|

Jimbo la Shanxi linajulikana kwa kulima ngano, hivyo chakula kikuu cha wenyeji ni unga wa ngano. Kwa muda mrefu watu wamefahamu tabia ya ngano, na wamevumbua mapishi mengi kama vile: kuchemsha, kukaanga na kuoka na hatimaye kuunda utamaduni wa unga. Mababu wa kale walisema: Chakula kwanza ni kwa ajili ya shibe, halafu urembo. Kuhusu urembo wa chakula cha unga hutumiwa sana nyakati za sikukuu na sherehe. Kwenye mikate hutiwa michoro ya aina mbali mbali.
Kwenye arusi, mkate mmoja tu hutumia unga kilo 5 hivi. Michoro kwenye mikate hutofautiana hapa na pale. Sehemu ya kaskazini ya jimbo hilo hupenda kufinyanga sungura aliyebeba fyulisi, samaki wa dhahabu aliyebeba mkomamanga, ina maana ya kuwa bi-arusi ataishi maisha marefu na kupata watoto wengi. Lakani sehemu ya kusini hupenda kufinyanga maua, ndege na wanyama. Mikate ya aina hiyo huzawadiwa bwana arusi kwa bi-arusi. Kwa kawaida bi-arusi hukataa kunawa na kujipamba mpaka kwanza zawadi hiyo ya mikate ifike katika siku ya ndoa.

Katika sherehe mbalimbali kama vile kuzaliwa kwa mtoto, kutimiza mwezi mmoja kwa mtoto tangu kuzaliwa, siku ya kuzaliwa kwa watu wazima na hata katika mazishi huhitajiwa mikate hiyo iliyonakshiwa.
Sikukuu kubwa kabisa ni sikukuu ya chipuko. Siku ya Majiko ya Desemba 23 ni sikukuu ya kuaga mwaka mkongwe na kukaribisha mwaka mpya. Katika siku hiyo watu hufinyanga mikate ya "Zaosha" kama sadaka kwa Mungu wa jiko ili awaletee baraka. Katika sikukuu ya Qingming, wakati mimea inapoanza kuchipuka baada ya siku za baridi, watu wanatunga mikate ya "Hanyanshan" kwenye matawi ya miti na kutundika majumbani mwao. Akina mama hupata fursa ya kufunzana wakati wa kufinyanga mikate na kuvumbua aina mpya.
Mikate hiyo hufinyangwa kwa unga wa ngano iliyovunwa mwaka huo huo. Baada ya kuchanganywa maji na kuachwa kuchacha kwa muda fulani huongezwa unga kiasi na kuachwa tena uchache halafu hukandwa mpaka tabaka ya juu ya kinyunya ing'ae.
Wafinyangaji huwa wanawake wa nyumbani. Tangu utotoni mwao wanaishi kwenye utamaduni huo, kwa hivyo hupata uzoefu bila ya mafunzo maalumu. Wao hutumia kitana na mkasi kunakshi mikate, halafu huipamba kwa tende na maharage ili kutengenezea macho na vinywa, mwisho huoka. Mikate ya sanamu na huwapa watu matumaini ya furaha.
Idhaa ya Kiswahili 2004-05-07
|