Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2004-05-14 18:47:22    
Mkulima aliyetajirika kwa ufugaji wa ng'ombe

cri
    Katika wilaya ya Wuchuan ya mkoa ujiendeshao wa Mongolia ya ndani, sehemu ya kaskazini ya China, watu wengi wanamzungumzia mkulima kijana Fan Fushou na mkewe Zhula, anayetoka nchini Mongolia, ambao wametajirika kutokana na ufugaji wa ng'ombe. Hivi karibuni, mwandishi wetu wa habari alifika wilaya ya Wuchuan kuwaona wanandoa hao.

    Siku mwandishi habari alipofika nyumbani kwa mkulima Fan Fushou, kijana huyo alikuwa akitayarisha zawadi, na kuijiandaa kumpeleka mkewe na mtoto wake kwenda nchini Mongolia kuwaona baba na mama mkwe. Fan Fushou ni kijana mrefu na mpole; mkewe ambaye ni mzaliwa wa Ulan Bator, mji mkuu wa Mongolia, ni mrembo mwenye ngozi nyeupe na nywele ndefu.

    Miaka mitano iliyopita, kijana Fan Fushou alikwenda Ulan Bator kufanya kibarua ambapo alifahamiana na msichana Zhula ambaye alikuwa akifanya kazi katika saloon moja karibu na kiwanda alichofanya kazi. Fan Fushou alisema, "Wakati nilipofanya kibarua mjini Ulan Bator, alikuwa anafanyakazi ya kutengeneza nywele ambapo nilikwenda kukata nywele mara kwa mara, tukafahamiana, na nilikwenda kumwangalia kila nilipopata nafasi. Baada ya kufika huko, nilikuwa na matatizo ya mawasiliano kutokana na lugha tofauti lugha, hivyo alinisaidia katika shughuli zangu nyingi. Baada ya kuchumbiana kwa zaidi ya miaka miwili, tulijiandikisha na kufunga ndoa huko Ulan Bator."

    Fan Fushou anaishi kwenye upande wa kaskazini wa mlima Yin, sehemu ya kati ya mkoa wa Mongolia ya ndani. Wakulima wa huko wanaishi kwa kilimo kizazi baada ya kizazi. Ingawa ardhi ya huko haina rutuba na kutishiwa na hali ya ukame. Katika miaka michache iliyopita, familia ya Fan Fushou ililima zaidi ya hekta mbili ambazo katika mwaka wenye mavuno mazuri kabisa, pato lake lilikuwa kati ya Yuan elfu tano au sita, kiasi hiki ni kati ya dola za kimarekani 610 na 732. Tangu serikali ianzishe huko kwao mradi wa kupanda miti kwenye ardhi iliyoendelezwa kuwa mashamba ya kilimo, wakulima wa huko walianza kujishughulisha na shughuli za kiuchumi za aina mbalimbali.

    Familia ya Fan Fushou ilitakiwa kupunguza shamba lake kiasi cha hekta moja. Fan Fushou aliwaza kuwa endapo wanapanda majani katika sehemu hiyo ya shamba lao na kufuga ngombe katika sehemu hiyo itakayopanda majani, licha ya kuweza kuhifadhi ya mazingira ya asili, pia wataweza kuongeza pato lao. Baada ya kushauriana na mkewe, walinunua ng'ombe kumi wa maziwa wenye madoa ya rangi nyeusi na nyeupe kwa kutumia fedha zao zote za akiba pamoja na fedha za mkopo wa benki.

    Kila siku, Fan Fushou anakwenda shambani kulima, au kukata majani na kuyapeleka nyumbani akisaidiwa na mkewe, wakitarajia kuishi maisha mazuri. Zhula alisema, "Napenda kila kitu cha hapa kwa kuwa ninampenda Fan Fushou, ninapaswa kuanzisha hapa maisha yetu wenyewe. Baba na mama mkwe pamoja na wakazi wa hapa pia wananipenda sana, sijioni hata kidogo kama mimi ni mgeni."

    Zhula ni mwanamke mwenye bidii, anafanya karibu kazi zote za nyumbani zikiwa ni pamoja na kulisha ng'ombe, kusafisha zizi, kukamua maziwa na kumsaidia mama mkwe kupika chakula.

    Dada watatu wa Bw. Fan pia wanamsifu sana mke wa kaka yao. Dada wa pili Fan Shuqing alisema kuwa Zhula hatulii, anafanya kazi kwa juhudi kubwa na kutotaka kupumzika.

    Fan Fushou alisema kuwa kuongezeka kwa pato lao kutokana na njia sahihi waliyochagua na sera nzuri za serikali. Alisema, "Tunafuga ng'ombe, tulitoa fedha zetu za akiba na kupata mkopo wa serikali. Sasa pato letu linaweza kufikia Yuan za Renminbi elfu 40 hadi 50 kwa mwaka."

    Hivi sasa, familia ya Bw. Fan ambayo inafuga ng'ombe 20 wa maziwa pamoja na kondoo zaidi ya 40, imenunua trekta, mashine za kukatia majani na kujenga jengo kubwa la kuhifadhia majani mabichi.

    Bw. Fan Fushou alisema kuwa maisha yao mazuri ni ya mwanzo tu. mwaka huu serikali imebuni sera mpya za kupunguza mzigo kwa wakulima, katika miaka ya nyuma, kila mwaka familia yao ilipaswa kulipa kodi Yuan mia nane au mia tisa hivi kwa mwaka, lakini mwaka huu wamelipa Yuan zaidi ya mia tatu tu. Baada ya kutoa ardhi yao kwa ajili ya kupanda miti, wakulima walipata msaada wa chakula kutoka serikalini, licha ya hayo wanaweza kuwa na pato lingine kutokana na miti waliyopanda mlimani. Alisema kuwa ana uhakika endapo watafanya juhudi maisha yao yatakuwa mazuri. Ameshauriana na mkewe kuwa wataongeza idadi ya ng'ombe wao ili kuwa na pato kubwa zaidi.

Idhaa ya Kiswahili 2004-05-14