Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2004-06-10 22:16:37    
Walinzi wa bendera ya taifa

cri
    Tarehe mosi, Octoba, mwaka 1949, kwa mara ya kwanza ilipandishwa bendera ya taifa la China, ambayo ni bendera nyekundu yenye nyota tano, kwenye uwanja wa Tiananmen, katikati ya mji mkuu Beijing. Na kuanzia hapo, jamhuri moja mpya ikaasisiwa. Hivi sasa, miaka 54 imepita. Bendera hiyo hupandishwa kila asubuhi na kushushwa kila jioni kwenye uwanja wa Tiananmen, ambapo kuna timu moja maalumu wa askari wanaoshughulikia kazi hiyo na kulinda bendera ya taifa. Leo nakuleteeni maelezo juu ya askari hao wanaojulikana kama walinzi wa bendera ya taifa. Karibuni. 

     Kila asubuhi, huoneshwa tukio sawa kwenye uwanja wa Tiananmen, katikati ya mji mkuu Beijing, ambapo kwa kufuatana na muziki ya kijeshi, askari 36 wanaovalia wakilinda bendera ya taifa, huwa wanatembea kwa hatua za gwaride mpaka msingi wa mhimili wa bendera ya taifa, halafu wakasimama katika pande mbili. Askari mmoja anayeshughulikia kupandisha bendera hukabidhiwa bendera ya taifa yenye urefu wa mita 5 na upana wa mita 3.3 kutoka kwa askari mwingine, na kuiweka kwenye zana ya kupandisha na kususha bendera. Ofisa anayeongoza timu hiyo huwa anatoa amri ya kupiga saluti, wimbo wa taifa ukaanza na askari akapiga swichi kuhu akitupa hewani bendera anayoshikilia. Kwa kufuatana na wimbo wa taifa la China, bendera nyekundu yenye nyota tano huenda juu kwa utaratibu mpaka kimo cha mhimili wenye mita 30, wakati ambapo jua huchomoza.

    Kila ifikapo sikukuu muhimu na tarehe msoi, 11 na 21 za kila mwezi, kuna bandi ya kijeshi yenye watu 60 ambayo hucheza wimbo wa taifa hapo hapo.

    Kila siku, watu wengi wanakusanya kwenye uwanja wa Tiananmen kwa ajili ya kushuhudia sherehe hiyo ya kupandisha bendera ya taifa. Sui Yongyu ni mwana mwenye umri wa miaka 6 mwaka huu, akifuatana na wazazi wake, aliwahi kutizama sherehe hiyo. Anakumbusha, akisema, (sauti 3) "Najivunia kwa kuwa Mchina. Pia nawapenda askari wanaopandisha bendera ya taifa, ningependa nikawa mlinzi wa bendera ya taifa siku nyingine."

    Timu hiyo maalumu ya walinzi wa bendera ya taifa ilianzishwa mwishoni mwa mwaka 1982, ambapo sherehe yenyewe ilikuwa rahisi. Mwaka 1990, sheria ya bendera ya taifa ikaanza kazi nchini China, ambayo iliweka bayana utaratibu wa kupandisha bendera ya taifa. Hapo mwanzoni, walikuwepo askari watatu pekee walioshughulikia kupandisha bendera, na kuanzia mwaka 1991, wakaongezwa ofisa mmoja na askari wengine 32 wanaolinda bendera ya taifa.

    Kwenye sherehe ya kupandisha bendera ya taifa, watu wanashangaa na jinsi askari hao wanavyofanya vitendo sawa wakionesha ushujaa na heshima. Lakini nyuma yake ni jasho kubwa, na si rahisi askari mmoja akawa mlinzi wa bendera ya taifa.

    Kila mwaka, makumi kadhaa ya askari wapya wanaojiunga na jeshi wanachaguliwa na timu ya walinzi wa bendera ya taifa, askari hao ni lazima wawe na urefu wa mita kati ya 1.8 na 1.9, na wanasimama moja kwa moja bila kupinda. Halafu askari hao wanapokea mazoezi ya kijeshi ya miezi mitatu, na wale wanaofaulu mtihani wa kwanza wanaendelea na mazoezi zaidi ya miezi minne kabla ya mtihani wa mwisho. Ni askari wanaofaulu mtihani huo ambao wakaingia katika timu ya walinzi wa bendera ya taifa. Mkuu wa timu hiyo Bw. Liu Jianguang akitoa maelezo, anasema, "Askari anayetaka kuwa mlinzi wa bendera ya taifa, anapaswa kupitia vizuizi vitatu, nazo ni namana ya kusimama, kushikilia bunduki na kutembea. Katika mazoezi, askari wanasimama wakiegemea ukuta na kukabiliana na upepo bila kufumba macho. Askari wengi wanafanya mazoezi kwa bidii kiasi ambacho zinajitokeza lengelenge za damu miguuni na sugu mikononi."

    Bw. Wu Meng ameshika kazi ya kupandisha bendera kwa karibu miaka miwili. Askari huyo kutoka mkoa Anhui, kusini mwa China ni mmojawapo wa washindi aliyechaguliwa kutoka askari wapya zaidi ya elfu moja. Mwanzoni alipoteuliwa kushughulikia kupandisha bendera ya taifa, alitumia miezi minne kwa kufanya mazoezi ya vitendo viwili tu vya kutupa bendera wakati wa kuipandisha na kuikusanya wakati wa kuishusha. Hivi sasa, anaweza kufanya vitendo hivyo kwa ustadi mkubwa, hata hivyo anatenda bila uzembe kila mara. Anasema, "Tunafanya mazoezi kwa saa 3 na zaidi kila siku, tunapumzika wakati wa adhuhuri. Mazoezi yananipeleka kuchoka, lakini nimezoea. Naona majivuno na fahari kubwa kwa kazi hiyo, nayo inastahili jasho langu."

    Timu ya walinzi wa bendera ya taifa ina nidhamu kali. Hata hivyo, maisha ya askari hao ni ya rangi mbalimbali, nao wengi ni vijana wa umri wa miaka 20 hivi. Katika mabwenini yao, mwandishi wetu anaona picha nyingi ambazo ni kumbukumbu za maisha yao, kama vile wanapocheza mpira wa kikapu na soka, wanapoburudishwa na muziki, na wanaposhiriki kwenye maonyesho ya nguo. Mbali na picha, katika meza ya kila askari, vitabu vya aina mbalimbali vinapangwa safi.

    Wakiwa askari, hawaruhusiwi kurudi nyumbani mara kwa mara. Askari wengi wa timu ya walinzi wa bendera ya taifa wamekuwa hawatembelei jamaa zao kwa miaka kadhaa. Kwa hivyo, wakati wa mapumziko, wanaandikia barua na kuwapigia simu familia yao. Kwa maoni yao, familia ni tegemeo imara nyuma yao inayowahimiza kupata maendeleo na kulihudumia taifa.

    Kila mwaka, kuna askari wapya wengi wanaotarajia kujiunga na timu hiyo ya walinzi wa bendera ya taifa, na pia wapo askari kongwe wanaotimiza muda zao za kulihudumia jeshi. Lakini kwenye uwanja wa Tiananmen, ulio katikati ya mji mkuu Beijing, kila siku watu wanashuhudia walinzi hao wa bendera ya taifa wakiwa na uchangamfu mkubwa, ambao wanaonesha uaminifu na wajibu, na hadhithi yao pia inaendelea.

    Wasikilizaji wapendwa, mlikuwa mkisikiliza maelezo kuhusu askari walinzi wa bendera ya taifa wanaoandaa sherehe ya kupandisha na kushusha bendera ya taifa la China kila siku, kwenye uwanja wa Tiananmen, katikati ya mji mkuu Beijing.

Idhaa ya Kiswahili 2004-06-10