Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2004-06-23 21:45:40    
Majadiliano kuhusu suala la kuhifadhi wanyama pori au kuhifadhi maslahi ya wananchi nchini Kenya

cri

    Kenya nchi iliyoko Afrika ya Mashariki imebarikiwa kuwa na utajiri mkubwa wa wanyama pori. Sheria kali za kuwahifadhi wanyama zimeziwezesha sehemu nyingi za nchi hiyo ziwe ni mahali pazuri pa kuishi kwa wanyama pori. Lakini kuwahifadhi wanyama pori kumeathiri maslahi ya wakazi wa huko, kwani wamepata hasara kubwa ya mali na hata kupoteza maisha yao. Kipi ni muhimu zaidi, kuwahifadhi wanyama pori au kuhifadhi maslahi ya wananchi? Au kwa maneno mengine, vipi tunaweza kuzingatia mambo hayo yote?

    Siku za karibuni, maofisa, wataalamu wa kuhifadhi wanyama pori, wawakilishi wa wakazi waishio karibu na hifadhi za taifa na wawakilishi wa mashirika yasiyo ya kiserikali walijikusanya mjini Mombasa, Kenya, na kuanzisha majadiliano kuhusu suala la kuwahifadhi wanyama au kuhifadhi maslahi ya wananchi. Kwa serikali ya Kenya, kutatua suala hilo kuna maana kubwa kwa uchumi wa taifa na maisha ya wananchi.

    Kenya iliondoa utawala wa kikoloni wa Uingereza na kujipatia uhuru mwaka 1963. wakati huo, uwindaji haramu ulikuwa unahatarisha maisha ya wanyama wengi adimu kama vile tembo na vifaru. Kutokana na hali hiyo, serikali ya Kenya ilitunga sheria kali ya kuwahifadhi wanyama, na kuanzisha mbuga nyingi za wanyama na hifadhi za taifa.

    Lakini mpaka sasa, jumla ya eneo hilo ni asilimia 8 tu ya eneo zima la nchi hiyo. Asilimia 70 ya wanyama bado wanaishi nje ya hifadhi hizo. Hivyo, huwaletea hasara wakazi waishio karibu nao, na si rahisi kuwazuia.

    Kwa mfano, mwezi Juni, mwaka 2002, katika sehemu ya Voi iliyoko kusini mashariki mwa Kenya, simba wenye njaa waliwaua kondoo 54. Isitoshe, kila mwaka nchini Kenya kwa wastani watu makumi kadhaa huuawa na wanyama. Lakini ili kuhifadhi wanyama, sheria za Kenya zimeweka vikwazo vingi ambavyo watu hawawezi kuwauwa wanyama hao wanaowaletea hasara kubwa ya mali na miili yao, na ruzuku yanayotolewa na serikali kwa jamaa za watu waliouwa ni madogo sana. Miaka ya karibuni, hali hiyo imeboreshwa kwa kiasi, lakini bado haiwezi kuwaridhisha watu.

    Kwa upande mwingine, ingawa sheria kali inaweza kuzuia uwindaji haramu, lakini vilevile imeleta matokeo kadhaa mabaya. Tokeo moja ni kuwa idadi ya wanyama katika hifadhi kadhaa inaongezeka kwa kiasi kikubwa, na kupita uwezo wa mazingira na kuharibu uwiano wa kimaumbile. Lakini kupunguza idadi ya wanyama ili kuhifadhi uwiano wa kimaumbile kumepigwa marufuku kisheria. Hivyo jambo hilo linahitilafu.

    Utalii wa Kenya unaojulikana duniani kwa utajiri mkubwa wa wanyama pori umekuwa nguzo inayoweza kustawisha uchumi wa taifa hilo. Umekuwa chanzo muhimu kabisa cha kuingiza fedha za kigeni, na ni muhimu katika kutatua tatizo la ajira nchini humo. Mwaka 2003, utalii uliipatia Kenya mapato ya shilingi bilioni 24, sawa na dola za kimarekani milioni mia 3. Asilimia 10 ya Pato Kuu la Taifa linatoka sekta ya utalii, lakini asilimia 70 ya wakazi waishio na wanyama nadra wanapata faida hizo zinazoletwa na kuwepo kwa wanyama hao.

    Kwa mfano, mwaka 1988, katika hifadhi ya taifa ya Masai Mara, mapato kutokana na utalii lilikuwa dola za kimarekani milioni 26, lakini wamasai wa huko walipata asilimia 1 tu ya mapato hayo. Makampuni ya utalii yalipata asilimia 45, mahoteli yalipata asilimia 35. Hali hiyo si nadra nchini Kenya. Katika utaratibu huo wa kugawa mapato, bila shaka wakazi wa huko hawataki kuwahifadhi wanyama hao waishio katika ardhi yao, na wanawachukiza sana.

    Mkurugenzi wa Idara ya kuhifadhi wanyama pori ya Kenya (KWS) Bw. Evans Mukolwe alieleza kuwa, "Kwa kweli sheria inayotekelezwa hivi sasa inapendelea wanyama." Mbunge Leshore Sammy anaona kuwa, siasa hiyo lazima irekebishwe. Na maofisa wa idara ya utalii ya Kenya pia wamesema kuwa, watasukuma mbele maendeleo ya utalii kwa msingi wa jamii, ili kuongeza mapato ya wakazi.

    Kwa ujumla, kuhifadhi wanyama na kuhifadhi maslahi ya wananchi vyote lazima vitiliwe maanani. Suala muhimu kabisa ni kutafuta uwiano kati ya mambo hayo mawili. Likitatuliwa vizuri, basi Kenya itaweza kuendelea kuwa mahali pazuri pa kuishi kwa wanyama pori, na wanyama pori wataweza kuendelea kuwapatia maslahi wananchi wa Kenya.

Idhaa ya Kiswahili 2004-06-23