Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2004-06-09 21:10:38    
Hifadhi ya urithi wa duniani nchini China

cri

    Mkutano wa 28 wa Urithi wa Dunia utafanyika mwezi Juni katika mji maarufu wa bustani, Suzhou, mashariki mwa China. Ofisa aliyehusika wa China alipohojiwa na waandishi wa habari alisema kuwa katika muda mrefu uliopita China imefanya juhudi kubwa nyingi bila kulegea katika hifadhi ya urithi wa dunia, na itachukua fursa ya mkutano huo kufanya juhudi kubwa zaidi kuimarisha hifadhi ya urithi wa dunia nchini China.

    China ni nchi tajiri kwa kuwa na kumbukumbu nyingi za kimaumbile na za utamaduni wa kale. Tangu China ijiunge na "Mkataba wa Urithi wa Dunia" mwaka 1985, inajitahidi kuomba kumbukumbu maarufu za utamaduni wa kale nchini China ziwe za urithi wa dunia. Hivi sasa kumbukumbu hizo zilizoorodheshwa kwenye "urithi wa dunia" zimefikia 29, na imekuwa nchi ya tatu yenye kumbukumbu nyingi ikifuatia Hispania na Italia, kumbukumbu hizo ni pamoja na Ukuta Mkuu, Bustani ya Summer Palace ya Beijing na Mji wa Kale mkoani Yunnan, Mlima Emei na Kasri la Potala mkoani Tibet.

    Mkuu wa Idara ya Taifa ya Hifadhi ya Kumbukumbu Bw. Zhang Bo aliwaambia waandishi wa habari kuwa China imechukua hatua nyingi mfululizo za kuhifadhi kumbukumbu za utamaduni. Anasema,

    "Serikali za mitaa tayari zimekamilisha mfumo wa kusimamia na kutunza urithi wa dunia na zimetenga fedha nyingi zaidi kwa ajili ya gharama za hifadhi na kutekeleza kanuni zilizowekwa kwa ajili ya usalama"

    Bw. Zhang aliongeza kusema kuwa China siku zote inatanguliza mbele kazi ya kuhifadhi urithi wa dunia. Hivi sasa China imetunga sheria na kuiweka kazi ya kuhifadhi urithi wa dunia chini ya sheria hiyo. Pamoja na kutekeleza sheria hiyo China pia inafanya uenezi wa elimu kuhusu namna ya kuhifadhi kisayansi na maana ya hifadhi hiyo, inajitahidi kuwaelimisha wananchi wawe na mawazo ya kutunza urithi huo, kazi hiyo imeungwa mkono na wananchi, na inasimamiwa na jamii nzima. Hivi sasa kumbukumbu za urithi wa dunia nchini China karibu zote zimepata hifadhi nzuri na haikutokea uharibifu.

    Bustani mjini Suzhou ni ya kale na ni urithi wa dunia. Mkutano wa 28 wa Urithi wa Dunia utafanyika huko, hii inamaanisha jamii ya kimataifa inaridhika na kazi ya hifadhi ya bustani hiyo nchini China. Mkurugenzi wa Idara ya Usimamizi wa Bustani ya Mji wa Suzhou Bw. Xu Wentao anatueleza,

    "Tumetunga sheria na kanuni kwa ajili ya hifadhi ya bustani yetu, sheria na kanuni hizo zimeanza kutekelezwa kuanzia mwaka 1997. Kazi zetu zote zinafanywa kwa mujibu wa sheria na kanuni hizo, na mandhari ya kale haikuharibika wala kubadilika."

    Ili kuyafanya mazingira nje ya bustani yalingane na mandhari ya bustani, majengo yasiyostahili katika eneo lenye mita za mraba 7,000 yalibomolewa, na kwa ajili ya kuzuia uharibifu unaosababishwa na idadi kubwa ya watalii bustanini kiingilio kimepanda juu.

    Ingawaje China imefanya juhudi nyingi katika hifadhi ya urithi wa dunia, lakini matatizo bado yapo. Sababu ni kuwa baadhi ya sehemu za vivutio zinaendelezwa zaidi kuliko uwezo wa sehemu hizo kuubeba. Baadhi ya sehemu zinazovutia utalii hazikufanya mpango wa makini na kujenga mandhari na majengo mengi yasiyostahiki ambayo yameharibu ukamilifu na asili ya uzuri wa urithi. Kuhusu hali hiyo mwakilishi wa UNESCO mjini Beijing Ms. Domenach-chich anasema,

    "Ingawa matatizo bado yapo katika usimamizi wa kuhifadhi urithi wa dunia na yanahitaji kuboreshwa zaidi, lakini UNESCO inasifu juhudi za China katika hifadhi ya urithi wa duniani ambao ni mali za binadamu wote, UNESCO itaendelea kuunga mkono juhudi za China katika utatuzi wa matatizo na usimamizi wake.

Idhaa ya Kiswahili 2004-06-09