Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2004-05-13 19:41:35    
Kukua Pamoja Katika Miji

cri
    Kutokana na marekebisho ya miundo ya uzalishaji wa kilimo na uharakishaji wa mchakato wa kukuza miji midogo midogo nchini China, nguvu kazi zilizobaki vijijini zinahamia mijini siku hadi siku, na namna ya kuwapatia watoto wa vibarua mijini elimu nzuri pia limekuwa suala linalofuatiliwa na watu.

    Shule ya msingi ya Yuquanlu iliyoko mtaa wa magharibi ya mji wa Beijing ina wanafunzi zaidi ya 500, asilimia 90 ya wanafunzi hawa ni watoto wa vibarua mijini kutoka sehemu mbalimbali nchini China.

    He Xiaofeng mwenye umri wa miaka 12 mwaka huu ni mwanafunzi wa kike wa darasa la 5 wa shule ya msingi ya Yuquanlu. Alikuja mji mkuu Beijing pamoja na wazazi wake kutoka kijiji kimoja cha mkoa wa Sichuan alipokuwa ma umri wa miaka 4. Baba yake anafanya kazi ya kibarua katika kiwanda kimoja cha Beijing, mama yake ni msafishaji wa kiwanda hicho, mapato yao ya pamoja ya kila mwezi ni yuan za renminbi 2000 hivi. Maisha yao ya mjini ni mazuri zaidi kuliko kijijini. Lakini wakati binti yao He Xiaofeng alipofikia umri wa miaka 7,walikabiliwa na shida ya kutoa gharama kubwa ya kumpeleka binti shuleni. Kutokana na utaratibu wa wakati huo, kama watoto wa familia isiyo wakazi wa kudumu wa Beijing wakitaka kusoma katika shule za kiserikali,lazima walipe gharama kubwa za masomo. Hivyo, wazazi wa He Xiaofeng walipaswa kumpeleka katika shule moja ya kibinafsi.

    Miaka miwili iliyopita, mji wa Beijing ulianza kulegeza sharti kwa watoto wa vibarua kuingia katika shule za kiserikali za Beijing,watoto wa vibarua wanaweza kusoma katika shule za Beijing kwa kulipa yuan kidogo tu. Zaidi ya hayo, katika sehemu vibarua wengi wanakoishi, zimejengwa shule maalum za msingi na sekondari kwa ajili ya watoto wao, na Shule ya msingi ya Yuquanlu ndiyo mojawapo.

    Mkuu wa shule ya Yuquanlu Bi.Wang Mei alisema: "Shule yetu ilijengwa mwaka 1986,mwanzoni ilikuwa shule ya kawaida,tuliwaandikisha watoto wote wa wakazi wenyeji na wa wafanyakazi kutoka sehemu nyingine. Kwa sababu idadi ya watoto wa vibarua ni wengi sana, ili kuwapatia watoto hao fursa za kwenda shule, kuanzia mwaka 2002,serikali ya mtaa iliamua kuifanya shule hiyo kuwa shule maalum ya kuwaandikisha tu watoto wa vibarua, na kuwapa huduma bora ya elimu ya mji wa Beijing."

    Shule ya msingi ya Yuquanlu kama zilivyo shule nyingine za mitaa ina walimu bora na vifaa bora. Kwa jumla ina walimu 23, na madarasa 9, kila darasa ina vifaa vya kisasa vya masomo kama vile kompyuta na vinginevyo.

    He Xiaofeng na wazazi wake wanakaa karibu na shule ya msingi ya Yuquanlu, zaidi ya mwaka mmoja uliopita, He Xiaofeng alihamia hapo kutoka shule ya kibinafsi aliyosoma, na ameteuliwa kuwa kada wa darasa kutokana na masomo yake mazuri na mienendo mizuri. Katika miaka miwili iliyopita, He Xiao Feng ni mwanafunzi hodari katika kila upande, akasifiwa sana na walimu wa shule hiyo.He Xiaofeng alisema kuwa,anafurahia sana kusoma katika shule ya msingi ya Yuquanlu. Akisema:"Walimu wa shule hiyo walitutendea vizuri sana, hata baada ya masomo, wanazungumza na sisi kama marafiki. Wanafunzi kutoka sehemu mbalimbali nchini kote tunajifunza pamoja na kucheza pamoja, tuna furaha kubwa."

    Mwandishi wetu wa habari aliambiwa kuwa,walimu wa shule ya msingi ya Yuquanlu waliwafuatilia watoto wa vibarua kama walivyofanya wazazi wa watoto hao, walimu hao wana simu na anuani ya wazazi wa kila mwanafunzi, kama mwanafunzi mmoja akikosa shule, mwalimu wake atawapigia simu wazazi wake ili kujua sababu;hata kama wanafunzi wanapochelewa, walimu walijaribu kuuliza sababu kwanza kabla ya kuwakosoa.Walimu wengine waliwapatia watoto maskini nguo na vitu vingine. Kwa ajili ya kuhakikisha watoto waliokaa mbali kidogo kufika shuleni kwa wakati na salama, shule hiyo pia ilinunua gari maalum la kuwapokea na kuwarudisha wanafunzi nyumbani kwao kila siku.

    Watoto wa vibarua ni wajenzi wa miji, serikali ya China imefuatilia sana ukuaji wao mzuri. Mwezi Septemba mwaka jana,waziri mkuu wa China Wen Jiabao alikwenda kukagua mwenyewe shule ya msingi ya Yuquanlu. Aliwaambia walimu wa shule hiyo kuwapa watoto hao huduma bora ya elimu, na kuwatendea vizuri.

    Katika nusu ya pili wa mwaka jana, China ilizitaka serikali za sehemu zote kuchukua hatua halisi, ili kutatua suala la watoto wa vibarua kupewa elimu ya lazima mijini, na kutoa mwito kwa jamii kuchangia fedha, vifaa kwa watoto wa vibarua wenye matatizo ya kiuchumi ili kuhakikisha watoto wote wanasoma shuleni kama watoto wengine walivyo. Na kazi hiyo imeshapata mafanikio. Sasa mji wa Beijing una watoto zaidi ya laki 2 wa vibarua kutoka vijijini wanaohamahama, ambapo asilimia 80 ya watoto hao wameshasoma shuleni.

    Suala la kuwapatia huduma ya elimu watoto wa vibarua pia limetiliwa maanani sana na jamii ya China. Muda si mrefu uliopita, kampuni moja ilichangia yuan za renminbi milioni 50 kwa mfuko wa maendeleo ya watoto wa China, kuanzisha mfuko wa kwanza wa elimu ya watoto wa vibarua. Fedha hizo zinawasaidia watoto wa vibarua wenye matatizo ya kiuchumi.

    Inafahamika kuwa, sasa katika miji ya China wako vijana na watoto wa familia zinazohamahama milioni 20 hivi,na wengi wao ni watoto wa vibarua. Japokuwa serikali ya China bado haijaweza kutatua kikamilifu suala la elimu ya watoto hao wote, lakini serikali na jamii ya China nzima imetilia maanani na kufuatilia suala hilo, hivyo suala la elimu ya watoto wa vibarua kutoka vijijini litatatuliwa hatua kwa hatua.

Idhaa ya Kiswahili 2004-05-13