Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2004-05-20 19:06:23    
Kituo cha Wasiojiweza mjini Jinan, China

cri

    Kinyume cha hali ya shamrashamra katika likizo la "Mosi Mei" yaani siku ya wafanyakazi duniani, huko kwenye sehemu ya makazi Nam. 306 mjini Jinan nchini China ilikuwa kimya kabisa. Wazee waliotunzwa na wahudumu, baadhi yao walikuwa wakiongea na kuota jua, wengine wakicheza karata, au kufanya mazoezi mepesi ya kutia afya. Hao ni wazee katika kituo kimoja cha wasiojiweza katika mji wa Jinan.

    Mwandishi wetu wa habari alipotembelea huko alimkuta mkurugenzi wa washika zamu akikagua wodi, Bibi Ma Jie, alimwambia mwandishi wetu akisema, "siku zetu za likizo ni sawa na siku za kawaida. Ingawa katika likizo la kila sikukuu ya kitaifa wazee wachache huwa wanachukuliwa na jamaa zao nyumbani, lakini sisi pia tunashika zamu za kutoa huduma. Pamoja na madaktari na wauguzi tuko zaidi ya 70 kushughulika na kazi ya kuwatunza wazee na watoto zaidi ya 300, kati ya watu hao mwenye umri mdogo ni kitoto kichanga aliyezaliwa siku chache tu, na mwenye umri mkubwa ametimiza miaka 106, kwa wastani umri wa watu hao una miaka zaidi ya 80.

    Bibi mzee Zhang Guizhi ana umri wa miaka 88, ameishi katika kituo hiki kwa miaka 8, alisema, "Wahudumu wa hapa ni wazuri kuliko binti yangu, hata binti yangu angejibizana nami asipokuwa na furaha, lakini wahudumu hao kamwe hawakuwahi kuwa na hasira! Mwaka wangu wa kwanza nilipokuja hapa nilipitisha sikukuu ya mwaka mpya nyumbani, lakini baadaye kila mwaka katika siku hiyo naipitisha hapa!" Ndani ya chumba cha nyanya Zhang zilitundikwa ukutani picha za wenzake wa taasisi yake, shule na marafiki wa ng'ambo waliokuja kumtembelea, na picha za nyota wachezaji. Ingawa amekaribia umri wa miaka 90 lakini ana hamu tele na maisha yake.

    Mzee Zhao Yanchang ana umri wa miaka 73, kila siku anaongea ongea na kutembea tembea akiwa katika hali nzuri ya afya. Lakini kabla ya miaka mitano iliyopita alipokuja kituo hiki alikuwa na ugonjwa mzito wa moyo na alilala kitandani tu. Mkurugenzi aliniambia, "Nilimpiga sindano ya kuutilia moyo nguvu mara kadhaa kwa siku, nilidhani angeshindwa kupona, lakini sikutegemea kwamba sasa amekuwa mwepesi wa kutembea, na kuweza kutusaidia kuwatunza wengine!" Naye mzee alisema kwa msisimko, "Alhamdulilahi! Nisingetunzwa nao kwa makini nisingeweza kuishi mpaka leo. Kutokana na kuzeeka nimekuwa mwepesi wa kukasirika, lakini wahudumu wananivumilia. Baadhi ya wenzangu wana udhaifu wa akili, na baadhi wana tabia ya ajabu, hata bila sababu wanapindua meza ya chakula, kuwatukana wahudumu, lakini wahudumu wanasimamisha meza na kusafisha safisha chakula kilichomwagika kimya kimya. Je, hata watoto wao wenyewe wanaweza kuwa hivyo? Wamenitunza mpaka nikaweza kuwasaidia, msaada huu mdogo unanifurahisha moyoni."

    Bi. Ma Jie amewauguza wagonjwa miaka kumi kadhaa, kabla kuja kituo alikuwa muuguzi katika hospitali, anaona, "kazi ya hospitali ni matibabu, lakini kazi ya hapa ni utunzaji licha ya matibabu. Kitu muhimu zaidi lazima tulicho nacho ni upendo licha ya kuwa na majukumu. Hapa hakuwahi kutokea mgogoro kati ya wagonjwa na wahudumu, ni jambo la kawaida kupindua meza ya chakula, hata tuliwahi kumwagiwa mikojo na vinyesi, lakini kwa sababu wao ni wazee punguani, hatuwezi kuhojiana nao kama tulivyokuwa na watu wa kawaida."

    "Usumbufu tulioupata si kitu, kitu kinachotusumbua ni kuwa watoto wao hawaji kuwatembelea wazazi wao. Baadhi ya wazee wanadhani pengine watoto wao watakuja kuwalipia, walituambia kama watoto wao wakija tusisahau kuwaita wasipokuwa chumbani. Mara nyingi tulipogundua watoto wao barabarani tuliwakimbilia na kuwazuia warudi kuwatembelea wazazi wao."

    Saa 11 jioni harufu nzuri ya chakula ilipenyeza puani mwangu, nilisikia kelele, "Chakula tayari!" Niliona wahudumu wakipeleka chakula kwenye kila chumba cha wazee. Wao sio wa familia moja lakini waonekana wenye uhusiano wa karibu zaidi ya familia moja.

Idhaa ya Kiswahili 2004-05-20