Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2004-05-25 18:19:28    
Barua za Wasikilizaji 25/5/2004

cri

    Msikilizaji wetu Gulam Haji Karim wa P.O.BOX 97, Zanzibar, Tanzania anasema katika barua yake kuwa, hali yake ni nzuri, kwa sasa amerudi Zanzibar kutokana na sababu zisizojulikana. Anaomba barua au vifurushi vyote mtumiwe kwa anuani yake ya zamani. Poleni kwa usumbufu. Anaipongeza Radio China Kimataifa kwa vipindi vyake maalum kwa mujibu wa kutimiza miaka 40 ya kuanzishwa kwa uhusiano wa kibalozi kati ya Jamhuri ya Watu wa China na Jamhuri ya Muungano ya Tanzania, sawa na kutimiza miaka 40 ya muungano kati ya Zanzibar na Tanganyika.

    Anasema katika vipindi hivyo, amewasikia mabalozi pamoja na viongozi wa pande zote mbili wakisifu uhusiano huo, pamoja baadhi ya barua za wasikilizaji kusomwa kuonesha nchi mbili hizi zinavyoshirikiana kirafiki na kindugu hasa kwani nchi ya China imetangulia kujikomboa na kuwa nchi ya mwanzo kuitambua. China ilitoa misaada ya aina mbali mbali kwa Tanganyika na Zanzibar, sisi Zanzibar tumepata kujengwa viwanda mbalimbali kama kiwanda cha sukari Mahonda, kiwanda cha viatu cha Maruhubi na misaada mbali mbali za maendeleo, madaktari na madawa kwa wingi.

    Anapendekeza uhusiano huu usiishie kuadhimisha miaka 40 tu bali uendelezwe na uendelee kwa miaka mingi. Kadiri itakavyowezekana kusaidiana kwa mali na hali, kwa sisi bado tuko nyuma sana kimaendeleo. Japo tunakaribia miaka 45 ya kujikomboa, bado tunakabiliwa na hali ngumu ya kiuchumi. Tumepata maendelo kidogo tu.

    Bwana Gulam anasema , anachukua nafasi hii kukupongezeni kwa kazi kubwa ya kupanga vipindi hivyo, wengi wetu tumepata kujua mengi tusiyoyajua.

    Pongezi ziende kwa uongozi mzima kwa Radio China Kimataifa. Hongera.

    Na msikilizaji wetu Mr. Kilulu Kulwa wa P.O.BOX 161, Bariadi-Shinyanga, Tanzania ametuletea barua akisema kuwa, Tarehe 26 Aprili mwaka huu wa 2004 ilikuwa sikukuu ya kutimia miaka 40 tangu ulipoanzishwa uhusiano wa kibalozi kati ya China na Tanzania.

    Bwana Kulwa anasema, kuanzia tarehe 23 hadi tarehe 29 Aprili 2004 Idhaa ya Kiswahili ya Radio China Kimataifa ilitutangazia kipindi maalumu kilichozungumzia juu ya maadhimisho hayo. Mimi nilisikiliza kwa makini sana na kwa kweli nilivutiwa sana. Kwani Idhaa ya Kiswahili ya Radio China Kimataifa ilifanya mpango maalumu wa kukutana na kuongea na watu mbali mbali, wakiwemo watu maarufu, viongozi na wanadiplomasia kadhaa kutoka pande zote za nchi hizi mbili. Viongozi hao ni pamoja na waziri mkuu wa Tanzania Frederik Sumaye, Balozi wa Tanzania nchini China Ndugu Charles Sanga, mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa Meja General Mwamnyange, mwanadiplomasia mstaafu wa China Bwana Chen, wengine ni pamoja na mpiga picha maarufu wa Tanzania Ndugu Hillary Bujiku na Balozi wa China nchini Tanzania Bw. Yi. Viongozi hao waliweza kutoa maelezo ya kina na yenye kusisimua sana kuhusu uhusiano wa China na Tanzania katika miaka 40 iliyopita, na hasa katika nyanja za siasa, uchumi, utamaduni, miundo mbinu na huduma za jamii.

    Bwana Kulwa anasema , katika mfululizo wa makala hizo tulielezewa pia kwamba Rais wa Kwanza wa Tanzania Marehemu Mwalimu Julius Kambarage Nyerere wakati wa uhai wake aliitembelea China mara 13. Rais mstaafu wa awamu ya pili, mzee wetu Alhaji Ali Hassan Mwinyi aliitembelea China mara 4. Rais wa sasa wa awamu ya tatu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Benjamin William Mkapa ameitembelea China mara nne.

    Bwana Kulwa anasema, China kwa upande wake kuna mamia kwa maelfu ya viongozi na maofisa wa ngazi za juu ambao wamewahi kuizuru Tanzania, akiwemo kiongozi maarufu wa China waziri mkuu marehemu Chou-En-Lai. Wahandisi, madaktari na wataalamu wengineo wengi, ni miongoni mwa wachina wengi ambao wamewahi kuja Tanzania kwa nyakati tofauti ili kuja kuhudumia na kushughulikia mipango ya maendeleo na afya za wananchi wa Tanzania.

    Mtu mwingine maarufu ambaye aliwahi kufanya ziara nchini Tanzania ni waziri mkuu mstaafu wa China ambaye alikuwa spika wa Bunge la Umma la China Bw. Li Peng ambaye aliitembelea Tanzania mwezi Mei mwaka 1997. Wakati huo mimi nikiwa nchini China kwa mwaliko maalumu. Tangu uhuru nchini zetu mbili zimekuwa na ushirikiano mkubwa kabisa, China imeweza kutoa misaada mingi ya hali na mali bila masharti yoyote kwa Tanzania, na ukweli huu unajulikana na watu wote, hivyo katika makala yangu hii sina sababu ya kurejea wasifa, mambo mengi na sifu nzuri zinazojulikana na Watanzania na zilizotolewa na watu mbalimbali kuhusu taifa la China na watu wake na kwa upande wa Tanzania na watu wake. Kwani kukamilisha Taarifa ya shughuli zilizofanyika baina ya China na Tanzania kwa kipindi cha miaka 40 iliyopita itahitaji kutunga kitabu kikubwa kabisa chenye mfano wa Encyclopedia ili kutoa ripoti na kuhifadhi yote yaliyofanyika na yanayoendelea kufanyika baina ya nchi zetu za China na Tanzania.

    Tunaposherehekea na kuadhimisha miaka 40 ya uhusiano wa kibalozi kati ya China na Tanzania ni lazima tuwakumbuke na kuwaenzi mashujaa na waasisi wa mataifa yetu hayo mawili ambao ni mwenyekiti wa China hayati Mao Zedong na Baba wa taifa la Tanzania marehemu mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Uhusiano wetu huu umejengwa katika msingi imara na hauna historia yoyote ya kuzorota au kuteteleka.

    Bwana Kulwa anasema, nikiwa rafiki wa China ninaamini kwamba uhusiano na ushirikiano huu utazidi kuimarika zaidi na kudumu katika vizazi vyote. Ninamaliza kwa ujumbe huu China imara daima, na Tanzania imara daima.

Idhaa ya Kiswahili 2004-05-25