Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2004-05-20 20:49:59    
Maisha ya wakazi wa Beijing

cri

    Mji wa Beijing umekuwa mji mkuu wa China kwa zaidi ya miaka 850 . Mji wa Beijing wa sasa si kama tu una barabara nzuri na pana, na majengo merefu ya kisasa pembezoni mwake, pia una vichochoro vingi vilivyopitana, na wale wanaoishi katika mitaa ya vichochoro hivyo huitwa wakazi wenyeji wa Beijing. Wakati mji wa Beijing unapoendeleza kuwa mji wa kisasa na wa kimataifa, maisha ya wakazi hawa pia yamebadilika.

    Mzee Song Lianbao mwenye umri wa miaka 70 mwaka huu anaishi katika nyumba tatu zisizo na ghorofa lililoko karibu na hekalu maarufu ya kibudha-hekalu ya Yonghegong. Mzee Song alianza kuishi hapo alipokuwa na umri wa miezi minne tu. Mzee Song na mke wake mama Xue walizaliwa mjini Beijing, ni wakazi wenyeji kabisa wa Beijing, hivyo bila shaka wanaendelea na desturi za zamani za Beijing, kwa mfano wazee hao wanapenda kunywa kinywaji cha soya. Mzee Song alisema kuwa, kinywaji cha soya ni kinywaji cha kipekee cha Beijing, ambacho kilitengenezwa na maharage ya soya kwa njia maalum, ladha yake ni chachu, watu wa kawaida hawawezi kuzoea, lakini wakazi wenyeji wa Beijing wanakipenda sana kinywaji cha soya. Mzee Song alisema:

    "Ladha ya kinywaji cha soya ni nzuri sana, watu kutoka nje hawapendi kunywa kinywaji hicho, lakini sisi wakazi wa Beijing tunakipenda sana, uchachu ndio ladha yake halisi."

    Japokuwa kinywaji cha soya ni aina moja tu ya vinywaji, lakini kunywa kinywaji hicho kuna utaratibu wake. Mzee Song alisema kuwa, kunywa kinywaji cha soya lazima kula pia mboga ya achali yenye pilipili. Kwa mfano,kisibiti, matango au mafigili ya achali yaliyochanganywa na mafuta yenye pilipili.

    Mzee Song alisema, zamani, wachuuzi wa Beijing huwa walisukuma mikokoteni wakitembeza kinywaji cha soya mitaani. Licha ya kuuza kinywaji cha soya, walikuwepo wachuuzi wengine waliotembeza vitu vidogo vidogo vilivyotumika nyumbani kama vile visu, na kukusanya vitu visivyotumika zilizoweza kurudishwa. Mikokoteni ikifika, wachuuzi huwa walipiga makelele, na wakazi wenyeji huwa walitoka kutoka nyumbani mwao na kununua walivyohitaji. Lakini sasa huduma kama hiyo imetoweka, wakazi wakitaka kunywa kinywaji cha soya au kununua vitu vingine, lazima waende dukani.

    Kufuga wanyama vipenzi ni jambo lingine wakazi wenyeji wa Beijing wapendalo, kwa mfano kufuga njiwa. Njiwa wanaorukaruka angani mwa mji wa Beijing wakipiga makelele nyororo huleta furaha kemkem kwa maisha ya wakazi wengi wa Beijing. Mzee Song ana njiwa zaidi ya 40. Alisema kwa fahari kwamba, njiwa zake wote wameandikishwa katika shirikisho la njiwa la mji wa Beijing, na waliwahi kupata tuzo kwa mara nyingi katika mashindano ya njiwa mjini Beijing. Mzee Song alisema kuwa, ili kuzuia njiwa wake kuambukizwa homa ya mafua ya ndege, kila mwaka anawapa chanjo , na anasafisha vizimba vyao kila siku.

    Kama wakazi wengine wa Beijing, katika miaka kumi kadhaa iliyopita, maisha ya mzee Song yamepata mabadiliko makubwa. Japokuwa nyumba zake zilijengwa zamani kidogo, lakini nyumbani vimejaa vyombo vya umeme vya kisasa, kama vile TV ya rangi, friji, kiyoyozi, jiko la wimbi micro na kadhalika. Mzee Song alisema kwa furaha kwamba, vitu hivi vyote vililetwa na watoto wake .

    Mama Na ana umri wa miaka 72 mwaka huu, anaishi katika nyumba za kijadi za Beijing zenye ua katikati ziitwazo Siheyuan kwa Kichina. Siheyuan za Beijing zilianza kujengwa mjini Beijing kuanzia karne ya 12, nyumba za Siheyuan zilijengwa katika upande wa mashariki, magharibi, kusini na kaskazini zilitazamana na ua upo kati kati. Nyumba hizo ni za mtindo wa kipekee kabisa wa kijadi wa mji wa Beijing. Mama Na ameishi katika nyumba za Siheyuan kwa miaka zaidi ya 40, anapenda sana maisha ya Siheyuan. Alisema kuwa, katika nyumba za Siheyuan alizoishi, kwa jumla wanaishi familia 6, watu kutoka familia mbalimbali wanasikilizana kama familia moja kubwa, anapendelea kuishi katika nyumba za Siheyuan kuliko jumba refu la kisasa.

    "Nafikiri kuishi katika nyumba za Siheyuan ni bora kuliko kuishi kwenye majengo marefu, kila siku wakazi wanakutana kama walivyo wa familia moja, ukiwa na shida ya kimaisha, hakuna matata, watu wote wako tayari kukusaidia."

    Mama Na ni wa kabila la waman. Kwa kuwa enzi ya kimwinyi nchini China, yaani enzi ya Qing ndiyo iliasisiwa na watu wa kabila la waman, na Beijing ni mji mkuu wa enzi ya Qing. Hivyo watu wa kabila la waman wanachukua nafasi kubwa kiasi katika idadi ya wakazi wenyeji wa Beijing. Mama Na alisema kuwa, waman wana mila maalum, nyumbani kwa mama Na hadi sasa bado anaendelea kufuata mila na desturi kadhaa za kabila la waman.Kwa mfano, sikukuu inapofika, jamaa na marafiki huwa wanatembeleana, hasa katika siku kuu ya jadi ya mwaka mpya, watoto wote lazima warudi nyumbani kukutana na kula kwa pamoja na wazazi wao na kukaribisha kwa pamoja siku ya mwaka mpya.

    Wasikilizaji wapendwa, kama Mzee Song na mama Na, wakazi wenyeji wengi wa Beijing bado wanashikilia mila na desturi za Beijing ya zamani, ambazo zina uzito wake wa kiutamaduni kama majengo yaliyo mengi ya kihistoria yanayohifadhiwa mjini Beijing . Lakini kutokana na maendeleo ya haraka ya kiuchumi na kijamii, wakazi wa kizazi kipya wa Beijing wanaoishi katika nyumba za jadi za Siheyuan wamekuwa na fikra tofauti , maisha yao siyo ya pole pole kama wakazi wa zamani, hawawezi kuzoea tena kunywa kinywaji cha soya, wana shughuli nyingi za kufanya, wanaishi kwa njia yao maalum katika mji wa Beijing unaobadilika siku hadi siku.

    Hata hivyo, wakazi wa kizazi kipya wa Beijing bado wanaendelea na desturi kadhaa katika maisha ya zamani. Kwa mfano wanaheshimu utamaduni wa kijadi, kuwapenda watu wa karibuni na kufuatilia sana mambo yanayotokea kila siku nchini China na duniani.

Idhaa ya Kiswahili 2004-05-20