Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2004-06-03 19:44:47    
Maisha ya wakazi wa Shanghai,China

cri

   Sehemu ya Waitang iliyoko magharibi ya mto Huangpu ni mahali muhimu kwa wakazi wa Shanghai. Sehemu hiyo yenye mandhari nzuri na majengo mengi yenye mtindo wa kimagharibi, kila siku panawavutia watalii wengi wa nchini China na nchi za nje.

    Kila mara mwandishi wetu wa habari akienda Shanghai kwa matembezi huwa anahisi kwamba, Shanghai ni mji unaofuata sana mkondo wa kimataifa. Wafanyakazi wa soko la hisa wanapasha habari bila kusita kuhusu hali ya hisa inayobadilika kwa haraka, majengo yenye mitindo mizuri yanachomoza kila baada ya muda mfupi, na mikutano ya aina mbalimbali ya kimataifa inafanyika katika kituo cha mikutano.

    Lakini wakazi wengi waliozaliwa mjini Shanghai wanapojaribu kufuata mabadiliko hayo, pia wanaendelea na desturi za maisha ya zamani.

    Katika sehemu ya Waitang kulikuwa na uzio wa matofali, katika miaka ya 70 hadi 80 ya karne iliyopita, vijana wachumba wengi wa Shanghai walipenda kukutana katika sehemu hiyo, hivyo uzio huo uliitwa "ukuta wa wachumba". Kila giza lilipoingia wachumba wawili wawili wakinong'onezana na kujazana katika eneo hilo la ukuta wa matofali. Kwa miaka mingi "ukuta wa wachumba" ulikuwa sehemu yenye mvuto huko Shanghai. Lakini hivi sasa ukuta huo wa matofali umebomolewa, na badala yake, umejengwa uzio wa chuma. Bibi Lu Xiuqing mwenye umri wa miaka 40 mwaka huu bado ana kumbukumbu nzuri ya maisha yake ya ujana.Kila akipita sehemu ya Waitang, huwa anahisi kama anakosa kitu.

    Kama wakazi wengine wengi wa Shanghai, Bibi lu anapenda vitu vinavyoweza kuonyesha Shanghai ya zamani. Alikuwa anaishi katika nyumba za kijadi zenye ua katikati, ambazo mlango wake mkuu ulijengwa kwa mawe marefu. Bibi Lu alisema kuwa, katika nyumba hizo za kijadi zenye ghorofa moja, zilikuwa na vyumba 8, kila familia iliishi katika chumba kimoja, lakini waliishi kwa furaha:

    "Nyumba za kijadi za Shanghai ni kama nyumba kubwa zenye ua, wakati wa joto, watu wote wa familia hizo huwa walipunga upepo pamoja uani, wakipashana habari za aina mbalimbali na kusimuliana hadithi zinazosisimua. Na watu wazima waliwafundisha watoto namna ya kujiheshimu."

    Sasa Shanghai bado kuna nyumba nyingi za kijadi zenye mtindo wa pekee wa Shanghai. Ukipanda juu ya mnara wa TV wa Dongfangmingzhu, utaona nyumba nyingi za kijadi zinazounagnishwa pamoja, na ukitaka kutafuta maisha yalivyo ya Shanghai, lazima uende kwenye nyumba hizo za kijadi: watu kumi kadhaa wanaingia na kutoka katika mlango mmoja,familia moja ikiwa na shida, wakazi wote wanajitokeza kutoa msaada; familia zote zinapika chakula katika jiko moja.

    Kufuatana na kupanuka kwa mji wa Shanghai, sehemu kubwa za mji mkongwe zimejengwa upya, na hivi sasa wakazi wengi wameagana na maisha ya nyumba za kijadi, na kuhamia katika majengo ya kisasa. Bwana Chen Deyu mwenye umri wa miaka 50 na zaidi mwaka huu aliagana na maisha ya nyumba za kijadi miaka kumi na zaidi iliyopita, na kuhamia katika mashariki ya mto Huangpu. Akishirikiana na wengine aliendesha kiwanda cha kutengeneza vyombo vya plastiki. Baada ya kupata uwezo mkubwa, alinunua nyumba 5 za majengo. Licha ya kukaa mwenyewe, nyumba nyingine nne amezipangisha kwa wageni,Alisema:

    "Baada ya mazingira kuboreshwa katika sehemu nilizoishi, naona kuwa, kununua nyumba ni chaguo kizuri. Sasa watu wengi wanakuja Shanghai kutafuta kazi na kuwekeza vitega uchumi, wote wanahitaji nyumba za kupangishwa. Kwa hivi sasa kila mwezi mapato yangu kutokana na kodi ya nyumba hizo nne ni yuan za renminbi elfu kumi."

    Wakazi wa Shanghai wanajua sana kusimamia mali zao. Bwana Chen alinunua nyumba moja kwa yuan za renminbi laki 4, na kuipangisha kwa yuan za renminbi elfu 3 kila mwezi, anaweza kurudisha gharama zake baada ya miaka kumi na kitu.

    Licha ya kupangisha nyumba, wakazi wa Shanghai sasa wanapenda sana kununua hisa, hata akina mama wazee wenye umri wa miaka 70 hivi wanatumia akiba yao ya pesa kununua hisa, na kila siku wanaenda sokoni kuangalia hali ya hisa.

    Baada ya kazi, Bwana Chen pia anajua kupika chakula,akirudi nyumbani huwa anaingia jikoni.Alisema:

    " Nikirudi nyumbani tu napenda kupika chakula, kama wakazi wengine wanaume wa Shanghai, mimi najua kupika chakula, najua jinsi ya kufanya shughuli nyumbani, kama vile kununua mboga, kupika chakula, na kufua nguo. Hii ni desturi kwa wakazi wa kiume wa Shanghai."

    Tofauti na wakazi wa sehemu nyingine, wanaume wa Shanghai wanapenda kupika chakula, wanajua jinsi ya kufanya shughuli za nyumbani, na jinsi ya kuwasaidia wake zao. Msichana akimpata mume kutoka Shanghai, maisha yake ya baadaye yatakuwa ya raha sana.

    Shanghai pia ni mji wa kisasa, wakazi wengine wanapenda kufuata maisha ya mtindo wa kisasa. Katika mtaa wa Xintiandi kuna baa nyingi zenye hali nzuri ya kimazingira, ambazo zilijengwa kwa mitindo tofauti ya nchi mbalimbali, utawakuta makarani na wawakilishi wa kampuni za nchi mbalimbali zilizoko mjini Shanghai .

    Katika mkahawa unaoendeshwa na mjerumani, mwandishi wetu wa habari alimkuta Bwana Nilsson kutoka Sweden, Bwana Nilsson alimwambia:

    "Kwa kweli mimi napenda sana kuishi mjini Shanghai, kwani Shanghai ni mji wa kisasa na wa kimataifa, na ni mji unaoendelea kwa haraka sana, maisha ya hapa ni ya kufurahisha. Sasa watu wengi kutoka nchi za magharibi wanataka kuja Shanghai kuwekeza vitega uchumi, au kufanya kazi. Hapa Shanghai naweza kuwakuta marafiki wengi kutoka nchi mbalimbali duniani, bila shaka maisha ya Shanghai ni ya mvuto kwangu."

    Katika miaka ya hivi karibuni, kutokana na mabadiliko makubwa yaliyotokea mjini Shanghai, wageni wengi kutoka nchi za nje kama Nilsson wamemiminikia Shanghai, na wamekuwa wakazi wapya wa Shanghai wenye rangi tofauti, lakini wote wanaupenda mji wa Shanghai. Katika miaka miwili iliyopita, mgeni kutoka Poland aliteuliwa kuwa balozi mwakilishi wa Tamasha la utalii wa kimataifa. Mwaka 2010, Shanghai itaendesha maonesho ya vitu ulimwenguni, wakati huo kama utaweza usisahau kuja Shanghai kujionea mwenyewe maisha ya Shanghai.

Idhaa ya Kiswahili 2004-06-03