Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2004-06-18 22:22:20    
Hekalu la Confucius

cri

    Confucius alikuwa mwanafilosofia, mwanasiasa na mwelimishaji mkubwa katika zama za Spring na Autumn yaani toka mwaka 770 hadi 475 K.K. nchini China. Katika miaka zaidi ya elfu moja iliyopita wafalme wote wa China walimwenzi sana Confucius na karibu kila mahali palikuwa hapakosi hekalu lale ili watu wamfanyie tambiko. Kati ya mahekalu yote, lililo kubwa zaidi ni hekalu lililojengwa katika maskani yake, Qufu, mkoani Shangdong. Ufahari wa jengo la hekalu hili hata laweza kulingana na Kasri ya Kifalme mjini Beijing. Yafuatayo ni maelezo kuhusu hekalu hilo.

    Hekalu la Confucius liko mjini Qufu mkoani Shandong, mashariki mwa China. Mwaka 478 K.K., mwaka wa pili baada ya Confucius kufariki, mfalme wa Dola la Lu aligeuza makazi ya Confuciua kuwa hekalu, na aliweka vitu alivyotumia Confucius ndani ya hekalu kama nguo, kofia na baadhi ya vyombo vya kutolea sadaka. Mfalme huyo kila mwaka alikwenda huko kufanya tambiko. Tokea hapo na kuendelea, kwa miaka zaidi ya elfu mbili, utamaduni ulioanzishwa na Confucius umezidi kuota mizizi katika ardhi ya utamaduni wa Kichina. wafalme wa kila enzi hawakusahau kujenga zaidi na kulifanya hekalu hilo kuwa lenye fungu kubwa la majengo. Katika karne ya 18 mfalme wa Enzi ya Qing aliamrisha kuongeza majengo mengi kupita enzi zote akatupatia hekalu la leo.

    Hekalu la Confucius lina urefu wa mita zaidi ya 1,000 kutoka kusini hadi kaskazini, eneo lake ni mita za mraba karibu laki moja, lina vyumba 500. Ujenzi wa hekalu hili ulitumia kiwango cha juu kabisa cha ufundi katika jamii ya umwinyi nchini China kwa kiwango cha ujenzi wa kasri ya kifalme. Majengo yake muhimu yanapangwa kwenye mstari wa katikati, na pande mbili za mstari huo, ni majengo mawili mawili ya kufanana na kukabiliana. Mpangilio huo wa ulinganifu wa majengo umeongeza utukufu na adhama. Ujenzi wa hekalu la Confucius ulitumia sana tarakimu 9. Mathalan, kuna nyua tisa mbele ya kumbi tisa, kati ya kumbi hizo ukumbi mkuu kwa jina la Dacheng una nafasi za vyumba tisa. Tisa ni namba kubwa kabisa miongoni mwa tarakimu moja. Katika jamii ya umwinyi nchini China "tisa" iliruhusiwa tu kutumika kwa ajili ya mfalme, hasa katika ujenzi, yeyote mwingine akitumia "tisa" atakatwa kichwa, lakini kwa hekalu la Confucius ilikukwa vingine. Kabla ya kufikia ukumbi mkuu wa Dacheng kuna milango mitano, ambayo kisheria milango mitano ya kuingilia ndani haikuruhusiwa kutumika katika ujenzi ila tu kasri ya kifalme. Lakini hekalu la Confucius lilijengwa kwa milango mitano, hii imeonesha heshima kubwa kwa Confucius sawa na mfalme.

    Kutokana na ujenzi usio wa kawaida wa hekalu hilo, tumeelewa kwamba Confucius alikuwa akiheshimiwa kama mfalme katika jamii ya umwinyi nchini China. Hii ni kwa sababu ya kuwa watawala wa China ya zamani walikuwa na haja na fikra zake kuitawala China.

    Ukumbi mkuu wa Dacheng ni mahali hasa pa kufanyia tambiko kwa Confuciua. Ukumbi huo una urefu wa kwenda juu mita 30 na upana kutoka mashariki hadi kaskazini ni zaidi ya mita 50, paa yake imeezekwa kwa vigae vya kauri ya njano, kwenye upenu wa ukumbi huo kuna nguzo 10 za mawe, ambazo juu ya kila nguzo wamechongwa dragoni waliouzungushia nguzo mawinguni. Kila nguzo ina urefu wa mita 6 na kipenyo karibu mita moja. Juu ya nguzo hizo kumi hakuna dragoni hata moja anayefanana na mwingine, chini ya mwanga wa jua kwa mbali dragoni waonekana kama wa kweli, ni michongo yenye thamani kubwa katika sanaa ya michongo ya kale ya China, hata imeshinda nguzo ndani ya kasri ya kifalme mjini Beijing. Inasemekana kwamba kila mfalme alipokwenda huko kufanya tambiko, nguzo hizo zilifungwa kwa kitambaa cha hariri nyekundu ili mfalme asikasirike iwapo akigundua kuwa kuna dragoni kwenye nguzo.

    Nyuma ya ukumbi mkuu wa Dacheng, kuna ukumbi mwingine wa kumkumbuka Confucius ambapo zilichongwa shughuli zake kwa michoro ya picha juu ya bamba za mawe zilizobandikwa ukutani zikionyesha maisha yote ya Confucius, jumla michoro ni 120 na kila mchoro una sentimita 40 kwa upana na sentimita 60 kwa urefu, michoro hiyo ni ya kwanza kabisa ya hadithi nchini China.

    Ndani ya hekalu hilo pia kuna minara ya mawe yenye maandishi zaidi ya 2000, na miongoni mwa minara hiyo, iko 50 iliyoandikwa na wafalme wenyewe, hii imeonesha kuwa Confucius alitukuzwa sana na wafalme katika jamii ya kimwinyi.

    Majengo ya hekalu la Confucius yanamaanisha watawala wa China ya kale jinsi walivyotukuza fikra za Confucius. Hivi leo, kwa sababu ya historia ndefu ya hekalu hili na utukufu wake wa ujenzi na vitu vivilivyohifadhiwa ndani, hekalu hili linasifiwa kuwa ni "Hekalu la Kwanza" la China. Mwaka 1994 hekalu hili limeorodheshwa na Unesco kwenye kumbukumbu za utamaduni wa dunia.

Idhaa ya Kiswahili 2004-06-18