Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2004-06-21 22:31:45    
Msomi Wang Shixiang

cri
    Tarehe 3 mwezi Desemba mwaka jana mwanamfalme wa Uholanzi Johan Friso kwa makusudi alikuja Beijing kumpatia tuzo msomi na mjuzi maarufu wa mambo ya kale Bw. Wang Shixiang tuzo ya "Sifa ya Juu Kabisa ya Mwanamfalme Claus" ya mwaka 2003 kutokana na mchango wake mkubwa katika utamaduni. Leo hii katika kipindi hiki nitawafahamisheni msomi huyo mwenye umri wa miaka karibu 90.

    Msomi Wang Shixiang alizaliwa mwaka 1914 katika familia ya afisa wa diplomasia. Mama yake alikuwa mchoraji mashuhuri. Utotoni mwake Wang Shixiang alipenda sana kucheza cheza. Mambo aliyocheza nayo yalikuwa mengi, aliwahi kuchezea nyenje, njiwa, mwewe, na vile vile alifurahia samani za Enzi ya Ming, enzi ambayo ilianzia mwaka 1368 hadi 1644. Hayo yote aliyapenda sio tu kwa ajili ya burudani bali kwa kweli aliyapenda kutoka rohoni mwake. Ili apate kitu alichopenda alitumia pesa nyingi na muda mwingi. Katika kujipatia ujuzi alijenga urafiki na watu kutoka fani mbalimbali na akiwa mnyenyekevu mwenye kuuliza uliza. Siku nenda siku rudi akawa mjuzi wa mambo aliyocheza nayo. Alisema,

    "Toka nilipokuwa shule ya msingi hadi chuo kikuu karibu miaka yote niliipitisha katika michezo, mambo niliyoyacheza yalikuwa mengi mno, kama kufuga mbwa, kukamata vicheche wakati usiku kwenye makaburi, na nilifuga njiwa, hata nilipofika chuo kikuu sikuacha michezo yangu. Lakini tokea mwaka 1939 mama yangu alipofariki, ghafla tabia yangu hiyo ikabadilika, mwaka huo ndipo nilipohitimu katika chuo kikuu. Niliona kuwa sitafanikiwa lolote iwapo nitaendelea kuwa hivyo. Basi tokea hapo nikajizamisha katika kazi, nikawa kama mtu mwingine kabisa."

    Kutokana na familia yake iliyokuwa ya wasomi, Bw. Wang Shixiang alilelewa kwa kupata elimu nyingi kuhusu utamaduni, historia, mashairi ya kale, muziki na uchoraji. Baada ya kuhitimu masomo ya chuo kikuu Bw. Wang Shixian alianza kazi ya utafiti.

    Mwaka 1946 wavamizi wa Japani walishindwa katika vita vya vya kuivamia China, Wang Shixiang aliajiriwa na kufanya kazi katika makumbusho ya kasri la kifalme kuokoa vitu vya kale vilivyochukuliwa kiholela wakati wa vurugu za vita. Katika muda huo alikuwa akipiga mbio huku na kule akaviokoa vitu vya kale zaidi ya 2,000. Na kwa miongo kadhaa kwa nyakti tofauti aliwahi kufanya kazi katika taasisi ya muziki wa Kichina, Idara ya Taifa ya Vitu vya Kale ya China, taasisi ya fasihi na historia ya China, na aliandika maandishi mengi ya taaluma yenye mawazo mapya.

    Bw. Wang Shixiang alianza kuthaminiwa tena baada ya China kuanza kufanya mageuzi na kufungua mlango kiuchumi. Mwaka 1981, alichapisha kitabu chake "Utafiti wa Samani za Enzi ya Ming", hiki ni kitabu alichojitayarisha kwa miaka zaidi ya 40, kina picha mia kadhaa, hadi kufikia mwaka 1988 kitabu hiki kilitafsiriwa katika nchi za Uingereza, Marekani, Thailand n.k. kwa lugha za Kiingereza, Kifaransa, Kijerumani n.k. lugha 9 kwa jumla na kuwa kitabu chenye taathira kubwa kabisa baada ya China kuanza kufanya mageuzi, na kimesababisha homa kwa wakusanyaji wa kimataifa wa samani za Enzi ya Ming.

    Kwa kuwa Bw. Wang Shixiang ana elimu ya pande nyingi, aliwahi kuchapisha vitabu zaidi ya 30, vikiwemo vitabu vya "Faharasa ya Muziki wa Kale wa China", "Usanii wa Uchongaji wa Mianzi", "Utafiti wa Samani za Enzi ya Ming" n.k. Vitabu hivyo vimeziba pengo la vitabu vya utafiti katika utamaduni wa asili na ni matunda ya jasho lake la miongo kadhaa. Miongoni mwa vitabu hivyo, vingi zaidi viliandikwa katika miaka ya 60 na 70 ambapo mazingira ya kisiasa yalikuwa mabaya kwa sababu ya mapinduzi ya utamaduni. Bw. Wang Shixiang alisema,

    "Vitabu nilivyoandika vilikuwa havithaminiwi katika miaka ya 60 na 70 kutokana na dhana potofu zilizoshamiri katika jamii miaka ile. Lakini nilikuwa na uhakika kuwa vitapokelewa baadaye, na sasa kweli vimetambuliwa kuwa ni vitabu muhimu ulimwenguni. Si muda mrefu baada ya China kuanza kufanya mageuzi ya kiuchumi, nilichaguliwa kuwa mwanachama wa Halmashauri Kuu ya Baraza la Mashauriano ya Kisiasa, kisha niliendelea na kazi yangu kwa zaidi ya miaka 20, jumla nilifanya utafiti katika taaluma yangu kwa miaka 50."

    Bw.Wang Shixiang pia alijitahidi kutumia mjuda wake na mapumziko kukusanya vitu alivyovipenda. Kutokana na elimu yake kubwa, vitu alivyovikusanya vilikuwa vya thamani kubwa. Si muda mrefu uliopita kwenye mkutano wa mnada aliuza vitu vyake 143 kwa RMB yuan milioni 63 kiasi cha dola za Marekani milioni 7 na laki 7. Kinanda cha kale cha Kichina cha karne ya 10 alikiuza kwa yuan milioni 9 kiasi cha dola za Marekani milioni moja na laki moja, hii ni ghali kabisa katika mauzo ya vitu vya kale. Kuhusu hilo Wang Shixiang alituambia kwa utulivu na unyekekevu,

    "Kwa kweli mimi sio mkusanyaji wa vitu vya kale, mkusanyaji lazima awe tajiri. Hii ndio sababu ya kuwa mimi sikusanya vyombo vya kauri, picha za kuchorwa, vyombo vya shaba nyeusi, kwa sababu vitu kama hivi ni aghali, sijihusishi navyo, kwa hiyo mbele ya wakusanyaji wakubwa mimi ni kabwera tu."

    Bw. Wang Shixiang ana masikitiko mengi maishani mwake, lakini lililo kubwa kabisa ni kwamba mwezi uliopita mkewe aliyekuwa mwandani wake alifariki. Mke wake pia alikuwa msomi mwenye elimu tofauti tofauti. Miaka kadhaa iliyopita Wang Shexiang alichagua baadhi ya makala za mkewe na kuhariri kuwa kitabu kimoja. Kitabu hicho ilinunuliwa sana na wasomaji, ndani yake kuna picha zaidi ya 200 alizochora mkewe. Kitu kilichomfariji ni kuwa kabla ya mkewe hajaaga dunia alikuwa amefahamu kuwa Wang Shixiang amepata tuzo ya "Sifa za Juu Kabisa za Mwanamfalme Claus" wa Uholanzi, na walikuwa wamekubaliana kwamba pesa zote alizopewa Euro laki moja watazitoa kwa ajili ya kusaidia watoto wenye shida za masomo.

Idhaa ya Kiswahili 2004-06-21