Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2004-05-18 22:21:53    
"Yao Ming ni balozi mzuri wa China"

cri
    Mbarouk Msabah wa P.O.BOX 52483, Dubai, U.A.E ametuletea barua akiandika makala maalum yasemamayo Yao Ming ni balozi mzuri wa China. Anasema:

    Yao Ming mwanamichezo wa Kichina mwenye umri wa miaka 23 na urefu wa mita 2.26 mzaliwa wa Shanghai nchini China, anaonekana kuwa ni mmoja kati ya Wachina watakao weka historia kubwa ya umashuhuri kote ulimwenguni, kwani hata jarida mashuhuri la kimarekani "THE TIME" katika toleo lake la mwezi April mwaka huu wa 2004, lilimuorodhesha Yao Ming kati ya watu 100 mashuhuri kabisa duniani.

    Mchezaji huyo hodari wa mpira wa vikapu (basketball) wa kichina, ambaye sifa za uhodari wake hatimaye zilimfikisha nchini Marekani mwezi Oktoba mwaka 2002, pale alipoanza kuichezea timu ya Huston Rockets katika mashindano ya shirika la NBA lenye kuwashirikisha wachezaji mashuhuri wa kulipwa katika mchezo huo kote duniani, umashuhuri wake haukuishia katika viwanja vya mpira wa vikapu pekee kote nchini Marekani, lakini pia Yao Ming ameonekana ni   mwanamichezo mwenye kutajika na kupendwa mno nchini Marekani na nchi za nje na hata kufananishwa na wanamichezo maarufa wa kimarekani kama vile Michael Jordan au Tiger Woods.

    Isitoshe na hayo, Yao Ming tayari ameshakuwa na mkataba wa matangazo ya biashara na kampuni mashuhuri ya kimarekani ya migahawa ya vyakula ya MacDonal na vile vile mashirika mengine makubwa ya kibiashara ya Marekani kama vile Reebok, Pepsi, Apple na Visa yameshaonesha hamu yao kubwa ya kuutumia umashuhuri wa Yao Ming katika matangazo ya kibiashara.

    Juu ya yote hayo, Yao Ming hakusahao kutoa mchango wake nyumbani alikotoka yaani China, kwani alishiriki vilivyo na kuwa mstari wa mbele katika kampeni kubwa za kupambana na ugonjwa wa homa ya mapafu "SARS" ulioikumba China mwaka jana, jambo ambalo lilisaidia sana kufaulu kwa kampeni hizo.

    Bila shaka yoyote, Yao Ming anaonekana kuwa ni kama "Balozi" mzuri wa China kwa nchi za nje na pia ni mmoja kati ya vizazi vipya vya Jamhuri ya Watu wa China, ambavyo vinaudhihirishia ulimwengu juu ya ufahari na ufanisi mkubwa wa kimichezo wa China, chini ya malezi na mafundisho ya jamii za kisoshalisti za nchi yenu. Ni wazi kabisa Wachina wana kila sababu za kujivunia kijana wao huyo aliyejipatia umaarufu kote duniani katika kipindi kifupi tu.

    Mimi binafsi ni shabiki mkubwa na mchezaji wa mchezo huo wa mpira wa vikapu tangu nikiwa shuleni, kwa hivyo nitafurahi sana ikiwa Radio China Kimataifa itachukua juhudi za kutusimulia historia ya Yao Ming kwa kupitia vipindi vyake au hata kutoa maelezo kama hayo katika tovuti yenu mpya ndani ya mtandao wa Internet.

Idhaa ya Kiswahili 2004-05-18