Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2004-05-04 21:01:43    
Udumu milele urafiki kati ya China na Tanzania

cri
    Msikilizaji wetu ambaye ni mtanzania lakini sasa anaishi nchini Falem za kiarabu Mbarouk Msabah wa sanduku la posta 52483, Dubai, U.A.E hivi karibuni ametuletea barua akisema kuwa, akiwa Mtanzania, angependa kuchukua fursa hii kutoa pongezi zake za dhati kwa maadhimisho ya miaka 40 tangu kuanzishwa kwa uhusiano wa kibalozi kati ya nchi yake Tanzania na Jamhuri ya Watu wa China .

    Anasema, kwa kweli watanzania wote wanaona fahari kubwa sana kwa maadhimisho hayo, kwani uhusiano wa kirafiki na kindugu kati ya China na Tanzania umekuwa na historia ya muda mrefu tangu pale nchi ya Tanzania ilipojipatia uhuru wake.

    Bwana Msabah anasema, licha ya kuwa waziri mkuu wa Jamhuri ya Watu wa China Bw.Zhou Enlai aliwahi kufanya ziara nchini Tanzania katika miaka ya mwanzo ya uhuru wa Tanzania, China ilikuwa ni moja kati ya mataifa ya mwanzo kabisa yaliyokuwa mstari wa mbele kuisaidia Tanzania katika kujenga mustakabali wake wa baadaye, pamoja na kuboresha maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa wananchi wake.

    Moja kati ya juhudi kubwa zilizofanywa na Jamhuri ya Watu wa China nchini Tanzania ni ujenzi wa Reli ya "TAZARA" iliyounganisha bandari ya Dar es Salaam na nchi ya Zambia. Hatua ambayo imesaidia sana kukuza maendeleo ya kiuchumi katika eneo zima la Mashariki na Kusini mwa bara la Afrika. Vile vile China imekuwa ikisaidia sana katika ujenzi wa viwanda, barabara, hospitali na maeneo mbalimbali ya kiserikali na kiraia nchini Tanzania kunzia miaka ya 60 hadi hii leo.

    Anasema, wataalamu wa China wamekuwa wakifanya kazi bega kwa bega na Watanzania katika sekta za huduma mbali mbali za kijamii, jambo ambalo limekuwa likishukuriwa mno na Watanzania.

    Bwana Msabah anasema, ni vigumu kueleza yale yote ambayo yameufanya uhusiano wa Tanzania na Jamhuri ya Watu wa China kuimarika katika msingi wa kusaidiana kindugu na kirafiki kwa maslahi ya pande zote mbili.

    Watanzania na Wachina wana kila sababu ya kufurahia siku ya kuadhimisha mika 40 tangu pale waliposhikana mikono na kuanza urafiki wao.

    Mwisho Bwana Msabah ametuandikia shairi lake maalumu alilolitunga kwa ajili ya maadhimisho ya mika 40 ya uhusiano wa kibalozi kati ya China na Tanzania, shairi hilo linaitwa: "Udumu urafiki wa China na Tanzania".

                                             Udumu Urafiki China na Tanzania

                                             Ni miaka arobaini, sasa imeshatimia

                                             Sote tusheherekeni, China na Tanzania

                                              Tujae matumaini, urafiki utaendelea

                                               Udumu urafiki, China na Tanzania.

                                               Furaha haisemeki, leo tunafurahia

                                              Umedumu urafiki, China na Tanzania

                                              Kamwe hautetereki, wazidi kushamiria

                                              Udumu urafiki, China na Tanzania.

                                               Tangu enzi za uhuru, China ilijitolea

                                               Ilikua kama nuru, inayo tuangazia

                                               Nasi tunaishukuru, juhudi imechukua

                                               Udumu urafiki, China na Tanzania.

                                               Tuliotesha mbegu, nakisha kuipalilia

                                               Kwa uwezo wa Mungu, ikaota na kuchanua

                                               Leo sote ni kama ndugu, Wachina na Watanzania

                                               Udumu urafiki, China na Tanzania.

                                               China ni kipenzi chetu, Watanzania twajivunia

                                               China ni rafiki yetu, vyema twamtambua

                                               China ndiye mwenzetu, mikono twamshikilia

                                               Udumu urafiki, China na Tanzania.

    Na msikilizaji wetu Epaphra S. Deteba wa sanduku la posta 20166 Dar es Salaam Tanzania alisema katika barua yake kuwa, kutokana na vipindi vya idhaa ya kiswahili ya Radio China kimataifa wasikilizaji wetu wamepata habari mbalimbali kuhusu mawasiliano kati ya China na Tanzania na wametiwa moyo na kuona kuwa China na tanzania ni nchi zinazoshirikiana vizuri, hivyo aliipa heko Radio China kimataifa kwa vipindi makini na murua kwa lengo la kuwapasha habari wasikilizaji wa idhaa ya kiswahili ya Radio China kimataifa, alisema, endeleeni na motomoto huo huo.

    Kama msikilizaji wetu Nelson Baregu wa sanduku la posta 2565 Mwanza Tanzania alivyosema katika barua yake kwetu kuwa , vipindi vya idhaa ya Kiswahili ya Radio China kimataifa vinatujenga, hasa kwa wanafunzi kama yeye vinawasaidia kupanua uelewa wao ndani na nje ya nchi na kuongeza maelewano na urafiki katika ya Radio China kimataifa na wasikilizaji wake. Anatuunga mkono katika juhudi za kufanya kazi.

    Barua za wasikilizaji wetu wengi zinatutia moyo tuendelee kufanya kazi vizuri zaidi ili kuboresha vipindi vyetu na kufanya juhudi katika kuwahudumia wasikilizaji wetu. Kazi nyingi tumefanya lakini bado tunapaswa kuendelea na kazi nyingi tunazotakiwa kufanya. Tutachapa kazi bila kulegalega ili kuwaridhisha wasikilizaji wetu, na kwa kupitia matangazo yetu kulenga kuongeza maelewano kati yetu na wasikilizaji wetu na kuzidisha urafiki kati ya wananchi wa China na Tanzania pamoja na nchi nyingine za Afrika.

    Wasikilizaji wapendwa, mlikuwa mkisikiliza maelezo yasemayo:Udumu urafiki China na Tanzania, kesho tarehe 26 itakuwa siku ya maadhimisho ya miaka 40 ya uhusiano wa kibalozi kati ya China na Tanzania, kesho tutaendelea na sehemu nyingine ya kipindi maalum cha maadhimisho ya miaka 40 ya uhusiano wa kibalozi kati ya China na Tanzania , msikose kuwa nasi.

Idhaa ya Kiswahili 2004-05-04