Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2004-05-12 19:04:20    
AIDS(UKIMWI)

cri
    AIDS ni ugonjwa ambao hatuna hata jina lake katika lugha yetu. Kwa maelezo ya makato tunaweza kusema kwamba huu ni ugonjwa wa siri kwa kuwa asilimia tisini ya wale walio nao wanaambukizwa na zinaa.

    Ujuzi wetu kuhusu ugonjwa huu bado sio kamili, lakini unaongezeka haraka sana siku hadi siku. Maelezo yaliyotolewa katika kitabu hiki huenda yakahitaji masahihisho fulani fulani hapo baadaye kulingana na ujuzi mpya utakaopatikana kutokana na utafiti mkali unaoendeshwa sehemu (nyingi) mbalimbali duniani kuhusu ugonjwa huu.

    Yafuatayo ni baadhi ya maswali ambayo watu wengi wamekuwa wakiyaulizauliza kuhusu ugonjwa huu:

    Neno AIDS maana yake nini?

    AIDS ni kifupi cha maeneo manne ya Kiingereza-Acquired Immune Deficiency Syndrome.

    Sydrome maana yake ni matokeo, au kikundi cha dalili, au kikundi cha mambo yanayojitokeza pamoja.

    Acquire maana yake ni kukumbwa na

    Immune maana yake ni uwezo wa mwili wa kujihami dhidi ya magonjwa.

    Deficiency maana yake ni upungufu, au dosari, au kuwa duni.

    Tafsiri ya Kiswahili ya maneno hayo ya Kiigereza "The Syndrome of Acquired Immune Deficiency" ni Matokeo ya Kukumbwa na Hali Duni ya Kujihami. Kama tunavyofahamu kujihami kunahitaji kuwa na silaha. Ndio kusema basi kwamba mwili wenye Hali Duni ya Kujihami ni mwili ambao silaha zake za kujihami zimeburugika.

    Kwa hiyo tafsiri nyingine ya Kiswahili kilicho rahisi zaidi kuelezea maana inayofanana na maneno hayo ya Kiingereza "The Syndrome of Acquired Immune Deficiency" ni Matokeo ya Hali ya Burugiko la Silaha za mwili, na kifupi chake kinaweza kutupatia neno UKIMWI. U inasimama badala ya ukosefu, KI inasimama badala ya kinga. MWI inasimama badala ya mwilini.

    Neno hili UKIMWI licha ya kuwa tafsiri ya AIDS, linasaidia sana kutoa picha sahihi ya mtu mwenye ugonjwa huo. Kama tutakavyoona hivi punde, mtu mwenye UKIMWI (AIDS) ni sawa na askari ambaye amenyang'anywa silaha, yaani ni UKIMWI, hawezi kujitetea.

    UKIMWI(AIDS) husababishwa na nini? 

    UKIMWI husabaishwa na viini vidogo sana sana vyenye uhai ambavyo wataalam huviita "VIRUS". Hivi ni viumbe vidogo sa-a-na ambavyo havionekani kwa macho wala kwa darubini za kawaida. Viumbe wa kabila hili la "virus" wapo wa aina nyingi na hutofautiana kwa maumbile na kwa madhara au magonjwa wanayoleta. Kwa mfano kuna virus wanaoleta ugonjwa wa mafua; na kuna virus wanaoleta ugonjwa wa surua; n.k.

    Kwa kawaida mwili unao katika damu chembechembe maalum ambazo hutumika kama askari au silaha za kupigana na maadui, yaani viini vinavyoleta magonjwa. Viini vinavyoleta UKIMWI (AIDS) vikipata nafasi ya kupenya na kuingia katika damu yako vitaanza kuingia ndani ya baadhi ya chembechembe hizo maalum ambazo ndizo zenye jukumu la ulizi na usalama mwilini. Baadhi ya chembechembe hizo zilizoingiliwa huweza kufa baada ya muda wa siku 20 hivi; baadhi nyingine huenda zikadhurika lakini zisife; na baadhi nyingine huenda zikadhurika kidogo tu. Kwa vyovyote viini vya UKIMWI ni kiboko kikali kwa chembechembe hizi ambazo ni baadhi ya silaha muhimu za mwili.

    Viini vya UKIMWI vitakavyoingia ndani ya chembechembe hizo maalum za kujihami vitaweza kuendelea kuzaana humo na baadhi yake vitaweza hata kutoka na kuingia katika ubongo ambako vitaweza kujificha ama kuendelea kuzaana.

    Viini hivyo vya UKIMWI vinapoendelea kuishi mwilini mwako huenda mambo matatu yakaweza kutokea baada ya kupita muda wa miezi minne mpaka miaka mitano au zaidi.

    1. Utaweza kunyemelewa na magonjwa ya hatari ambayo yatakuletea kifo. Jambo hilo likitokea tutasema umepatikana na UKIMWI Moto.

    2. Utaweza kunyemelewa na magonjwa rejareja yasiyoweza kuleta kifo. Jambo hilo likitokea tutasema umekumbwa na UKIMWI Vuguvugu.

    3. Utaweza kuendelea kuwa na afya nzuri kama kawaida ya watu wengine. Jambo hilo likitokea tutasema kwamba UKIMWI uliyo nayo ni Baridi.

Idhaa ya Kiswahili 2004-05-12