzalishaji katika viwanda vya serikali ambapo idadi kubwa ya ziada ya wafanyakazi walipunguzwa, na iliwahi kufikia laki nne na elfu kumi wakati fulani.

    Kuwatafutia ajira wafanyakazi hao waliopunguzwa lilikuwa ni jukumu la serikali ya mji wa Shenyang na idara ya dhamana ya jamii. Naibu mkurugenzi wa idara ya kazi na dhamana ya jamii Bw. Song Naiyi alisema, "Mambo tuliyofanya hasa ni kuwasaidia kutokana na kuweka sera, kuwapatia huduma ya ajira na mikopo midogo ili kuwawezesha kupata nafasi mpya za kazi. Hivi sasa kazi zetu hizo zimepata mafanikio."

    Naibu mkurugenzi Song alisema kuwa wafanyakazi waliopunguzwa karibu wote walikuwa wanatoka katika viwanda vya serikali, na ingawa hawakuwa na ufundi mkubwa, lakini walifanya kazi kwa makini na bila kujali taabu. Kulikuwa na kazi nyingi zinazowafaa, na mji wa Shenyang uliwatafuta njia nyingi za kuwapatia ajira. Kwanza, serikali ya mji ilibuni sera zinazowasaidia na kuwahamasisha kujiajiri wenyewe. Wafanyabiashara wanaoanzisha viwanda vyao binafsi, wanasamehewa kodi kwa miaka mitatu isipokuwa wale wanaojihusisha na ujenzi wa majengo na burudani. Kwa wale wasio na mitaji ya kuanzisha shughuli za biashara, serikali inawapa mikopo isiyo na riba au mikopo yenye riba ndogo.

    Katika miaka ya hivi karibuni, serikali ya Shenyang ilibuni sera nyingi zinazohimiza viwanda na makampuni kuajiri wafanyakazi waliopunguzwa kutoka kwenye viwanda vya serikali. Viwanda vinavyowaajiri wafanyakazi hao kiasi cha kufikia 30% ya idadi ya wafanyakazi, vinasamehewa kodi za aina nyingine 5 ikiwemo kodi ya biashara kwa miaka mitatu. Kwa kuvutiwa na sera zenye nafuu, viwanda vingi vimeajiri wafanyakazi waliopunguzwa kutoka viwanda vya serikali. Meneja mkuu wa kiwanda kimoja binafsi Bw. Teng Yan-ping alisema, "Mwaka huu tuliajiri wafanyakazi 53 waliopunguzwa kutoka viwanda vya serikali. Wafanyakazi hao ni watulivu na wana bidii kazini. Licha ya hayo, kiwanda chetu kimepunguziwa gharama kutokana na sera mwafaka za serikali."

    Ajira kwa wafanyakazi waliopunguzwa kutoka kwenye viwanda vya serikali wenye umri mkubwa ni tatizo moja kubwa, kwa kuwa wamekosa nguvu ya kujiajiri, na viwanda havipendi kuwaajiri. Kwa watu hao, serikali ya mji wa Shenyang inatumia njia ya kuanzisha kazi za huduma ya jamii zikiwa ni pamoja na kuchunga usalama kwenye mitaa, kuweka utaratibu mzuri wa mawasiliano barabarani, kupanda maua na majani kandokando ya barabara na kutengeneza njia. Kazi hizo zilizoanzishwa na serikali ya mji wa Shengyang zimetoa ajira kwa kiasi cha wafanyakazi elfu 20 waliopunguzwa kutoka kwenye viwanda vya serikali.

    Aidha, serikali ya mji wa Shenyang ilianzisha vituo vya mafunzo na huduma katika mitaa mbalimbali, ili kuwapa watu hao elimu za kompyuta na uhasibu ili kuongeza uwezo wao wa kazi ili kukabiliana na ajira mpya. Licha ya hayo, serikali ya mji wa Shenyang pia inaitisha mazungumzo ya ajira ili kuleta nafasi nyingi kwa wafanyakazi waliopunguzwa kutoka kwenye viwanda vya serikali kupata ajira mpya. Baada ya watu hao kupata ajira mpya katika viwanda, serikali ya mji pia inahimiza kutia saini mikataba ya kazi kati ya viwanda na wafanyakazi hao na kuwawekea bima ya jamii ili kuwapa dhamana ya haki zao.

    Kutokana na jitihada za serikali ya Shenyang, karibu wafanyakazi laki 3 na elfu 60 kati ya laki nne na elfu kumi waliopunguzwa kutoka kwenye viwanda vya serikali wamepata ajira mpya. Bw. Liu Peng ambaye alifanya kazi kwa zaidi ya miaka 30 katika kampuni ya ujenzi mjini Shenyang alipata ajira mpya katika uwanja wa kuegesha magari, alisema, "Hivi sasa ninafanya kazi katika uwanja wa kuegesha magari, nimekuwa na pato zuri pamoja na marupurupu mengine, nimeridhika kabisa, sasa ninafanya kazi bila wasiwasi. Katika kipindi fulani baada ya kupunguzwa kutoka kazini nilikuwa na wasiwasi mkubwa."

    Naibu mkurugenzi wa idara ya kazi na dhamana ya jamii ya mji wa Shenyang Bw. Song alisema kuwa ana imani kwamba katika muda mfupi ujao, wafanyakazi wengi waliopunguzwa kutoka kwenye viwanda vya serikali watapata ajira mpya.

Idhaa ya Kiswahili 2003-03-10