Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2004-05-25 21:54:28    
Mkulima Kiongozi wa Utalii "Mama wa Mwezi"

cri
    Katika lugha ya Kichina, maana ya Yueliang ni "mwezi", katika wilaya ya Yangsuo, mkoani Guizhou, kusini magharibi mwa China, ambayo ni maarufu sana kwa utalii, kuna mlima wa Yueliang, yaani "mlima wa mwezi". Mama Xu Xiuzhen mwenye umri wa miaka 60 hivi mwaka huu anaishi katika kijiji kimoja chini ya mlima huo, kila siku anawaongoza watalii wageni kutembelea mlima wa mwezi wenye mandhari ya kiasili na kuwafahamisha mila na desturi za kienyeji kwa lugha ya Kiingereza. Tabasamu yake na huduma nzuri anazotoa zimewapa wageni picha nzuri sana, hivyo amesifiwa kuwa "mama wa mwezi".

    Mama Xu Xiuzhen hajawahi kusoma sana, alisoma shule kwa miaka mitatu tu, lakini alikuwa anajitahidi sana kujiendeleza na kuboresha maisha ya familia yake. Miaka kadhaa iliyopita, kutokana na kuongezeka kwa watalii waliomiminikia maskani yake kwa matembezi, mama Xu alianza kuuza vinywaji . Baada ya kukutana mara kwa mara na watalii kutoka nchi za nje, aliona umuhimu wa kujifunza lugha ya kigeni. Hivyo kuanzia mwaka 1997, kila siku alijifunza neno moja au sentensi moja ya Kiingereza kutoka kwa wageni wa nchi mbalimbali, halafu alikariri neno hilo mara kwa mara mpaka kuliweka akilini. Kidogo kidogo hujaza kibaba. Baada ya jitihada za miaka michache, mama Xu Xiuzhen aliweza kuzungumza na wageni kutoka ng'ambo. Wakati biashara yake ya kuuza vinywaji ilipoendelea vizuri, wanakijiji wenzake wengi pia walifanya biashara hiyo. Kuona hivyo, mama Xu Xiuzhen aliacha kuuza vinywaji, badala yake alijifanya kuwa kiongozi wa watalii wageni kwani anaona kuwa anajua kuongea kwa Kiingereza na wageni.

    Saa kumi na mbili ya kila alfajiri, mama Xu Xiuzhen anaamka na kufanya kazi shambani, kufikia saa tatu hivi, akibeba sanduku la vinywaji anaanza kupokea watalii wageni wanaokuja kuutembelea mlima wa mwezi. Kwa kawaida yeye hujitambulisha kwa kuwaonyesha wageni madaftari yaliyoandikwa maneno ya kumsifu kwa uchangamfu wake na huduma yake nzuri. Ili wageni wakubali awe kiongozi wao, yeye huwaongoza kupanda mlima . Wanapofika kileleni, yeye huwapa wageni vinywaji alivyobeba. Tofauti na viongozi wengine, yeye kwanza huwaongoza watalii kutembelea mlimani, kuingia katika mitaa ya kijiji kujionea maisha halisi ya wanavijiji wa huko, kisha kuwaalika nyumbani kwake kwa chakula cha kienyeji. Wageni waliozoea chakula cha mtindo wa kimagharibi wanapenda sana vitoweo alivyopika. Baada ya chakula ,yeye huwaomba wageni kuandika maneno machache kuhusu huduma yake katika daftari. Kutokana na huduma bora anayoitoa na kutaka gharama ndogo, uongozaji wake huwafurahisha sana watalii wengi. Baada ya miaka kadhaa, amelimbikiza madaftari matano yaliyoandikwa maneno ya kumsifu.

    Katika majira ya joto ya mwaka 1997, siku moja wakati mama Xu Xiuzhen aliposhuka chini kutoka mlima wa mwezi, alimwona msichana kutoka Australia aliyeitwa Denny akiketi katika ngazi, akikumbatia tumbo lake huku akitokwa jasho jingi, alionekana kuumwa sana. Mama Xu Xiuzhen baada ya kufahamishwa hali yake ya ugonjwa, alimbeba Denny aliyekuwa mzito kuliko yeye mwenyewe, na kumpeleka hadi hospitalini, halafu alirudi nyumbani bila kuacha neno lolote. Asubuhi ya siku ya tatu, msichana Denny akisaidiwa na wenyeji, alimtafuta mama Xu Xiuzhen hadi nyumbani kwake kwa ajili ya kumshukuru. Mama Xu Xiuzhen aliongea vizuri kwa Kiingereza na Denny na kumwalika kupumzika nyumbani kwake kwa siku mbili. Denny alipoondoka alimwambia mama Xu Xiuzhen kuwa, "mimi nataka kukuita mama, wewe kweli ni mama wa mwezi mwenye moyo mkunjufu sana." Kisha Denny aliandika maneno ya shukrani kwenye ukurasa mzima wa daftari ya mama Xu. Baada ya kurudi Australia, Denny alimwandikia barua mama Xu Xiuzhen mara kwa mara.

    Kuanzia hapo, sifa yake ya "mama wa mwezi" ilivuma sana, watalii wageni wanaokwenda Yangsuo humtafuta "mama wa mwezi". Mtalii mmoja kutoka Ufaransa baada ya kupokea huduma yake nzuri, aliandika maneno : "Kama ukija Yangsuo, mtafute mama wa mwezi awe kiongozi wako. Yeye ni mtu mwaminifu sana, ni mtu mwenye sifa bora. Atakutembeza mahali pazuri kwa gharama ndogo tu."

    Sasa mama Xu Xiuzhen amejenga nyumba yenye orofa mbili kutokana na kazi ya kuwaongoza watalii. Chini ya uongozi wake, katika kijiji cha Liechun chenye idadi ya watu 400, wakazi 100 wa huko wanajishughulisha na biashara ya utalii.

Idhaa ya Kiswahili 2004-05-25