Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2004-05-27 22:22:32    
Ujenzi wa reli unaoendelea nchini China

cri
    Sasa ni miaka miwili na nusu tangu reli kati ya mikoa ya Qinghai na Tibet kuanza kujengwa. Hivi sasa reli kati ya Qinghai na Tibet imeshapita kwenye mlango wa mlima wa Tanggula wenye urefu wa zaidi ya mita 5,000 kutoka usawa wa bahari na kuingia mkoani Tibet. Reli kati ya Qinghai na Tibet ni mojawapo miongoni mwa miradi mikubwa inayojengwa katika miaka ya karibuni nchini China kwa ajili ya kustawisha uchumi wa sehemu ya magharibi. Reli hiyo itachangia sana maendeleo ya uchumi wa sehemu ya Tibet na kuimarisha uhusiano wa kiuchumi na kibiashara kati ya Tibet na mikoa mingine ya China.

    Reli kati ya Qinghai na Tibet iliyoko katika sehemu ya magharibi ya China, inaanzia mji wa Xining, mkoani Qinghai, hadi mji wa Lhasa, mkoani Tibet. Toka miaka ya 50 ya karne iliyopita, China ilinuia kujenga reli moja kutoka sehemu ya China bara iendayo Tibet. Ujenzi wa kipindi cha kwanza cha reli hiyo ambacho ni reli kati ya miji ya Xining na Geermu, mkoani Qinghai ulizinduliwa rasmi mwaka 1974 na ulikamilika mwaka 1984 ambapo ujenzi wa kipindi cha pili cha reli yenye urefu wa kilomita 1,118 kati ya miji ya Geermu na Lhasa ulianza rasmi mwezi Juni mwaka 2001.

    Ujenzi wa reli kati ya Qinghai na Tibet ni hatua muhimu inayochukuliwa na China ya kustawisha sehemu ya magharibi na kusawazisha maendeleo ya uchumi ya sehemu mbali mbali. Mtafiti wa idara ya utafiti wa uchumi na jamii ya taasisi ya utafiti wa elimu ya Tibet ya China, Bw. Xu Ping anasema kuwa ujenzi wa reli kati ya Qinghai na Tibet utaleta athari kubwa kwa maendeleo ya Tibet, alisema, "Ujenzi wa reli kati ya Qinghai na Tibet ni jambo kubwa katika harakati za ustawishaji wa sehemu ya magharibi ambalo litaleta athari kubwa kwa maendeleo ya Tibet. Kimsingi, itatatua kabisa tatizo la mawasiliano ambapo vikwazo vya mawasiliano kati ya Tibet na mikoa mingine ya China bara vitaondolewa kabisa."

    Mkoa ujiendeshao wa Tibet uko katika sehemu ya mpakani, kusini magharibi ya China ambao ni mkoa pekee usio na njia ya reli hapa nchini. Mawasiliano finyu na miundo mbinu hafifu vilikwamisha maendeleo ya uchumi wa Tibet. Katika muda mrefu uliopita, rasilimali za madini na mazao ya kilimo na mifugo ya Tibet havikuweza kusafirishwa kwa sehemu nyingine, na gharama ya usafirishaji wa bidhaa za viwanda na vitu vinavyohitajiwa katika maisha ya watu ilikuwa kubwa, hali ambayo ilisababisha maendeleo ya uchumi wa Tibet kuwa nyuma yakilinganishwa na mikoa mingine ya China.

    Hivi sasa vitu vyote vinavyohitajiwa na Tibet vinasafirishwa huko kwa magari, ingawa kuna barabara 4 ziendazo Tibet katika China bara, lakini iko barabara moja tu kati ya Qinghai na Tibet inayoweza kusafirisha mizigo bila kuathiriwa na hali ya hewa na vikwazo vingi vya ardhini, hivyo kazi za uchukuzi za barabara hiyo zimekuwa nyingi siku hata siku ambapo hivi sasa, zaidi ya 80% ya mizigo inasafirishwa huko kwa njia ya barabara. Hivyo ujenzi wa reli kati ya Qinghai na Tibet utaleta ufanisi mkubwa wa kiuchumi na kijamii kwa kuimarisha uwezo wa uchukuzi na marekebisho ya mfumo wa uzalishaji mali.

    Habari zinasema kuwa baada ya ujenzi wa reli kati ya Qinghai na Tibet kukamilika, inleta nafasi nyingi kwa maendeleo ya sekta za rasilimali ya madini, wanyama na mimea adimu ya uwanda wa juu, utengenezaji wa vinywaji visivyo na uchafuzi, tiba na madawa ya kitibet, mazao ya kilimo na mifugo na vitu vya kazi za mikono vya kabila la kitibet. Bidhaa mbali mbali zenye umaalumu wa uwanda wa juu pia zitaweza kusafirishwa kwa sehemu mbali mbali kwa njia hiyo ya reli ambapo kupungua kwa gharama ya usafirishaji kutaweza kukuza nguvu ya ushindani ya rasilimali za Tibet katika masoko ya nchini na ulimwenguni, na kuvutia uwekezaji vitega uchumi kutoka nchi za nje. Pamoja na kukuzwa kwa uhusiano wa kiuchumi na kibiashara kati ya Tibet na sehemu za nje, utandawazi wa masoko ya Tibet pia utaweza kuendelezwa, na uchumi wa sehemu hiyo utahimizwa zaidi.

    Reli kati ya Qinghai na Tibet itafanya mawasiliano yawe rahisi na salama, ya raha na ya gharama ndogo zaidi kwa watalii, hali ambayo italeta ongezeko kubwa la watalii na kuendeleza mambo ya utalii ya Tibet. Profesa Li Zhu-qing wa taasisi ya uchumi wa makabila madogo madogo ya chuo kikuu cha makabila cha China alifafanua zaidi, "sehemu ya Tibet ni sehemu isiyofaa kwa uendelezaji wa viwanda vya kijadi, bali ni mwafaka kwa kukuza mambo ya utalii. Tibet ina rasilimali nyingi za kiasili za utalii na mandhari nzuri yenye kivutio kikubwa. Pili, Tiber ina utamaduni wenye umaalumu wa kijadi, hivyo utalii unaweza kuwa nguzo ya uchumi wake."

    Kujengwa reli kati ya Qinghai na Tibet kutachangia maendeleo ya sekta ya huduma ya Tibet, pamoja na ujenzi wa reli na vituo vya treni, miji mingi itaanzishwa ambayo itatoa ajira nyingi mpya.

    Katika taarafa ya Liuwu iliyoko katika kiunga cha kaskazini mwa mji wa Lhasa, kijana aitwaya Dawa, baada ya kusikia kwamba kituo cha treni kitajengwa karibu na nyumba yake, alisema kuwa atajenga hoteli moja karibu na huko ili kupata pesa nyingi zaidi na kuishi maisha ya kama wakazi wa mjini. Mzee mmoja wa kabila la watibet alisema kuwa anataka kupanda treni kutembelea Beijing, kwani angeweza kuburudishwa na mandhari ya kando kando ya reli.

    Ukweli ni kwamba hata kabla ya ujenzi wa reli kukamilika, sehemu za ujenzi wa reli zilikuwa zimeleta manufaa kwa wakazi wa huko. Habari zinasema kuwa wenyeji wa huko wanauza vifaa vya ujenzi na vyakula kwa makampuni ya ujenzi, wakulima na wafugaji wengi wa huko waliajiriwa katika ujenzi wa reli, inakadiriwa kwamba mwaka 2003 Tibet itaweza kuwa na pato la Yuan zaidi ya milioni 300. Bw. Xu Ping kutoka taasisi ya utafiti wa jamii na uchumi ya kituo cha utafiti wa elimu ya Tibet cha China alisema, "Ujenzi wa reli kati ya Qinghai na Tibet umechangia moja kwa moja maendeleo ya uchumi wa Tibet na kuleta ajira nyingi kwa wakulima na wafugaji wa huko. Hadi hivi sasa kiasi cha wakulima na wafugaji elfu 6 hadi elfu 10 wanashiriki katika ujenzi wa reli hiyo. Inakadiriwa kwamba toka mwaka 2002 hadi mwaka 2003, wenyeji wa huko wameongezewa pato la Yuan zaidi ya milioni 100 kutokana na vibarua.

Idhaa ya Kiswahili 2004-05-27