Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2004-05-17 22:21:42    
Mlima wa kwanza wa ajabu na hatari duniani

cri
    Mlima Huashan ni mmoja kati ya milima mikubwa mitano nchini China, watu huuita mlima huo ni "mlima wa kwanza wa ajabu na hatari duniani". Ukiutazama kutoka mbali, utaona maelfu ya vilele vyake vikisimama kama miti msituni, na virefu kama kwamba vimeingia mawinguni. Mandhari zake ni za aina mbalimbali: Ukiangalia kwa karibu, utaona vilele vyake vimechongoka, na vinaonekana maridadi na adhimu kama kwamba vimetengenezwa na miungu na mashetani.

    Mlima Huashan uko sehemu ya kati ya mji wa Huayin, jimboni Shaanxi. Uko Umbali wa kilomita 120 kutoka Xi'an, mji mkuu wa Jimbo hilo. Mlima Huashan umeundwa kwa pandikizi la jabali kamilifu la itale, kimo cha kilele chake kirefu kabisa ni mita 2160.5 juu ya usawa wa bahari. Wachina wa kale walisema kuwa: "Mlima Huashan unatanda kilomita 5, una vilele 5000, lakini ni jabaili moja tu." Jina la Mlima Huashan lilianza kuandikwa katika kitabu cha kale imeandikqa kwamva ukiutazama mlima huo kutoka mbali, sura yake inaonekana kama maua, kwa hivyo ukaitwa Mlima Huashan, m. y. ni Mlima wa Maua.

    Ukitaka kupanda mpaka kilele kikuu cha mlima huo, njia ya kwanza unayolazimika kupita ni Qianchichuang. Kwa mujibu wa maelezo ya kitabu hicho, waliotangulia kugundua njia hiyo ya hatari walikuwa watu wa enzi ya Han, ambao waliona tumbili wakipanda na kushuka mlimani huko Qianchichuang, basi wao pia walipanda juu kwa kufuata njia hiyo. Katika enzi zilizofuata, njia hiyo iliyotumiwa na tumbili ikawa mchirizi wa wima kutoka juu hadi chini. Hadi mwisho wa enzi ya Ming na mwanzo wa enzi ya Qing, mchirizi huo ulichongwa kuwa ngazi ambayo ina vidato 370. Kando ya ngazi hiyo sasa kuna mnyororo unaosaidia wapandaji. Wakati wa kupanda ukiinua kichwa kuangalia juu, utaona mstari mmoja tu wa mbingu na ukiinamisha kichwa kutazama chini, utahisi kama kwamba uko kando ya kisima kirefu sana; lakini unapofika kileleni, mara utapata hisia ya kuwa umeshavuka mpaka wa ubinadamu na kutengana na maisha ya kawaida.

    Baada ya hapo, utaweza kufuata ukingo wa kilele kupita Genge la Ca'er. Chini ya miguu yako ni bonde lenye kina kirefu, mwili wako hauna budi kusogelea inakubidi usogee mbele kwa kushika sehemu zile zilizobenuka. Uso na masikio yako vitakuwa vinakwaruzwa mara kwa mara na ukuta. Katika shairi la Yuan Hongdao wa enzi ya Ming, aliandika:"ukitaka kujua hatari ya njia ya gengeni ikoje, tafadhali angalia mwani wa unyevu iliyobaki usoni mwangu."

    Lakini sasa njia hiyo imeshapanuliwa, imeshachongwa vidato na kuwekwa wigo. Hakuna hatari tena.

    Baada ya kupanda Kilima Canglong utahisi kama kwamba umefika ncha ya mawingu, moyo wako utakudundadunda. Inasemekana kwamba Han Yu, mshairi maarufu wa enzi ya Tang, alipopanda Mlima Huashan na kufika Canglong kutalii, alilia kwa kuogofywa na hatari yake. Tangu hapo ikaenea hadithi kwamba alitupa kitabu na kuomba msaada kwa kupiga yowe.

    Utamaduni wa Mlima Huashan ni tele na wa miaka mingi. Katika kitabu cha historia kiitwacho "kumbukumbu ya historia" imeandikwa kwamba Wafalme Huangdi, Yao na Shun, waliwahi kutalii mlima huo. Wafalme wa kwanza wa Enzi ya Qin, Mfalme Wudi wa Enzi ya Han, mfalme wanamke Wu Zetian na Mfalme Xuanzong wa Enzi ya Tang, waliwahi kufika huko kutambika mbingu na ardhi. Zaidi ya hayo, wasomi mashuhuri wengi wasiotaka udhia, waliondoka mijini na kwenda huko kuishi na kuwafundisha wanafunzi. Mlima Huashan pia ni mojawapo ya sehemu muhimu za dini ya kitao nchini China. Mpaka sasa bado yako mapango 72 na mahekalu 20 ya dini hiyo. Watu wengi mashuhuri waliandika mashairi, kumbukumbu za mambo ambyo yalichongwa kwenye mabamba ya mawe na makala kuhusu Mlima Huashan kwa jumla 1200. Aidha, yako maandiko 1000 yaliyochongwa kwenye majabali.

   Miaka ya karibuni, majengo mengi yanayohusu utalii yamejengwa. Taa za kumulika njia, simu na vyifaa vingine vya mawasiliano vimeshawekwa. Hotele na mikahawa imeshajengwa juu na chini ya mlima huo. Njia za nyaya za chuma imekamilika kujengwa na kuanza kutumiwa. Sasa watalii wanaweza kufika Kilele cha Kaskazini kwa kupanda vigari vinavyoning'inia kwenye nyaya hizo. Watalii wanaongezeka kila usiku uchao.

Idhaa ya Kiswahili 2004-5-17