Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2004-05-19 21:08:56    
Makumbusho Binafsi

cri
    Makumbusho huwa ya serikali, lakini katika miaka ya karibuni yametokea makumbusho binafsi mjini Beijing. Siku chache tu zilizopita makumbusho binafsi mengine zaidi matatu yametokea.

    Mwezi Novemba mwaka jana, majumba ya makumbusho ya kauri za kale ya Lu Mingtang, makumbusho ya sanaa za kiasili ya Song Tangzhai na makumbusho ya sanaa ya Jin Tai yalianza kufunguliwa katika nyakati tofauti mjini Beijing. Makumbusho hayo ni ya binafsi. Kuanzia mwaka 1996 makumbusho kama haya yameongezeka hadi kufikia manane. Mkurugenzi wa Ofisi ya Makukmbusho katika Idara ya Mabaki ya Kihistoria ya Beijing, Bi. Liu Chaoying anaona kuwa kuibuka kwa makumbusho hayo kunatokana na ustawi wa uchumi wa taifa na maisha ya wananchi kuboreka. Alisema, "Kufuatana na uchumi wa taifa unavyoendelea kukua, maisha ya wananchi pia yanaboreshwa zaidi, na yanapofikia kiwango fulani yataingia kwenye uwanja wa utamaduni. Sababu ya pili ni kwamba, baadhi ya watu wametajirika, wana uwezo wa kununua vile vitu vya zamani vilivyopotelea nchi za nje ili kuwaonyesha wananchi wenzao na kuwafurahisha kwa vitu vya mababu zetu. Hiki ni kitendo kinachothamini utamaduni wetu, ni uzalendo hasa. Kwa hiyo, naona makumbusho ya binafsi hakika yataendelea zaidi."

    Kutokana na maelezo yaliyotolewa, kuanzia miaka ya 90 watu wengi walikuja kuulizia kuhusu uanzishaji wa makumbusho binafsi. Mwaka 1996, Ma Weidu alianzisha makumbusho yake ya vitu vya kale, haya ni makumbusho binafsi ya kwanza kabisa katika Beijing.

    Makumbusho binafsi yametajirisha aina za mabaki ya utamaduni katika hifadhi ya vitu vya kale. Yapo jumla ya makumbusho binafsi manane mjini Beijing. Vitu vingi vilivyoko kwenye makumbusho hayo havimo kwenye makumbusho ya serikali. Kwa mfano, Jumba la makumbusho ya picha za kuchorwa linaloendeshwa na Bwana na Bibi He Yang na Wu Qian, ni jumba la uchoraji la kwanza la binafsi. Pia Jumba la Makumbusho ya Sandali Nyekundu ni jumba la kwanza na kubwa kabisa linalohifadhi samani za kale za sandali nyekundu. Vipande vya kauri ndani ya Makumbusho ya Kauri yaliyofunguliwa karibuni havipo katika makumbusho ya serikali. Kwenye jumba hili vimekusanywa vipande zaidi ya elfu 50, na aina zaidi ya 30, vipande hivi ni kivutio kikubwa kwa washabiki wa kauri ya kale.

    Sio vitu tu vilivyohifadhiwa ndani ya makumbusho ya binafsi ni vya pekee bali pia mtindo wa kuonyesha ni tofauti na yale makumbusho ya serikali. Kwa mfano, jumba la kauri ya kale la Lu Mingtang, limeunganisha maonyesho pamoja na utamaduni wa chai. Jumba la maonyesho pia ni jumba la kunywa chai, rafu za maonyesho zimetenga sehemu sehemu za kunywea chai, watazamaji hufurahia vigae vya kauri huku wakiburudika kwa chai wakiwa wanatumbuizwa na muziki wa kale. Kwa kuzingirwa na mazingira haya watizamaji wanahisi kama wapo kwenye utamaduni wa siku za kale. Isitoshe, kuna sehemu maalumu iliyotengwa kuwaruhusu watizamaji kugusa vitu vya maonyesho. Hali hii pia ni tofauti katika makumbusho ya serikali, kwani huko kila kitu kimebandikwa kitambulisho "Usiguse". Mpenzi wa kauri ya kale Bibi Liang alisema, "Ninapogusa vitu hivi najisikia kuwa karibu sana na vitu vya kale."

    Ili kuwatosheleza wapenzi wa kauri ya kale Lu Mingtang ametenga sehemu ya uchunguzi , "siku ya mapokezi" na "siku ya mhadhara wa wataalamu" ili watalaamu na watizamaji waweze kujadiliana ana kwa ana. Mkuu wa jumba hili Bai Ming alisema, "Ni matarajio yangu ya kuwapatia watizamaji nafasi ya kugusa historia, kuwapa uwanja wa kuchunguza na elimu ya kutofautisha vya kweli na vya bandia."

    Mkurugenzi wa Ofisi ya Makumbusho katika Idara ya Mabaki ya Kihistoria ya Beijing Liu Chaoying anaona kwamba kutokea kwa makumbusho binafsi kunasaidia mambo ya makumbusho kuendelea katika hali nzuri. Kadiri China inavyofungua zaidi ndivyo makumbusho binafsi yatakavyoendelea vizuri zaidi.

Idhaa ya Kiswahili 2004-05-19