Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2004-06-22 22:27:06    
Barua za wasikilizaji 22/6/2004

cri
     Msikilizaji wetu Mbarouk Msabah P.O.BOX 52483 Dubai, Falme za Kiarabu anasema katika barua yake kuwa kwanza angependa kutupa pongezi zake za dhati kutokana na makala maalumu tulizozitangaza mwezi Mei mwaka huu katika kipindi cha Sanduku la Barua, ambazo baadhi zilihusu mahojiano tuliyofanya na waziri kiongozi wa Zanzibar mheshimiwa Shamsi Vuai Nahodha alipokuwa zirani nchini China.

    Anasema kwa kweli maelezo aliyotoa mheshimiwa Nahodha kuhusu maendeleo makubwa yaliokwishafikiwa na Jamhuri ya Watu wa China katika ziara yake hiyo, yamewadhihirishia wasikilizaji hali halisi ya juhudi zinazoendelea kuchukuliwa na umma mkubwa wa wananchi wa Tanzania katika kustawisha maendeleo ya kiuchumi, kisayansi, kijamii pamoja na kuwa kama ni mfano mzuri unaopaswa kuigwa na mataifa mengine yanayoendelea kama vile Tanzania.

    Bwana Msabah anasema bila shaka yoyote mheshimiwa Nahodha alijifunza mengi katika ziara yake hiyo nchini China, ambayo kama kiongozi wa juu visiwani Zanzibar, anapaswa kuyatumia kama ni kigezo kinachostahiki kuigwa na umma wa wawazanzibari na Tanzania kwa ujumla, katika kuboresha maendeleo ya kiuchumi na kijamii. Ni wazi kabisa watanzania wana mengi sana ya kujifunza kutoka Jamhuri ya Watu wa China katika kujikwamua kutoka katika hali duni ya kimaendeleo.

    Pia ansema ni jambo la kusikitisha sana kuona viwanda vya sukari huko Mahonda na kile cha viatu huko Maruhubi visiwani Zanzibar, vilivyojengwa kwa msaada wa Jamhuri ya Watu wa China katika miaka ya sabini, vimesimamisha uzalishaji wake kwa muda mrefu sasa na kubakia kama ni magofu matupu tu.

    Hata hivyo ana imani kubwa kwamba, China bado ina moyo wa dhati wa kuisaidia Zanzibar kuinua hali ya uchumi na kuboresha maendeleo ya kijamii, kwani ziara kama hiyo aliyoifanya Mheshimiwa Nahodha zinaweza kutoa changamoto kubwa kwa viongozi nchini Tanzania katika kuharakisha ujenzi wa taifa.

    Msikilizaji wetu Kilulu Kulwa P.O.BOX 161, Bariadi, Shinyanga, Tanzania ameandika barua barua mbili ya kwanza inaanza kwa pongezi zake kwa wahariri na watangazaji wote wa Idhaa ya Kiswahili ya Radio China Kimataifa, akitaka tupokee salaamu nyingi kutoka huko Tanzania. Anatuambia yeye ni mzima na anaendelea na shughuli za ujenzi wa taifa la Tanzania, pamoja na kusikiliza vipindi na matangazo ya Radio China Kimatafia.

    Anasema anapenda kutumia nafasi hii kutoa shukurani zake kutokana na vipindi vinavyorushwa na idhaa ya kiswahili ya Radio China Kimataifa ambavyo kwa hakika vimekuwa vikitoa elimu ya mambo mengi yanayohusu China na ulimwengu mzima. Anasema wao wasikilizaji wanaahidi kuendelea kuitegea sikio Radio China Kimataifa kila siku inapokuwa hewani.

    Pia bwana Kula anaelezea furaha yake kuwa, tangu tarehe 26 mwezi Decemba mwaka jana Idhaa ya Kiswahili ya CRI ilipoanzisha mpango maalumu ambapo vipindi na matangazo yake yanaweza kupatikana kwa njia ya mtandao wa Internet kwenye tovuti ya www.cri.cn, na msikilizaji au mtazamaji anapochagua Kiswahili basi bila shaka anavipata vipindi vya Idhaa ya Kiswahili ya Radio China Kimataifa . Anasema hayo ni maendeleo na mafanikio makubwa kwa Radio China Kimataifa, kwa juhudi zake za kutaka kuwafikia zaidi wasikilizaji wake, anasema tena pongezi kwa Radio China Kimataifa.

    Zaidi ya hayo anasema anapenda atoe shukrani zake nyingi kwa watayarishaji wa kipindi cha sanduku la barua mtangazaji Chen na bwana Fadhili Mpunji kutokana na kipindi cha tarehe 11 mwezi Aprili mwaka huu wa 2004. Katika kipindi hicho tulinukuu barua ya bwana Kulwa kitu ambacho anasema kilimtia moyo sana na vilevile alizidi kutambua wazi kwamba Radio China Kimataifa inawashirikisha wasikilizaji wake kwa ukamilifu.

    Anasema anapenda kutujulisha kuwa katika siku zijazo atatutumia barua na ripoti ya usikilizaji wa vipindi na matangazo yetu, ikiwemo makala kuhusu miaka 40 ya uhusiano wa kibalozi kati ya Jamhuri ya Watu wa China na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambapo urafiki na undugu baina ya nchi zetu mbili umeendelea kustawi siku hadi siku bila kusita. Hili ni jambo la kujivuna sana kwa wananchi wote wa pande zote mbili pamoja na serikali zake. Anasema ni matumaini yake kuwa ushirikiano huo wa kindugu utaendelea kustawi na kudumu siku.

    Katika barua yake ya kwanza bwana Kulwa anamakiza kwa kusema kuwa atafurahi sana kama tutazidi kuwasiliana kwa njia ya radio na barua. Vilevile atawashukuru kama mtakuwa na utaratibu wa kuwatumia vitabu wasikilizaji vinavyoeleza mambo mbalimbali kuhusu maendeleo ya China.Baada ya kupata Barua kutoka kwa Bwana Kulwa, kama kawaida yetu tuliijibu haraka, bwana kulwa naye bila kuchelewa akatuandikia barua nuyingine.

   Katika barua yake ya pili anasema anafuraha kuandika barua kwa wahariri na watangazaji wa Idhaa ya Kiswahili ya Radio China Kimataifa, na anapenda kutujulisha kuwa ni hivi karibuni tu amepokea bahasha mbili tulizomtumia zikiwa na barua za kuvutia na kusisimua sana, ambazo pamoja na mambo mengine tulinimjulisha kwamba maelezo na taarifa kuhusu klabu yao ya wasikilizaji ya Bariadi tumeipokea na kwamba tumevutiwa sana na taarifa hiyo inayojumuisha wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili ya Radio China Kimataifa.

    Vilevile katika bahasha hizo anatuambia kuwa alipokea zawadi tulizomtumia ikiwa ni pamoja na magazeti mawili pamoja na bahasha zilizokwishalipiwa gharama ya posta. Magazeti hayo ni China Today na China Pictorial ambayo yana habari motomoto kuhusu mambo mbalimbali yanayohusu China yakiwemo masuala ya uchumi, sayansi na utamaduni. Anasema kwa kweli amefarijika sana kutokana na barua hizo tulizonitumia zikiambatana na zawadi za magazeti.

    Pia anasema kuwa barua nyingine tuliyomtumia ilisifu sana mchango na ushirikiano anaouonesha yeye na wasikilizaji wengine kwa kuandika barua mara kwa mara na kutoa maoni mashauri na mapendekezo mbalimbali, ili kuboresha vipindi vyetu vya radio kwa matangazo yanayoelekezwa katika nchi za Afrika mashariki na kati na kwingineko, ambako Kiswahili kinasikika na kueleweka. Anasema katika barua hiyo tumemualika kuendelea kutuandikia barua ili kuzidisha na kukuza urafiki ambao tumeuanzisha tangu siku nyingi.

    Mwisho anasema anapenda kutueleza na kutuhakikishia kwamba tusiwe na shaka yoyote, kwani akiwa mmoja wa wasikilizaji wetu wa kudumu wa Radio China Kimataifa na rafiki wa China, ataendelea kuwasiliana nasi kila mara na kutupa habari kuhusu usikilizaji wake wa matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya Radio China Kimataifa.

Idhaa ya Kiswahili 2004-06-22