Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2004-04-21 20:32:01    
Sumaye ataka makampuni kuhudumia waathirika wa Ukimwi

cri
Waziri Mkuu Bw. Frederick Sumaye, ametoa wito kwa wamiliki wa makampuni nchini kuwahudumia wafanyakazi wao waliothirika kwa Ukimwi.

    Bw. Sumaye amesema si vema kuwaacha wapoteze maisha waathirika hao na hivyo kulazimika kuingia gharama kubwa ya kuwaajiri wengine.

    Waziri Mkuu aliyasema hayo mwishoni mwa wiki alipokuwa akikabidhi mashine ya kupimia chembe chembe hai za kulinda mwili wa binadamu (CD4), kwa kituo cha Matumaini kinacholea watoto yatima waishio na virusi vya Ukimwi.

    Alisema fedha nyingi zinazotumika kuwatafuta na kuwaajiri wafanyakazi wapya ni bora zikatumika kuwatibu wafanyakazi hao walioathirika na ugonjwa huo ili waendelee kufanya kazi.

    "Inasikitisha sana kuona kuwa wataalam mbali mbali wanapoteza maisha kutokana na ugonjwa huo, na mbaya zaidi waajiri wao kutowathamani na kuwahudumia mara wanapokuwa katika hali hiyo," alisema.

    Bw. Sumaye alitoa wito kwa wananchi na makampuni mengine yenye uwezo, kuwasaidia watoto hao ili kupunguza makali ya ugonjwa huo na hivyo kuwafanya waendelee kuishi kwa matumaini na kwa muda mrefu.

    Mashine hiyo ya CD4 imenunuliwa kwa msaada wa makampuni matatu ambayo ni Shirika la Bima la Taifa (NIC), Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) na Shirika la MEDEX iliyogharimu Sh. milioni 31.

    Naye mlezi mkuu wa kituo hicho Sista Maria Rosalia, alisema mashine hiyo ya CD4 itakuwa inatoa huduma kwa wananchi wote wa Mkoa wa Dodoma na mikoa ya jirani bila kubagua rangi, kabila wala dini.

    Alisema huduma hiyo itakuwa inatolewa kwa gharama ya sh, 4,000 tu ili kuchangia huduma kwa watoto hao, tofauti na huduma ya aina hiyo inayotolewa katika hospitali nyingine kwa gharama ya Sh, 30,000 hadi 40,000.

    Kituo hicho cha Matumaini kina jumla ya watoto 84 wanaoishi na virusi vya Ukimwi na pia kinatoa huduma ya dawa za kurefusha maisha kwa watu walio nje ya kituo hicho.

    Alisema hadi hivi sasa jumla ya watu 100 kutoka nje ya kituo hicho wanapatiwa huduma katika kituo hicho, wakiwemo wanawake wajawazito kwa ajili ya kuwawezesha kutowaambukiza watoto wakati wa kujifungua.

    Kituo hicho kinamilikiwa na masista na mapadre waabuduo Damu Takatifu ya Yesu ambao wako chini ya Kanisa Katoliki. Kilifunguliwa Agosti, 2002 na Balozi wa Papa John Paulo wa Pili nchini Tanzania.

Idhaa ya kiswahili 2004-04-21